Binti mkubwa wa Mwalimu Nyerere asiye na makuu

 

Nimepanda daladala eneo la Posta, Dar es Salaam nikienda Kawe. Muda ni jioni, na kwa sababu hiyo abiria tumebanana kweli kweli.

Tunapofika katika kituo cha Palm Beach, kondakta anamtaka dereva asimamishe gari – aongeze abiria. Sisi tuliomo ndani tunalalamika. Tunahoji hao abiria wengine watakaa au kusimama wapi? Kondakta kwa jeuri, anajibu: “Inajaa ndoo ya maji, gari halijai.”

Foleni za jioni ni kali kweli kweli. Magari yanasogea polepole. Foleni inayoanzia Drive Inn hadi hapa Msasani Bonde la Mpunga, inatisha; lakini abiria hatuna namna ya kukwepa adha hii.

Taratibu, tunakwenda hadi kituo kinachoitwa ‘Kwa Mwalimu’. Wengine wanakiita ‘Kwa Baba wa Taifa’. Hapo yule mama mwembamba aliyevaa kilemba, anaomba kushuka.

Naam! Ameshashuka. Abiria mwenzetu kwa kuona yule mama ameshaanza kuvuka kwenda upande wa pili wa barabara, anasema: “Mnamuona binti wa Nyerere?” Abiria, kama walioambizana, wanahoji kwa pamoja: “Yuko wapi?”

Yule abiria anasema: “Huyo anayevuka barabara, si tulikuwa naye humu?” Maneno ya huyu abiria mwenzetu yanaonekana kama porojo tu na mtu wa kujitafutia sifa ili aonekane ‘anawajua sana watoto wa wakubwa’.

Lakini wakati akimalizia kuvuka barabara, anageuka nyuma, na hapo mmoja wa abiria akiitikiwa na wenzake, anasikika akisema: “Kweli, ninaona sura kama ya Mwalimu Nyerere.”

Basi, kutoka hapo ikawa gumzo hadi niliposhuka kituo changu cha Kawe Ukwamani. Gumzo lenyewe lilikuwa la kuhoji namna hawa watoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walivyolelewa kiasi kwamba wanapanda daladala kama walivyo Watanzania wengine wengi. Hawana makuu.

Naam! Mtoto huyu wa Mwalimu anayesemwa hapa ni Anna Watiku Nyerere, ambaye ni mtoto wa pili kwa Mwalimu na Mama Maria Nyerere. Kama walivyo ndugu zake wengine, anasifika kwa ucha Mungu na upole. Hamiliki gari. Ndiyo maana haishangazi kuona akitumia usafiri wa umma.

Staha yake imemfanya mwandishi wa makala hii amtafute na kufanikiwa kuzungumza naye. Wanaomjua wanasema si mzungumzaji sana, na pengine ndiyo maana ni nadra mno kumuona kwenye vyombo vya habari au katika majukwaa ya siasa.

Anna anazungumziaje miaka kadhaa tangu kifo cha baba yake, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere?

“Tunamshukuru Mungu, watu wengi wa nje na ndani ya nchi. Nashangaa jinsi ambavyo watu wengi ambao siwafahamu, wakiniona wananifurahia; si kwa sababu yangu mimi, bali kwa sababu ya Mwalimu.

“Watoto ambao ni kizazi cha wajukuu zangu ambao hata hawakumuona Mwalimu, wakiambiwa: “Mnamjua nani huyu? Wanachangamka sana.”

Je, anamkumbukaje Mwalimu kama mzazi na mlezi wa familia?

Anasema: “Wazazi wetu wote ni walimu. Wametufundisha kuongea kwa mpangilio mzuri wa mantiki. Wametufundisha kuwaheshimu watu wote; na kuheshimu na kuthamini hekima ya watu wazima. Wametufundisha kushiriki kazi zote za nyumbani bila kujali jinsia. Wametufundisha kuthamini vipaji vyetu na uwezo wetu bila kushindana na wengine, bali kwa kujiwekea viwango mwenyewe vya kushindana hadi kufikia upeo wako mwenyewe.”

Anasema anawashukuru wazazi wake kwa sababu ya malezi waliyowapa. “Tungelelewa tofauti, tungekuwa tofauti. Hiyo ni sifa ya wazazi wangu – hawakuwa wanafiki wala waongo. Mimi najijua mwenyewe kwamba sina pembe badala ya nywele, wala sina mabawa badala ya mikono. Lakini ningelelewa tofauti ningeweza kuwa na bahati mbaya ya kujidhani niko tofauti,” anasema Anna.

Vipi kuhusu kumuenzi Mwalimu? Anna anajibu swali hilo kwa kusema: “Kila mtu katika hali aliyonayo – awe kijana, mwalimu au mwanafunzi, ana nafasi ya kumuenzi Mwalimu kwa kutimiza wajibu wake kikamilifu popote alipo.”

Kama walivyo Watanzania wengine wengi wenye mapenzi ya dhati kwa Mwalimu, Anna naye anaona kuna mambo kadhaa ambayo hayaendi vizuri kama Mwalimu alivyokusudia.

“Kama Mwalimu angekuwa hai, jambo moja ambalo lingemsikitisha ni kwa kila raia binafsi kutoshiriki kikamilifu kulitumikia taifa hili. Mwalimu alipouchukia ukoloni alijishughulisha kwa kila namna akisaidiana na kila mtu aliyehamasika ili kuleta Uhuru. Na sisi tufanye hivyo. Tutafutane tunaoweza kufanya kazi pamoja, tushirikiane kila tatizo kwa uwezo wote tulio nao,” anasema na uongeza:

“Maskini ni wengi sana kuliko matajiri. Zamani hongo ilikuwa malipo aliyopewa mtawala ili kuwaruhusu wafanyabiashara wapite maeneo yake na kuwapa ulinzi. Maskini wajue kwamba nchi hii ni yao. Wao ndio machifu wenyewe. Viongozi wakitaka kupita kama wafanyabiashara, wawadai ‘hongo’ ya kuridhisha,” anasema Anna.

‘Hongo’ anayozungumzia hapa Anna ni kwamba wananchi wana wajibu wa kuwabana viongozi na kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza ahadi wanazotoa, badala ya kuwapa maneno ya hadaa au vijizawadi visivyokuwa na tija kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

“Hapo kiongozi kama mfanyabiashara, wananchi wampe ulinzi na usalama. Anaporudi kwenye msafara wake wa biashara (kuomba kura) awe tayari amekwishaweka msingi wa chuo kikuu na hospitali safi,” anasema.

Hadi mauti yanamfika, Mwalimu Nyerere hakusita kutamka wazi kwamba vitabu viwili alikuwa haachani navyo. Vitabu hivyo ni Biblia na Azimio la Arusha.

Azimio la Arusha limeshazikwa. Anna anasema: “Mwalimu alisema hajawahi kuona kosa kwenye Azimio la Arusha. Venezuela wamelichukua, wanalifanyia kazi. Sisi bado tumemezwa na wakati.”

Kama walivyo Watanzania wengine, Anna anaiona hatari inayolikabili taifa, inayosababishwa na pengo kati ya maskini na matajiri.

“Hofu ya Mwalimu ilikuwa kwamba wasio nacho siku moja watachoka; halafu hakutakuwa na amani,” anasema.

Kuna mapendekezo kutoka kwa wananchi kadhaa wanaodhani siku sahihi ya kumuenzi Mwalimu iwe ile aliyozaliwa; na siku aliyoaga dunia. Anna kwa mtazamo wake, anasema: “Mimi sina maneno. La muhimu ni kumbukumbu. Lakini ningependa zaidi akumbukwe kwa kutumia mfano wake. Alikuwa mwalimu hodari, mzazi mwelewa, mkulima mwenye bidii, aliyekuwa tayari kujifunza asilolijua, si mchoyo wa elimu, mwandishi stadi. Kila mtu kwa nafasi yake amkumbuke kwa kutimiza wajibu wake.”

Anna si mwanasiasa kama walivyo wadogo zake wengine, akiamini kuwa ingawa si wa kusimama majukwaani, bado na yeye ni mwanasiasa kwa namna yake.

“Siasa ni mpangilio wa kanuni na taratibu za maisha ya raia, kwa hiyo inamhusu kila mtu, hata wewe (mwandishi wa habari) ni mwanasiasa. Lakini naielewa maana yako. Magige (Emil Magige (mdogo wake anayemfuata Anna) alikuwa mwanasiasa, Rosemary (Nyakasero) na Makongoro (Charles) walikuwa wabunge; na Makongoro bado ni Mbunge katika uwanja mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki.

“Lakini baba alikuwa pia mwalimu; Magige, Makongoro, Rosemary na mimi wote tumewahi kuwa walimu katika vipindi fulani vya maisha yetu.

“Baba alikuwa mkulima; Madaraka (Godfrey) mpaka leo analima. Baba alikuwa mwandishi na mfasiri wa mashairi; Andrew (Burito), John (Nyerere), Madaraka na mimi ni waandishi na wafasiri; na mimi ni mshairi pia.

“Baba alikuwa Amiri Jeshi Mkuu; Andrew, John na Makongoro wote walikuwa maaskari. Kwa hiyo kila mmoja alikuwa kwenye mpangilio fulani wa kanuni na taratibu za maisha ya raia katika kurithi fadhila za baba,” anasema Anna.

By Jamhuri