Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waislamu wa Ansar Sunni, Sheikh Salim Abdulrahim Barahiyan, amesema jumuiya hiyo haina uhusiano na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda. “Mimi sijawahi kukaa na Sheikh Ponda katika kikao hata kimoja. Tuna misikiti karibu 20 Tanga, hajawahi kuingia hata msikiti mmoja,” amesema Sheikh Barahiyan.

Akizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, Sheikh Barahiyan amesema taarifa kwamba yeye ana ushirika na taasisi ya al-Qaeda na kuwa anashirikiana na Sheikh Ponda si za kweli, na amekiri kuhojiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani kuhusiana na tuhuma hizi.

 

Alisema Sunni hawana uhusiano wowote na kundi la Uamsho linalohusishwa na kundi la al-Hijra la Kenya, na kuwa makundi haya yanapokea msaada wa moja kwa moja kutoka kundi la al-Qaeda.

 

“Sisi hatuna mawasiliano na watu wote wanaofanya maandamano. Hatuna uhusiano wowote na Uamsho. Hatutaki confrontation (mapambano) sisi. Tanga pamoja na kuwa ni mji wa Waislamu hakuna tawi la Uamsho,” amesema.

 

Kwa upande mwingine, amesema Sunni wanapinga habari ya Sheikh Ponda au viongozi wa kundi la Uamsho kukamatwa na kuwekwa ndani, kwani hilo linaongeza vurugu.

 

Amesema viongozi wa makundi mbalimbali wakikamatwa na kuwekwa ndani, inawafanya wafuasi wao kupandisha jazba na hatimaye kuzaa maandamano yasiyo ya lazima.

 

Kiongozi huyo amesema: “Answar Sunni hatujiingizi kwenye siasa. Sisi tunafuata mafunzo yetu halisi yaliyokuja kwa Mtume Mohammed (SAW) kuwa dini isichanganywe na mambo mengine ya asili.

 

“Hatujiingizi kwenye vurugu za maandamano. Mimi na taasisi yangu ndiyo nayazuia hayo. Njia nzuri za kupingana ni kutoa maoni bila kupigana na vyombo vya dola. Hatuna police case hata moja,” amesema.

 

Kuhusu suala la kufuga ndevu na kuvaa suruali fupi, amesema: “Tukisema Waislamu wanaweka ndevu, hata Wakristo walikuwa wanaweka ndevu. Kwa wanaume wameamuriwa waweke ndevu wawe tofauti na wanawake. Ndiyo uanaume huo. Sisi tuovaa nguo fupi tumefanya lini maandamano? Mara nyingi wapinzani wetu ni Waislamu wenzetu wanaotupinga,” ameongeza.

 

Sheikh Barahiyan ameiambia JAMHURI kwamba pamoja na kutuhumiwa na FBI na akaripoti serikalini mwaka jana, lakini hadi sasa hajapewa hati ya kusafishwa.

 

“FBI walikuja kwa sura ya Kitanzania, kwa maagizo yao wakaniita migration kule, wakaniuliza ya migration, lakini mwisho wakaniuliza masuala ya al-Qaeda. Niliwajibu, ila hadi sasa sijapewa jibu, sikamatwi wala kupewa certificate of clearance (hati ya kusafishwa),” amesema Sheikh Barahiyan.

 

Amebainisha kuwa makao makuu ya Sunni yako Tanga, inamiliki shule 16 za msingi 16, sekondari tano, chuo cha ualimu Tanga mjini, hospitali mbili na jumuiya hiyo imesambaa katika mikoa karibu 15 nchini.

 

“Shughuli zetu ni za kielimu, kidini na kijamii. Tumesajiliwa rasmi mwaka 1995 na hujawahi kusikia mlipuko hata mmoja, al-Qaeda wanabomoa hawajengi. Sisi tunajenga,” amesisitiza.

1878 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!