Serikali imeajiri askari ardhi 15 na kuwapangia kazi katika manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam. Manispaa zinazounda jiji hilo ni Temeke, Kinondoni na Ilala.

 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye, ametoa takwimu hizo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed

 

Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua mipango ya Wizara hiyo kaatika kuajiri askari maalumu ili kupambana na wavamizi wa ardhi.

 

Medeye alisema “Katika wa mwaka 2011/2012 Wizara yangu iliajiri askari ardhi 15 na kuwapangia kazi kwenye Manispaa za Jiji la Dar es Salaam . Lengo lilikuwa ni kupata uzoefu kabla ya kuendelea katika halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya nyingine nchini. Kutokana na kuajiriwa kwa askari ardhi, Serikali imepata mafanikio ambayo ni pamoja na haya yafuatayo:-

 

“Askari ardhi waliopangiwa Manispaa ya Temeke walibaini maeneo manne ya wazi yaliyovamiwa ambayo ni Miburani, Chang’ombe, Temeke na Sudani. Hivyo wavamizi waliondolewa na maeneo hayo yalirudishwa kwenye matumizi ya awali.

 

“Askari ardhi waliopangiwa Manispaa ya Kinondoni walibaini uvamizi katika maeneo ya wazi 10 eneo la Sinza. Hatua za kuyarejesha maeneo hayo zinaendelea. Aidha, Wizara imeanza kusimika mabango kwenye maeneo ya wazi yanayotahadharisha wavamizi waondoke katika maeneo hayo wakati hatua za kisheria zinachukuliwa.

 

“Serikali inatambua umuhimu wa kuwapo kwa ulinzi shirikishi katika kulinda maeneo ya wazi na uhifadhi wa mazingira. Wizara yangu imeanzisha programu ya kutoa elimu kwa umma juu ya sera na sheria zinazosimamia sekta ya ardhi.

 

“Programu hii itatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari. Hata hivyo, ninaendelea kuwahamasisha wananchi kuwa wa kwanza kutambua uvamizi unaofanywa kwenye mitaa yao , hususan maeneo ya wazi na ya huduma.”

 

1150 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!