Na Mwandishi Maalum

 

Wiki iliyopita tuliwaletea makala ya jinsi Bandari ya Tanga ilivyo fursa muhimu kwa uchumi wa Tanzania na kwa nchi za Uganda na Sudani Kusini, pia bandari hiyo inaweza kuhudumia soko la DRC, Burundi na Rwanda kupitia Bandari Kavu ya Isaka na Bandari ya Kigoma kwa kutumia miundombinu ya reli na barabara.

 

Leo tunaendelea kuwahabarisha umuhimu Bandari ya Kigoma katika kukuza maendeleo ya uchumi wa taifa letu ambalo liko katika mapinduzi ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi unaotegemea viwanda. Bandari hii ni muhimu pia kwa nchi jirani zinazotumia Bandari ya Kigoma katika kuleta maendeleo ya nchi zao.

 

Bandari ya Kigoma ambayo ipo katika mwambao wa ziwa Tanganyika upande wa magharibi mwa Tanzania. Ilijengwa kuanzia mwaka 1922 hadi 1927 na Serikali ya Wakoloni wa Ubelgiji waliokuwa wakitawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Rwanda na ikaanza kufanya kazi mwaka 1927 hadi leo hii.

 

Mkuu wa Bandari za Kigoma ndiye mwenye jukumu la kusimamia bandari zote zilizopo mwambao wa Ziwa Tanganyika upande wa Tanzania ikijumuisha bandari ndogo za Kasanga, Kipili, Kibirizi, Kabwe, Kagunga na Sibwesa pamoja na bandari ndogo ndogo zingine (Cluster Ports).

 

Bandari ndogo ndogo zinazosimamiwa na Bandari ya Kigoma ni zile zilizopo katika Mkoa wa Kigoma ambazo ni Ujiji, Mwamgongo, Mtanga, Ilagala, Karago, Tongwe, Sigunga, Kaparamsenga, Herembe, Rukoma, Lagosa na Kalya na zilizopo katika Mkoa wa Katavi ni Ikola na Karema wakati zilizopo katika Mkoa wa Rukwa ni Kasanga, Korongwe, Kirando (Mtakuja), Ninde, Msamba, Wampembe na Kala.

 

Bandari ya Kigoma na bandari zake katika Ziwa Tanganyika kwa pamoja zina uwezo wa kuhudumia shehena tani 680,000 kwa mwaka pamoja na miundombinu mingine. Pia bandari inayo magati ambayo ni miundombinu muhimu katika kuhudumia meli, abiria na mizigo.

 

Katika kipindi cha miaka mitano (2012/2013 hadi 2016/2017) mtiririko wa shehena umekuwa ukipanda kutokana na ufanisi wa huduma inayotolewa na bandari sambamba na ukuaji wa uchumi katika nchi jirani ambazo husafirisha shehena kupitia katika bandari ya Kigoma. Sababu ya nyingine la ongezeko la shehena ni kuimarika kwa Reli ya Kati baada ya kupata injini za treni kwa ajili ya mabehewa ya mizigo hasa katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na 2016/2017.

 

Pia kuanza kazi kwa bandari ya majahazi ya Kibirizi ambapo shehena zilizochangia zaidi ni shehena za vyakula na bidhaa za ujenzi. Sababu nyingine ni ongezeko la soko kwa bidhaa za vyakula na ujenzi hasa saruji inayozalishwa nchini Tanzania kwenda katika nchi za DRC na Burundi.

 

Bandari ya Kigoma ni kiungo muhimu kiuchumi na kijamii kwa kuwa ipo karibu na nchi za ukanda wa Maziwa Makuu za Burundi na DRC. Kuwepo kwa njia ya reli inayounganisha na Bandari ya Dar es Salaam na Kigoma kunaifanya bandari hii ya Kigoma kuwa kiungo muhimu sana cha usafirishaji wa shehena kwenda au kutoka nchi za Burundi na DRC.

 

Aidha kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika nchi za Burundi na DRC kunatoa fursa ya kuongezeka kwa shehena kupitia bandari ya kigoma hivyo kusaidia kukua kwa uchumi wa mkoa wa Kigoma na taifa kwa ujumla. Pia kuanzishwa kwa ukanda maalum wa uwekezaji (EPZ) katika Mkoa wa Kigoma kutaongeza fursa za kibiashara kwa bandari ya Kigoma.

 

Kwa upande wa usalama wa mizigo na abiria, bandari ya Kigoma imeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya bandari, na kutokana na uimara wa ulinzi katika bandari ya Kigoma hakuna tukio lolote lililotokea la kuhatarisha usalama wa meli, abiria na mizigo.

 

Ili kuhakikisha Bandari ya Kigoma inaongeza ufanisi katika kuhudumia meli, mizigo na abiria, TPA imewekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile; ujenzi wa gati katika Bandari ya Kagunga, ujenzi wa gati ya Bandari ya Sibwesa iliyopo katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

 

Mradi mwingine unaotarajiwa ni ujenzi wa gati katika wa ufukwe wa Kibirizi ambao unatumiwa sana na majahazi na boti kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo pamoja na ujenzi wa ofisi ya Utawala. Miradi mingine ni ujenzi wa gati katika bandari ya Ujiji na ujenzi wa gati katika Bandari ya Lagosa.

 

Miradi mingine ambayo TPA imewekeza na ipo katika hatua mbalimbali ni pamoja na uendelezaji wa Bandari ya Kasanga, ujenzi wa barabara katika Bandari ya Kipili na ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho itakayosaidia kupunguza mlundikano wa mizigo bandarini kutokana na mipango iliyopo ya kuimarisha miundombinu ya reli na barabara.

 

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania itaendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa pamoja na kushirikiana na wadau ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa meli, taasisi za umma na binafsi, mawakala wa forodha na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa meli, abiria na mizigo.

 

TPA kwa kumjali mteja ina kituo cha huduma kwa mteja ambacho kina simu ambazo mteja anaweza kupiga au kutuma ujumbe mfupi (SMS) bure kuuliza swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini kwa saa 24. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047. Bandari imejipanga kutoa huduma bora kwa kila mwananchi.

Please follow and like us:
Pin Share