Baraza Maalumu la Siri kwa ajili ya kumchagua kiongozi mpya wa kanisa katoliki duniani, litaanza baadaye leo kwenye Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican.

Makadinali 133 kutoka kila pembe ya dunia watakusanyika kwenye kanisa dogo la Sistine kuanza zoezi la upigaji kura ili kumchagua mrithi wa Papa Francis aliyeaga dunia mnamo Aprili 21.

Watajifungia kwenye kanisa hili kwa muda usiojulikana hadi pale mmoja miongoni mwao atakapofanikiwa kupata theluthi mbili ya kura na kutawazwa rasmi kuwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo lenye waumini wapatao bilioni 1.4.

Waumini na wafuatiliaji wengine kote duniani watasubiri ishara ya kuchaguliwa kwa papa mpya kupitia moshi utakaotoka kwenye chimni iliyofungwa juu ya kanisa la Sistine.

Moshi mweupe utakapofuka itakuwa ni ishara kuwa baraza hilo la makadinali limefanikiwa kumchagua kiongozi mpya wa kanisa.