MADIWANI watano wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mkoa wa Mtwara wamebakia na mshangao baada kukuta barua zenye ujumbe zilizoandikwa kwa maandishi mekundi nyumbani kwao.

Ujumbe hizo zinazosomeka ‘Munatualibia maisha yetu na nyinyi mujiandae kuhalibiwa kwa namna yoyote maisha yenu’ zimeandikwa kwa wino mwekundu huku mwishoni ikiwa na jina la diwani aliyekusudiwa.

Ujumbe huo umebandikwa katika nyumba zao usiku wa kumkia Agosti 2, 2022. Akizungumzia ujumbe huo, Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Shadida Ndile amesema ameshangazwa na ujumbe huo ambao mwishoni umeandikwa jina lake.

Amesema kila mmoja alikuta ujumbe ukiwa kwenye bahasha umewekwa nyumbani kweke huku akisema ujumbe huo hauna lengo zuri kwao kwa kuwa umelenga kuwatisha kwa jambo ambalo hawalijui.

“Sijui wanamaanisha nini ni ujume huo yaani umekuwa wa tishio kwangu sijui walioandika wanamaanisha nini na kwanini walenge madiwani watano nikiwamo na mimi.Nilipoupata nilishtuka sana nilipowasiliana na baadi ya madiwani nao wakawa na ujumbe ule tulifika polisi kutoa taarifa ambapo ni madiwani wa kata za Mtonya, Vigaeni, Chuno, Naliendele na Ufukoni.

“Unajua Mtwara hatujafikia hatua hiyo tuko salama na shughuli za maendeleo zinaendelea, sio utamaduni wetu kutishiana kama kuna watu ambao wamekwazwa na jambo watoe taarifa kwenye mamlaka husika jambo hilo litafutiwe ufumbuzi sio sawa kutishiana na unaemtishia hajui nini kosa lake,”amesema.

Naye Diwani wa Vigaeni, Said Nassoro amesema jambo hilo ni kubwa,“Mimi sielewi kwanini wamefanya hivyo kwa upande wangu sielewi kwanini mtu aseme kuwa tumemuharibia maisha nasisi tujiandae kuharibiwa maisha yetu ni ujumbe mfupi lakini ni ujumbe ambao unazua maswali mengi kwangu.

“Huu ujumbe aliuona mwanangu akanipigia simu kuna ujumbe na akapiga picha akanitumia nikashangaa kwanini barua zinafanana na ndani ya bahasha kulikuwa na barua mbili yangu na ya meya hii ni kutishia maisha ya mtu kama mtu kaweza kuja nyumbani kwako na kuweka ujumbe huo anaweza kuja kufanya lolote,”amesema.

By Jamhuri