Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
 
Kitambo sijaandika makala ya Sitanii kwa mtiririko wake wa kawaida. Nafahamu msomaji umesikia na unalifahamu sakata linaloendelea kati ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ambapo Mpina anasema Bashe amelidanganya Bunge mara 18. Juni 4, 2024 Mpina ndipo alitoa tuhuma hizi na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimpa siku 10 Mpina kuthibitisha madai yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Mpina amekusanya huo ushahidi akauwasilisha kwa Spika, lakini mara tu baada ya kuuwasilisha akaitisha mkutano na waandishi wa habari akasoma kila alichokiwasilisha. Hili peke yake limenipa shaka na nia ya huyu mdogo wangu Mpina. Si nia yangu kumhukumu yeyote awaye, lakini sina uhakika kama Mpina hakuwa akifahamu utaratibu na kanuni za Bunge, linapokuja suala la kuwasilisha ushahidi na kusubiri uamuzi wa Spika.

Sitanii, leo sina mpango wa kurejea vifungu vya Kanuni au Sheria na Katiba, ila nataka kutumia mantiki tu katika makala hii. Kwamba nchi ilikuwa na upungufu wa sukari, upugufu uliozaa kupada kwa bei kutoka Sh 2,400 hadi Sh 10,000 katika baadhi ya maeneo. Sisi Gazeti la JAMHURI tumepata kuliandika hili sakata kwa kina.

Naomba nirejee kidogo mwaka 2000 wakati hayati Idd Simba akiwa Waziri wa Viwanda katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa. Ilikuwa ni sakata sawa na hili la sukari, ambapo Idd Simba alishutumiwa na Mbunge Thomas Nyimbo kwa kutoa vibali vya sukari kinyume cha utaratibu. Naambiwa sakata hili lililoendelea hadi mwaka 2001, liligharibu maisha ya Makamu wa Rais, Dk. Omary Ali Juma, ambaye wandani wanasema alijulishwa kuwa anahusishwa na utoaji wa vibali vya sukari akapata mshituko wa moyo, roho ikaachana na mwili.

Taarifa nilizonazo baada ya sakata hilo la 2001, ulifanyika uamuzi kuwa wenye viwanda vya kuzalisha sukari ndio pekee wapewe vibali vya kuingiza sukari utakapotokea upungufu wa sukari nchini. Kilichofuata baada ya hapo, ni tetesi kuwa wenye viwanda waliona uchochoro kuanzia wakati huo wakaufanya utaratibu huu kuwa kivuno. Yapo maneno kuwa hawa wakubwa walianza kushirikiana kupanga bei, hali iliyopandisha sukari kutoka wastani wa Sh 600 wakati huo hadi Sh 2,400 mapema mwaka jana bila nchi kushituka.

Sitanii, mwaka huu baada ya bei kupanda kuliko kawaida, Waziri Bashe akaamua kueleza nia ya kubadili Kanuni hii na akafanikiwa kuwapa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mamlaka ya kuagiza au kutoa vibali kwa waagizaji wa sukari. Baada ya hilo kufanyika, bei ya sukari iliyokuwa imepanda hadi Sh 10,000 ikaanza kushuka na sasa ipo hadi Sh 2,800 katika baadhi ya maeneo nchini.

Mpina anasema anatetea wanyonge na kwamba Bashe amelidanganya Bunge mara 18 wakati Bashe akieleza utaratibu alioutumia kuingiza sukari nchini, badala ya wenye viwanda wasiozidi saba waliopewa vibali vya kuingiza tani 30,000 na hawakufanya hivyo. Kwa hiyo Mpina anasimama na wenye viwanda 7, ambao hawakuingiza sukari nchini bei ikapanda hadi Sh 10,000 kwa kilo, anaosema wamepokwa haki, naye anatetea haki yao.

Kwa upande wake, Waziri Bashe anatetea Watanzania milioni 61 na zaidi, kuwa hawawezi kuendelea kununua kilo moja ya sukari kwa Sh 5,000 hadi Sh 10,000, hivyo akatoa vibali kwa aliowapa wakaingiza sukari nchini bei ikashuka. Naomba nieleweke. Ndiyo maana nimesema hapa sitataja masuala ya Kanuni, Sheria au Katiba. Mimi ni muumini wa Mwanamageuzi wa China, Deng Xiaoping. Deng alipata kusema: “Haijalishi iwapo paka ni mweusi au mweupe, ilimradi anakamata panya.”

Ni katika msitari huu, nami najiuliza shida ya Watanzania ilikuwa ni nini? Watanzania walitaka kufahamu nani ameingiza sukari au kupata sukari kwa bei isiyowaumiza? Sasa naanza kuziona hoja dhaifu kuwa Bashe amewapa vibali wauza simu, washona viatu na kadhalika. Hapa ndipo namkumbuka Deng Xiaoping. Ukiniuliza mimi rangi ya paka si muhimu, ilimradi anakamata panya.

Nchi yetu imechelewa mno kutokana na siasa uchwara. Wale waliokuwa wanalia kwa kukosa sukari au kuinunua kwa bei juu, leo sukari imekuja wanatafuta sehemu nyingine ya kupumulia. Narudia, binafsi nilimpenda Edward Ngoyai Lowassa (Mungu amlaze mahala pema peponi), si kwa jingine, bali kwa kufanya uamuzi. Lowassa alikuwa akisema bora ufanye uamuzi ukosee kuliko kutoamua.

Sitanii, ukiacha Lowassa nchi hii, alikuwapo Mzee Edward Moringe Sokoine, yupo Eliakim Maswi na Dk. Emmanuel Nchimbi. Hawa wamekuwa wanafunzi wa kweli wa Mwalimu Julius Nyerere. Ni watu ninaowafahamu kuwa misimamo yao inakuwa wazi linapokuja suala la kueleweka wapi umesimama. Narudia, hawa ni wafuasi wa kweli wa Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume. Wanasema ukweli bila kupepesa macho.

Yupo mwingine niliyekubaliana naye katika kufanya uamuzi. Hayati Rais John Pombe Magufuli. Ilihitaji moyo mgumu kuamua kujenga Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.

Ilihitaji moyo mgumu kuamua kuanza ujenzi wa Daraja la Busisi Mwanza. Jambo moja lililonikwaza kwa Dk. Magufuli ni historia yake juu ya haki za binadamu, vinginevyo alikuwa na kila sifa katika kufanya uamuzi.

Sitakuwa nimetenda haki duniani na ahera nisipotambua kwa mifano ujasiri wa kufanya uamuzi aliouonyesha Rais Samia Suluhu Hassan. Amepokea nchi ikiwa inatetemeka. Nchi ilikuwa inavuja damu. Wasiojulikana walikuwa wafalme. Uviko – 19 ilikuwa tunaambiwa haipo wakati watu wanakufa. Wanasiasa walizuiwa kufanya mikutano.

Nani asiyejua kuwa yote hayo Rais Samia ameyapindua na kurejesha hali kuwa ya kawaida? Nani asiyejua kuwa uhuru wa vyombo vya habari tumepanda duniani chini ya Rais Samia kutoka nafasi ya 143 hadi 97 na tukawa wa kwanza Afrika Mashariki?

Sitanii, nimemtaja Rais Samia kuonyesha kuwa zipo nyakati kiongozi anapaswa kusimama na wananchi walio wengi. Ukiniuliza mimi, Bashe amesimama na wananchi kwa kushusha bei ya sukari. Shida ninayoipata, najiuliza, hivi Mpina kwa kutetea kampuni 7 na Bashe kutetea Watanzania milioni 61, ni nani kati ya wawili hawa anatetea wanyonge? Mungu ibariki Tanzania.