Wauzaji wadogo wa mbole Mkoani Rukwa wamesifu juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha wakulima wanapatiwa mbolea kwa wakati na kwa bei elekezi inayoendana na maeneo husika ambayo mbolea hiyo inasambazwa kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata hadi Vitongoji.

“Tunashkuru kwamba zile bei elekezi za mara ya kwanza nina imani hawakujua Jiografia ya Mkoa wetu, lakini kwa sasa hivi hizi bei ambazo wametuelekeza zitawasaidia wananchi na sisi tupo tayari kupelekea sehemu yoyote na faida tutaipata, serikali imetutendea haki,” Damas Kofiambili mmoja wa wafanyabiashara wadogo wa mbolea alisema.

Sifa hizo zimeibuka baada ya Uongozi wa Serikali ya mkoa wa Rukwa kutangaza bei elekezi mpya zilizopitishwa na kamati za pembejeo za wilaya kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba wakati akikagua maghala ya mbolea Jijini Dar es Salaam ambapo alizitaka kamati hizo kufanya marekebisho ya bei hizo ili kuendana na gharama halisi za usafirishaji ili mbolea iweze kumfikia Mkulima hadi ngazi ya Kijiji.

Akisoma bei hizo mpya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya amesema kuwa bei hizo zilizopangwa zimezingatia maoni ya wafanyabiashara na wadau wa kilimo pamoja na kuandaa fomu maalum zitakazotumika katika ngazi ya kata ili kuweza kujua kiasi cha mbolea kilichoingia kila siku katika ngazi ya kata na kumfikia mkulima kwa bei hiyo elekezi.

“Kwa makao makuu ya Wilaya ya Kalambo Bei ya DAP imepanda kutoka 57,165 hadi 58,022 na maeneo ya kata na vijiji ni 62,522 na UREA imepanda kutoka 44,711 hadi 45,443 na maeneo ya vijiji ni 49,943. Kwa makao makuu ya Wilaya ya Nkasi Bei ya DAP imepanda kutoka 56,018 hadi 57,000 na maeneo ya kata na vijiji ni 60,000 na UREA imepanda kutoka 43,565 hadi 44,000 na maeneo ya vijiji ni 47,000. Kwa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Bei ya DAP imebaki vile vile, maeneo ya kata na vijiji ni 62,000 na UREA imepanda kutoka 44,480 hadi 45,000 na maeneo ya vijiji ni 49,500. Kwa makao makuu ya Manispaa ya Sumbawanga  Bei ya DAP imepanda kutoka 55,442 hadi 56,000 na maeneo ya kata na vijiji ni 57,000 na UREA imepanda kutoka 42,989 hadi 45,000 na maeneo ya vijiji ni 46,000,” Alimalizia.

Marekebisho hayo yamefanywa kwa mujibu wa kanuni ya 56 (4) kwa Mamlaka ya Mbolea nchini (TFRA) kupewa jukumu la kupitia na kurekebisha bei za mbolea kulingana na sababu maalum. Hivyo wadau na wafanyabiashara wote wa mbolea Mkoani Rukwa wametakiwa kutumia bei hizi mpya zilizopitishwa na kamati za pembejeo za Wilaya.

Hayo yote yamejiri baada ya Rais John Pombe Magufuli kutoa agizo la kusambaza mbolea kwa mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji nchini baada ya kusikia mikoa hiyo bado inasuasua katika upatikanaji wa mbolea hasa katika msimu huu wa kilimo.  Hivyo hadi sasa Mkoa unahitaji tani 2618 za mbolea ya kupandia (DAP) na tani 6958.6 za mbolea ya kukuzia (UREA).

Please follow and like us:
Pin Share