Bila kupitiwa mikataba …

Pamoja na kumpongeza Rais John Magufuli kwa uthubutu na uzalendo wake kwa Watanzania anaofanya katika maeneo mbalimbali, bila kupitiwa upya kwa mikataba yote bado hatutakuwa na jipya.
Hali ya umaskini wa Watanzania baada ya utawala wa awamu ya kwanza imechangiwa na ubinafsi wa kikundi cha watu wachache waliolenga maslahi yao binafsi, na jamaa zao badala ya umma wa Watanzania.
Kikundi hiki kikajitia upofu na uziwi kwani hakitaki kusikia wala kuona; na waliojitokeza na kukosoa wakaitwa wapinzani na wasioitakia mema nchi yetu.

Mema wanayodaiwa na kikundi hicho ni kuguswa kwa maslahi yao binafsi yanayotokana na shughuli zao za kujigeuza madalali wa kugawana rasilimali za nchi na wageni.
Watanzani tutajisumbua mno kumsaka mchawi wetu anayeturoga hadi tunakuwa mafukara wakati nchi yetu ina utajiri mkubwa wa rasilimali za kila namna.
Haiingii akilini kama wasomi wetu waliobobea, kusaini mikataba mibovu ya namna hii ya kuhujumu mali za Watanzania inayotugharimu sasa.

Nakumbuka ziara ya Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, aliyoifanya hapa nchini mwaka 2008 ambayo iliibua malalamiko mbalimbali kutoka kwa Watanzania kwamba wananyonywa rasilimali zao.
Awali, Harper alikuwa na kikao cha faragha na viongozi wa Kampuni ya Barrick na pia kikao cha siri na Ubalozi wa Canada kwa dakika 45 na wafanyakazi waliokuwa wameathirika na uamuzi wa kampuni hiyo kuwafukuza kazi baadhi ya wafanyakazi wake na hatima yao.
Kitendo cha kuwafukuza kazi wafanyakazi hao kilipingwa na baadhi ya wabunge wa Canada akiwamo Paul Dewar wa  chama cha NDP, kutoka Jimbo la Ottawa ya Kati, kwamba Kampuni hiyo ilishindwa kujali usalama wa wafanyakazi wake katika nchi za Chile na Tanzania.
Tuachilie mbali yaliyotokea wakati huo katika ziara ya Harper hapa nchini; lakini kubwa zaidi ni pale alipojibu hoja ya Watanzania kwamba hatunufaiki na madini yetu kwa sababu ya mikataba yetu.
Tangu aweke wazi hilo, Serikali haikueleza chochote wala kuchukua hatua zozote kuhusu mikataba hiyo na maslahi mapana kwa Taifa. Kipindi hicho chote nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini tumeendelea kuishikilia mikataba hii mibovu ya kinyonyaji wakati kiongozi wa ngazi ya juu wa Canada alieleza kuwa kiini ni mikataba yetu?

Kutokana na uthubutu wa Rais Magufuli kuzuia mchanga wa madini (makinikia) kusafirishwa nje ya nchi, mchawi wa Watanzania ni huyu: mikataba yetu yote ni mibovu siyo kwa gesi, madini au mafuta pekee bali kwa kila kitu na mchawi wa pili ni wasomi uchwara tulionao (elimu).
Kinachowasumbua wasomi wetu ni lugha ya Kiingereza, inayotumika kuandika mikataba hiyo? Kama tutaendelea kutumia lugha ya Kiswahili tu na Kiingereza cha kuchapia, basi tutarajie kuibiwa zaidi na wakoloni hawa walioibuka tena kisayansi kwa kucheza na akili za Waafrika.
Nasema mikataba yote ipitiwe upya na iwekwe wazi kwa Watanzania wote siyo kama mikataba ya mafuta na gesi ambayo imefichwa kama biashara ya haramu ya dawa za kulevya na aliyekuwa anaielewa ni yule aliyesaini na aliyeikaribisha. Hili ni balaa.