Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) mwaka 2027 ilifanya Sensa ya Idadi ya Watu na Mifugo kwa watu wanaoishi katika Tarafa ya Ngorongoro. Sensa hiyo ilikuwa maalumu kufanyika katika Tarafa ya Ngorongoro baada ya taarifa ya tathmini ya mwaka 2013 iliyofanywa na NCAA, iliyoonyesha hatari inayoikabili hifadhi hii. JAMHURI limeonelea lichapishe ripoti ya sensa hiyo ambayo ni taarifa rasmi ya kisayansi.
Utangulizi
Sekta ndogo ya mifugo ni sehemu muhimu kwenye sekta ya kilimo nchini Tanzania. Mifugo ina jukumu muhimu katika kupunguza umaskini, kuimarisha usalama wa chakula, kuzalisha ajira na kuhifadhi mazingira.
Aina kuu za mifugo inayofugwa nchini ni ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe. Katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), Wilaya ya Ngorongoro katika Mkoa wa Arusha, ni eneo la hifadhi kwa ajili ya kuhifadhi wanyamapori na rasilimali nyingine za asili huku likihudumia pia mahitaji ya wafugaji na kukuza utalii.
Mifugo kwa muda mrefu imekuwa nguzo ya uchumi, chakula na njia ya maisha kwa Wamasai na makabila mengine. Wamasai ni wafugaji wa mifugo wanaotegemea ng’ombe, mbuzi, kondoo na mifugo mingine kwa ajili ya maisha yao.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ilifanya kazi ya kutathmini idadi ya watu na mifugo katika Tarafa ya Ngorongoro inayojumuisha kata 11 na vijiji 25.
Wakati wa tathmini, takwimu zilikusanywa kuhusu sifa za kaya, rasilimali, hali ya chakula, lishe, uchumi wa kaya, idadi ya mifugo na huduma za mifugo. Takwimu hizi zitatumika katika mabadiliko ya sera kwa ushahidi, upangaji na uandaaji miradi na katika utoaji wa huduma za mifugo katika tarafa.
Sura hii inachambua matokeo yanayohusiana na idadi ya kaya zinazomiliki mifugo, idadi ya mifugo kwa aina na makundi katika kata tofauti za tarafa na huduma za mifugo. Mifugo iliyohusishwa hapa ni ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Umiliki wa ng’ombe
Matokeo ya sensa yanaonyesha kuwa ng’ombe ni rasilimali maarufu katika kaya za Kimasai: Kati ya kaya 20,866 zilizopo katika Tarafa ya Ngorongoro, kaya 16,302 (asilimia 78.1) zinamiliki ng’ombe ndani ya tarafa, huku kaya 4,564 (asilimia 21.9) zikiwa hazina ng’ombe.
Kwa kaya zinazomiliki ng’ombe ndani ya tarafa; Kata ya Nainokanoka ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya kaya (2,373; asilimia 14.6) zinazomiliki ng’ombe, ikifuatiwa na Naiyobi (2,298; asilimia 14.1), Endulen (2,018; asilimia 12.4), Alailelai (1,733; asilimia 10.6) na Ngorongoro (1,728; asilimia 10.6).
Kata za Eyasi zilikuwa na idadi ndogo zaidi ya kaya zinazomiliki ng’ombe (629; asilimia 3.1), ikifuatiwa na Alaitolei (1,066; asilimia 5.7).
Kata ya Nainokanoka (asilimia 19.9) ina asilimia kubwa zaidi ya kaya zinazomiliki ng’ombe nje ya tarafa. Inafuatiwa na Naiyobi (asilimia 19.3) huku Olbalbal (asilimia 12.4), Alailelai (asilimia 11.6), Ngorongoro (asilimia 11), Endulen (asilimia 9.8) na Ngoile (asilimia 7.3). Kata za Alaitolei, Eyasi, Kakesio na Misigiyo zina asilimia ndogo ya kaya zinazomiliki ng’ombe nje ya tarafa.
Kaya na aina ya ng’ombe wanaofugwa
Matokeo ya Sensa yalionyesha kuwa kaya katika Tarafa ya Ngorongoro zinafuga aina tofauti za ng’ombe. Kati ya kaya 16,302 zinazofuga ng’ombe, kaya 13,588 (asilimia 88.48) zinafuga aina ya zebu ikifuatiwa na kaya 273 (asilimia 1.78) zinazofuga aina ya borana na kaya 238 (asilimia 1.55) zinazofuga aina ya ankole.
Aina nyingine za mifugo inayofugwa ni pamoja na maasai, singida white, mpwapwa, friesian na ayrshire.
Kata yenye idadi kubwa zaidi ya kaya zinazofuga aina ya zebu ni Naiyobi (2,032) ikifuatiwa na Nainokanoka (1,929), Endulen (1,535), Alailelai (1,514), Ngorongoro (1,207) na Kakesio (1,182). Eyasi (489) ina idadi ndogo zaidi ya kaya ikifuatiwa na Alaitolei (706), Misigiyo (983) na Ngoile (985).
Ng’ombe wanaomilikiwa ndani na nje ya Tarafa ya Ngorongoro
Matokeo ya sensa yanaonyesha kuwa Tarafa ya Ngorongoro ina ng’ombe 243,069, ambako ng’ombe 238,826 (asilimia 98.3) wanafugwa ndani ya tarafa na ng’ombe 4,243 (asilimia 1.7) wanafugwa nje ya tarafa.
Jumla ya ng’ombe wote ndani na nje ya kata inatofautiana kutoka ng’ombe 15,111 katika Kata ya Ngoile hadi ng’ombe 32,729 katika Kata ya Endulen. Kata ya Endulen (32,729; asilimia 13.5) ina idadi kubwa zaidi ya ng’ombe ikifuatiwa na Ngorongoro (32,008; asilimia 13.3), Nainokanoka (29,433; asilimia 12.1), Kakesio (27,248; asilimia 11.2), Alailelai (20,988; asilimia 8.6), Naiyobi (19,095; asilimia 7.9) na Alaitolei (18,408; asilimia 7.9).
Wafugaji katika kata za Misigiyo, Eyasi, Ngoile na Olbalbal walikuwa na idadi ndogo ya ng’ombe ndani na nje ya tarafa.
Idadi ya ng’ombe ndani ya Tarafa ya Ngorongoro kwa kata
Tarafa ya Ngorongoro ina ng’ombe 238,826 ndani. Wamegawanywa kati ya kata kutoka ng’ombe 14,790 katika Kata ya Olbalbal hadi ng’ombe 32,273 katika Kata ya Endulen.
Kwa hivyo, Kata ya Endulen (32,273; asilimia 13.5) ina idadi kubwa zaidi ya ng’ombe, ikifuatiwa na Ngorongoro (31,387; asilimia 13.1), Nainokanoka (28,718; asilimia 12), Kakesio (26,998; asilimia 11.3), Alailelai (20,728; asilimia 8.7), Naiyobi (18,672; asilimia 7.8) na Alaitolei (18,275; asilimia 7.7). Kata yenye idadi ndogo ya ng’ombe ni Olbalbal (14,790; asilimia 6.2) ikifuatiwa na Ngoile (14,993; asilimia 6.7), Eyasi (15,145; asilimia 6.3) na Misigiyo (16,847; asilimia 7.6).

Rasilimali za ng’ombe kwenye Vitengo vya Mifugo ya Kitropiki (TLU)
Kipimo cha Mifugo ya Kitropiki (TLU) hutumika kulinganisha idadi na wingi wa mifugo inayochungwa katika eneo husika. Vitengo vya kulinganisha mifugo hutumika kutathmini athari ya jumla kwenye ardhi ya malisho ya aina mbalimbali za wanyama (au mchanganyiko wa wanyama), ikiwa imeonyeshwa kama jumla kwa shamba au shamba lote, au kama vitengo kwa hekta (ha) au ekari.
Katika tathmini hii, mifugo ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ilibadilishwa kuwa TLU. Kwa kuonyesha idadi ya mifugo kwa TLU, matokeo yanaonyesha kulikuwa na uwiano hasi kati ya eneo la ardhi na idadi ya mifugo.
Mwelekeo wa idadi ya ng’ombe katika Tarafa ya Ngorongoro
Kulingana na matokeo ya Sensa ya mwaka 2017, kuna ng’ombe 238,826 katika Tarafa ya Ngorongoro. Idadi hii ni kubwa zaidi kuliko ng’ombe 125,931 waliohesabiwa na NBS katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na ng’ombe 131,509 waliokadiriwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013.
Hili ni ongezeko la ng’ombe asilimia 89.6 kutoka 2012 hadi 2017; na asilimia 81.6 kutoka 2013 hadi 2017. Tofauti inaweza kuwa ilitokana na mbinu na ukubwa wa sampuli katika tafiti mbalimbali. Hata hivyo, matokeo haya yanaonyesha kuwa idadi ya ng’ombe inaongezeka kwa sasa katika Tarafa ya Ngorongoro.
Idadi ya ng’ombe kwa kategoria
Idadi ya ng’ombe wanaofugwa ndani ya Tarafa ya Ngorongoro ni 238,826. Kategoria kubwa zaidi ya ng’ombe hawa ni ng’ombe majike (asilimia 37.5) ikifuatiwa na mitamba (asilimia 17.8), ndama wa kiume (asilimia 12.9) na ndama majike (asilimia 12.6), mafahali waliohasiwa (asilimia 5.6), mafahali wasiohasiwa (asilimia 5.6), na mafahali wa uzazi (asilimia 5.2).
Matokeo ya sensa yanaonyesha kuwa kwa kila kategoria idadi ya ng’ombe inatofautiana kutoka kata moja hadi nyingine. Idadi ya ng’ombe majike inatofautiana kati ya 5,571 katika Kata ya Eyasi hadi 10,690 katika Kata ya Nainokanoka. Aidha, ng’ombe majike ndio kategoria kubwa zaidi katika kata zote ikifuatiwa na mitamba.
Ng’ombe nje ya Tarafa ya Ngorongoro
Idadi ya ng’ombe wanaomilikiwa na wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro, lakini wanahifadhiwa nje ni 4,243. Idadi hiyo ni pamoja na mafahali wa uzazi 325, mafahali wasiohasiwa 427, majike 1,291, mafahali waliohasiwa 392, mitamba 619, ndama dume 683, na ndama majike 506.
Matokeo ya sensa yanaonyesha kuwa ng’ombe majike ndio kategoria kubwa zaidi ya ng’ombe wanaomilikiwa nje ya Tarafa ya Ngorongoro. Inachangia asilimia 30.4 ya ng’ombe wote, ikifuatiwa na ndama madume (asilimia 16.1), mitamba (asilimia 14.6) na ndama majike (asilimia 11.9). Mafahali wa mbegu wana idadi ndogo zaidi ya asilimia 7.7. Inafuatiwa na mafahali waliohasiwa (asilimia 9.2) na mafahali wasiohasiwa (asilimia 10.1).
Idadi ya mbuzi inayomilikiwa ndani na nje ya Tarafa ya Ngorongoro
Asilimia ya idadi ya mbuzi inayomilikiwa ndani na nje ya Tarafa ya Ngorongoro inaonyeshwa kwa kata katika Kielelezo 7.15.
Matokeo yanaonyesha kuwa Tarafa ya Ngorongoro ina jumla ya mbuzi 226,260 wanaomilikiwa. Wengi wa mbuzi (asilimia 98.3) wanafugwa ndani ya tarafa na wachache (asilimia 1.7) nje ya tarafa. Asilimia ya mbuzi wanaomilikiwa nje ya tarafa ni ndogo katika kata. Hata hivyo, Kata ya Ngorongoro (asilimia 5.6) ilikuwa na asilimia kubwa ya mbuzi wanaomilikiwa nje ya tarafa. Katika kila kata, asilimia ya mbuzi ndani ya tarafa ni kubwa zaidi kuliko asilimia ya mbuzi nje ya tarafa. Asilimia ya mbuzi ndani ya tarafa inatofautiana kutoka asilimia 94.4 katika Kata ya Ngorongoro hadi asilimia 99.2 katika kata za Ngoile, Kakesio na Alailelai.
Idadi ya kondoo Tarafa ya Ngorongoro
Matokeo ya sensa kuhusu ufugaji wa kondoo inaonyesha asilimia ya kaya zinazojihusisha na ufugaji wa kondoo na idadi ya kondoo wanaofugwa kwa kata na kategoria ndani na nje ya Tarafa ya Ngorongoro, ni kubwa.
Katika kata zote, asilimia kubwa ya kaya zinamiliki kondoo. Kata ya Ngoile (asilimia 89.9) ina asilimia kubwa zaidi ya kaya zinazomiliki kondoo. Inafuatiwa na kata za Olbalbal (asilimia 89.7), na Misigiyo (asilimia 81.5). Kata yenye asilimia ndogo zaidi ya kaya zenye kondoo ni Ngorongoro (asilimia 55.7) ikifuatiwa na Eyasi (asilimia 55.8), na Endulen (asilimia 55.9).
Tarafa ya Ngorongoro ina kondoo 344,373. Hata hivyo, idadi ya kondoo inatofautiana sana kati ya kata. Kata ya Olbalbal (72,560) ina idadi kubwa zaidi ya kondoo ikifuatiwa na Kata ya Ngoile (63,592) na Alailelai (38,302). Kata yenye idadi ndogo zaidi ya kondoo ni Eyasi (3,709) ikifuatiwa na Alaitolei (15,031).

Idadi ya punda
Punda hutumika zaidi kama wanyama wa kubebea mizigo na kwa hivyo ni muhimu zaidi kuliko mifugo mingine kama nguruwe, mbwa na paka. Kati ya kaya 20,866 katika Tarafa ya Ngorongoro, kaya 9,636 (asilimia 46.2) zinamiliki punda. Kata ya Naiyobi (asilimia 64.5) ina asilimia kubwa zaidi ya kaya zinazomiliki punda, ikifuatiwa na kata za Alailelai (asilimia 60.7) na Olbalbal (asilimia 52.4). Kwa upande mwingine, Kata ya Endulen (asilimia 23.7) ina asilimia ndogo zaidi ya kaya zinazomiliki punda.
Huduma za mifugo
Katika ngazi ya tarafa, matokeo ya Sensa yanaonyesha kuwa asilimia kubwa ya kaya katika Tarafa ya Ngorongoro zinaona ubora wa huduma za mifugo kuwa katika hali duni huku asilimia ndogo ya kaya zikiridhika na ubora wa huduma hizo (asilimia 13.5).
Zaidi ya hayo, ubora wa huduma za mifugo ulionekana kuwa mbaya zaidi kwa asilimia kubwa ya kaya katika kata zote za tarafa isipokuwa Kata ya Olbalbal ambako kaya nyingi ziliona ubora wa huduma kuwa wa wastani.
Hata hivyo, Kata ya Eyasi (asilimia 89.8) ina asilimia kubwa zaidi ya kaya zinazosema kuwa huduma za mifugo ni mbaya, na Olbalbal (asilimia 28.8) ina asilimia ndogo zaidi ya kaya za aina hiyo.


