Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) haina meno mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hiyo, Madeni Kipande, baada ya kubainika kuwa maelekezo mengi anayopewa na Bodi anayapuuza.

Baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuunda Kamati ya Mbakileki kuchunguza kinachoendelea bandarini wakati wa uongozi wa Ephraem Mgawe, Kamati ilitoa mapendekezo ambayo bodi ilimwagiza Kipande kuyatekeleza, lakini zaidi ya asilimia 90 ya mapendekezo hayo ameyapuuza.

Kati ya mapendekezo hayo ni pamoja na mafuta kuingizwa bandarini bila kupitia kwenye mita maalum za kupima idadi ya lita zilizoingizwa nchini. Hadi Aprili hii, bado Bandari wanaendelea kuingiza mafuta nchini bila kutumia mita.

Phares Magesa, Mkurugenzi wa ICT, ameithibitishia JAMHURI kuwa  mita hizo hazitumiki kwa maelezo kuwa walielekezwa hivyo na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).

Kamera za Usalama pia hazifanyi kazi hadi sasa, na hili limethibitishwa na Magesa katika mahojiano na JAMHURI, hali inayotia wasiwasi juu ya usalama wa mizigo ya wateja. Haya na mengine mengi, yanathibitisha ubabe, kutojali na ukosefu wa weledi katika tasnia ya uongozi. Ifuatayo ni sehemu ya taarifa iliyowasilishwa na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, John Ulanga.

Baada ya Ulanga kuwasilisha taarifa hii, Kipande alitamka wazi kuwa atahakikisha anaondolewa kwenye ukurugenzi na kweli akamshinikiza Dk. Mwakyembe akavunja bodi na kumwondoa Ulanga kwa kusema ukweli huu, akamwingiza mfanyakazi wa ngazi ya chini kabisa bandarini kwenye Bodi ya Wakurugenzi, ambaye ana uhakika kuwa hawezi kuhoji lolote. Ifuatayo ni sehemu ya kiambatanisho cha taarifa ya Kamati ya Mbakileki kama ilivyowasilishwa na Ulanga, ikasababisha aondolewe kwenye bodi kwa kusema ukweli huu. Endelea…

1.0   Kuchunguza mfumo wa upokeaji na usambazaji wa mafuta bandarini:- Kuangalia mfumo wa upimaji mafuta (flow meters)

Maoni ya Kamati

Mfumo wa upimaji wa mafuta, “metering system” (ambao unajumuisha Flow meters), una kasoro za kiufundi zinazosababisha usiweze kutumika kama ulivyokusudiwa na Serikali ilipoamua kuujenga ili kudhibiti mapato yatokanayo na mafuta yanayoingizwa na kupitishwa (transit) nchini.

Matatizo au kasoro zilizopo zilitokana na Menejimenti ya TPA kutozingatia taratibu za manunuzi ipasavyo na kushindwa kufanya Upembuzi Yakinifu (Feasibility Study) na kuandaa “technical specifications” ili kufahamu mahitaji halisi ya mfumo uliokuwa unahitajika (metering system).

Kutoandaa technical specifications zinazotakiwa kunatokana na Menejimenti kutowashirikisha wataalamu waliopo ndani ya Mamlaka tangu hatua za awali za utekelezaji wa mradi. Hali hii imesababisha manunuzi ya vifaa vya uboreshaji (upgrading facilities) na vipuri mara kwa mara yasiyo na mpangilio kwa gharama kubwa bila kuondoa matatizo ya msingi ya kiufundi. Kamati ya Uchunguzi inashangazwa na usiri mkubwa, udanganyifu na ukaidi uliojitokeza katika jambo hili.

Mchakato wa manunuzi ya Mfumo wa Upimaji Mafuta (metering system) ambao unajumuisha “flow meters” haukuihusisha Wakala wa Vipimo kinyume cha Sheria ya Vipimo – Weights and Measures Act [Cap. 340 R.E. 2002].

Mapendekezo ya Kamati

Maamuzi ya awali ya Serikali yaliyoona umuhimu wa kununua mfumo wa upimaji wa mafuta (metering system) yaendelee kuzingatiwa kwa kuhakikisha kwamba mfumo unaokidhi mahitaji unakuwepo na kutumika kama ilivyokusudiwa.

Serikali ione umuhimu wa kuunda Kikosi Kazi (Technical Task Force) cha kushughulikia mchakato wa kukagua mfumo uliopo kwa madhumuni ya kubaini dosari zilizopo, ili kuziondoa na kuufanya mfumo ufanye kazi ipasavyo haraka iwezekanavyo.

Katika kufanya hivyo, Serikali ishirikishe wadau wote, izingatie sheria, kanuni na taratibu zote husika na kuondokana na usiri uliokithiri wakati wa ununuzi na matumizi ya mfumo uliopo. Iwapo mfumo uliopo utagundulika kuwa na kasoro ambazo hazirekebishiki ama zinarekebishika kwa gharama kubwa, Kamati inapendekeza kuwa Serikali ianzishe mchakato rasmi wa kununua mfumo mpya.

Ununuzi wa mfumo mpya, kama ilivyokuwa wakati wa kukagua mfumo uliopo, pia ushirikishe wadau wote, uzingatie sheria, kanuni na taratibu zote husika na kuondokana na usiri.

Wote waliohusika na manunuzi ya mfumo uliosababisha hasara kubwa kwa Serikali wachukuliwe hatua stahiki.

Maoni ya Bodi

Bodi ya Wakurugenzi itaiagiza Menejimenti ya TPA kuwasiliana na WMA ili wafanye uchunguzi wa kina na wa haraka juu ya flow metering system na watoe mapendekezo yao kabla ya Desemba 31, 2012. Baada ya mapendekezo hayo, Menejimenti ya TPA ilete kwa Bodi maoni na mpango wa kutekeleza mapendekezo hayo.

Ikiwa itapendekezwa kununua mfumo tofauti na wa sasa, basi Bodi ya Wakurugenzi itaagiza Menejimenti ya TPA ishirikishe wadau wote muhimu na kufanya upembuzi wa kina kabla ya ununuzi wa mfumo mpya.

Bodi ya Wakurugenzi itachukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria dhidi ya wote waliohusika katika kuisababishia Serikali hasara kutokana na kasoro za mfumo huu.

Utekelezaji

Menejimenti ya Bandari haijatekeleza lolote

Bodi imechukua hatua ilizopaswa kuchukua

8.0 Mfumo wa Ulinzi na Usalama Bandarini.

(a) Utendaji wa vyombo vinavyosimamia Ulinzi na Usalama TPA.

(b) Namna bora zaidi ya ushughulikiaji makosa makubwa yanayotendeka bandarini.

Maoni ya Kamati

Kamati imeona kwamba uongozi wa TPA umeshindwa kutoa kipaumbele cha kuweka na kusimamia ulinzi na usalama bandarini. Wameshindwa pia kuweka mfumo unaokidhi matarajio, haki na wajibu kati ya mwenye Bandari na wateja kwa upande mmoja na maslahi ya Taifa kiulinzi na kiusalama kwa upande mwingine.

Ni maoni ya Kamati kwamba TPA haijaweka mfumo mzuri wa Ulinzi na Usalama pamoja na kuwa na mamlaka kwa mujibu wa kifungu Na. 45 cha Sheria ya TPA.

Kamati ya Uchunguzi, kutokana na mahojiano na wahojiwa na takwimu zilizowasilishwa, imebaini kwamba kiwango halisi cha wizi unaofanyika bandarini, hasa Bandari ya Dar es Salaam, hakijulikani kwani kuna taarifa ambazo hazitolewi kwa sababu mfumo mzima wa ulinzi na usalama bandarini unategemea taratibu msonge (reactive, bureaucratic and hierarchical procedures).

Hata hivyo, katika matukio machache yanayotolewa taarifa katika vyombo vya usalama na ulinzi, Kamati ya Uchunguzi ilipokea maoni kwa maandishi na kwa njia ya majadiliano, kwamba yapo matukio ambayo hayafanyiwi kazi ingawa yanatolewa taarifa na ushahidi wa kutosha.

Mfano wa tukio kama hili ni wizi wa tani 26 za “MCK copper blister” zilizoibwa katika Bandari ya Dar es Salaam na zikatolewa taarifa. Kutokana na wizi wa makontena manne mnamo tarehe 19-20 May, 2011 Kampuni ya Wakala (Freight Meridien Co. Ltd) kwa barua yao ya tarehe 14 Juni, 2011 waliyomwandikia Mkuu wa Ulinzi wa TPA na kuinakili kwa Mkurugenzi Mkuu, walimshutumu Mkuu wa Ulinzi kwa ulegevu katika kushughulikia suala hili na kutolitolea taarifa. (Kiambatisho Na. 22)

Kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya kisasa vya Ulinzi na Usalama ikiwamo matumizi ya TEHAMA na CCTV, ulinzi bandarini umekuwa ukitegemea utashi wa maofisa na walinzi wanaowasimamia. Hali hii inasababisha mfumo mzima wa ulinzi na usalama kuwa usioaminika (non-reliable).

Ni maoni pia ya Kamati kwamba uwepo wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama pasipo kufafanuliwa uwajibikaji na mipaka ya kazi miongoni mwao, unasababisha kuwapo kwa mazingira ya kutegeana na hata kuhujumiana katika ngazi ya juu ya usimamizi.

Ni maoni ya Kamati ya Uchunguzi kwamba makosa makubwa ya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma yanayotendeka TPA, yanahatarisha uchumi wa Taifa. Makosa haya hayana tofauti na ya uhujumu wa uchumi. Kamati ya Uchunguzi imebaini pia kwamba mashauri ya jinai kuhusu wizi wa mali za wateja, yaliyo katika hatua mbalimbali yanachelewa kushughulikiwa.

Mapendekezo ya Kamati

(i) Kamati ya Uchunguzi inapendekeza kuboreshwa kwa Kitengo cha Ulinzi cha TPA kwa kufanya yafuatayo:

*Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi awe ni mwajiriwa wa TPA na apatikane kwa njia ya ushindani na kwa sifa zitakazoainishwa;

*Kitengo kipatiwe wafanyakazi wa kutosha kwa sifa na idadi;

*Kitengo kipatiwe mifumo na vitendea kazi vya kisasa ikiwa ni pamoja na TEHAMA;

*Wafanyakazi wote wa kitengo cha ulinzi na usalama utendaji wao upimwe kila mwaka kwa kutia saini mkataba wa utendaji (performance contracts), kanuni za kipolisi (Police General Order), atapaswa pia kuzingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma (code of conduct).

Kutokana na mahojiano yaliyofanyika na matukio mbalimbali ya wizi katika Bandari ya Dar es Salaam na Kitengo cha Kontena cha TICTS, Kamati ya Uchunguzi imebaini uzembe wa hali ya juu, kutowajibika na ushiriki wa wafanyakazi wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama kwenye vitendo vya uvunjifu wa maadili. Kutokana na matokeo ya uchunguzi, kamati inapendekeza wafuatao wachukuliwe hatua kulingana na uzito wa makosa yao:

Kulingana na kiwango cha uwajibikaji, Ephraem Mgawe ndiye aliyepaswa kusimamia utendaji wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama na hivyo kwa kutofanya hivyo, Serikali imwajibishe kama itakavyoonekana inafaa.

Wafanyakazi wa kitengo cha ulinzi wawajibishwe kama ifuatavyo:

– David S.Mranda, Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa TPA

– A.P. 43 PC Fortunatus Sandaria, Kiongozi wa Askari

KOJ

– A.P. Limbunga…….Mlinzi geti la KOJ

– A.P. Kilimba ……….Mlinzi geti la KOJ

– Walinzi wa zamu tarehe 19 na 20 Juni, 2011 geti na. 3- tukio la wizi wa makontena manne ya shaba.

(iii) Hali ya ulinzi ilivyo sasa imekuwa ikiachwa bila kuchukuliwa hatua stahiki kwa namna inayofaa licha ya matukio ya wizi kutolewa taarifa na walioathirika/ kushuhudia na hakuna hatua zilizochukuliwa.

Kuhusu namna bora zaidi ya kushughulikia makosa makubwa yanayotokea bandarini, Kamati ya Uchunguzi ina maoni kwamba:

Serikali ifikirie kurekebisha sheria ili baadhi ya makosa yenye uzito toshelezi yashughulikiwe na kuamuliwa kama makosa ya uhujumu uchumi.

Serikali ifikirie kuanzisha mfumo wa mahakama maalum (the admiralty court) kwa ajili ya kushughulikia makosa yanayofanyika bandarini, melini na kwenye bahari.

Maoni ya Bodi

Bodi ya Wakurugenzi itakisuka upya kitengo cha ulinzi ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi kwa ushindani na kuweka mkataba wa utendaji kwa kitengo hicho na kwa menejimenti nzima.

Bodi ya Wakurugenzi itachukua hatua stahiki za kinidhamu na za kisheria dhidi ya wote waliohusika katika kushindwa kusimamia ulinzi na usalama na hivyo kuisababishia TPA na Serikali hasara.

Utekelezaji

Menejimenti ya Bandari haijafanya lolote

9.1 Matumizi ya TEHAMA (ICT)

4.1.9.1 TPA inaendesha shughuli zake kizamani, bila kuzingatia matumizi ya sayansi na teknologia hususan katika nyanja za TEHAMA, CCTV na mengine mengi. TPA isipochukua hatua sahihi kwa haraka, itaendelea kubaki nyuma, itakosa biashara na kukimbiwa na wateja.

4.1.9.2 Kamati imeshuhudia uwepo wa miradi kadhaa na ya madhumuni mbalimbali katika TPA, ambayo ingekamilika ingeweza kusaidia kuyapatia ufumbuzi matatizo mengi kama siyo yote yanayohusishwa na uduni katika matumizi ya TEHAMA katika TPA.

Miradi hiyo inahitaji kuokolewa kwa kurekebisha upungufu uliotokea ili kujipanga vema zaidi katika kuikamilisha miradi hiyo.

4.1.9.3 Kamati imeshangazwa na tabia ya TPA kuibeba Kampuni ya M/s SofTech Consultancy katika mazingira ambayo anashindwa katika michakato ya zabuni lakini anapewa kazi hizo kiujanjaujanja kinyume na masharti na taratibu za zabuni husika.

Miradi ya TEHEMA inahitajika kwa haraka ili kuifanya Bandari kutekeleza majukumu yake kisasa zaidi. Hivyo inatakiwa iweke ratiba ya utekelezaji na itenge fedha za kutosha kwa ajili ya manunuzi na mafunzo ya watumishi. Miradi hiyo ni pamoja na:

Port Community System, Integration ya billing payment system na receipts, CCTV cameras, Wide area network (WAN) na Local Area Network (LAN) na Radio data on call nk.

Maoni ya Bodi

Bodi itaunda kamati ndogo itakayosimamia masuala ya TEHEMA na Usalama wa Bandari. Bodi kupitia kamati ndogo itakayoundwa itaiagiza menejimenti kufanya tathmini mifumo, matumizi, na ujuzi wa TEHAMA ndani ya Mamlaka ya Bandari; Kutengeneza mpango mkakati wa TEHEMA unaoshabihiana na Mpango mkakati wa Mamlaka ya Bandari (Provide strategy direction and the alignment of IT and the business).

Utekelezaji

Bodi imeunda Kamati Ndogo

Menejimenti ya Bandari haijatekeleza lolote zaidi ya kumkejeli Dk. Jabir Bakari na kuishia kumuondoa kwenye Bodi ya Wakurugenzi. Hadi sasa hakuna cha CCTV, wala mifumo ya fedha kuzungumza. Usikose mwendelezo wa habari hii wiki ijayo.

1526 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!