Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kijana Edger Edson Mwakabela (27), maarufu kwa jina la Sativa, mkazi wa Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam amepatikana katika Hifaadhi ya Katavi akiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali ya mwili wake.

Sativa ambaye alitoweka tangu Jumapili Juni 23, 2024 akiwa maeneo ya Ubungo.

Taarifa za kupotea kwa kijana huyo zilitolewa na familia baada ya kijana huyo kutorudi nyumbani kutoka katika fukwe za Coco beach alikokwenda na kaka yake.

Familia ilifanya jitihada mbalimbali za kumtafuta bila mafanikio na kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Kimara na kupewa RB namba 3249/ 2024.

Akizungumza na Jamhuri Digital, rafiki yake wa karibu James Nelson, amesema kuwa baada ya kusambaa kwa taarifa hizo, leo Juni 27, walipokea simu kutoka kwa wasamaria wema kuonekana kwa kijana huyo mkoani Katavi eneo Hifadhi ya Katavi akiwa amejeruhiwa nama kutelekezwa.

” Tulipata taarifa ya kuonekana kwa Sativa mkoani Katavi lakini akiwa hoi baada ya kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana huku miguu yake yote miwili ikiwa imevimba baada ya kupigwa” amesema.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo, wasamaria wema wamempeleka katika kituo cha afya cha Kibaoni kilichopo njia ya kwenda Majimoto kwa ajili ya huduma ya kwanza ya kitabibu.

“Tunawashukuru sana wasamaria wema hao na tumewaomba ndugu yetu aendelee kupata huduma zaidi wakati taratibu zingine zaidi zikiedelea.

“Hata hivyo tayari wadau mbalimbali wameanza utaratibu wa kuhakikisha Sativa anasafirishwa kwa ndege kutoka Mpanda hadi Dar es Salaam ili kupata matibabu ambapo tayari kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amechangia tiketi ya ndege.