Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo ya usajili na rasimishaji wa biashara kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Jamhuri Media.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Joyce Mgaya, Ofisa Habari Mkuu wa BRELA, amesema kuwa wameamua kuwatumia waandishi wa habari na wahariri kwa kutoa elimu hiyo ili ifikishwe ngazi ya jamii.

Joyce alisema kuwa lengo kuu ni kutumia waandishi wa habari kama njia ili jamii iweze kuelewa shughuli wanazozifanya kupitia kalamu zao.

Aidha, alitaja umuhimu wa kutambua mchango mkubwa wa waandishi katika jamii, kwa kuhakikisha umma unapata uelewa mzuri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na BRELA. Amesema kwa sasa, moja ya mikakati yao ni kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari.

“Kwa kushirikiana na waandishi na wahariri, tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu katika kutoa elimu katika maeneo mbalimbali kama vile semina, warsha, vyuoni, mashuleni, na makongamano.

Tumejikita katika kutoa elimu kuhusu masuala ya usajili na ulasimishaji wa biashara.

“Ni wazi kwamba vijana wengi sasa wamejikita katika biashara na ubunifu, hivyo tunawatia moyo watu kutafuta fursa za biashara.

“Tunatoa elimu katika maeneo mengi kwa vijana na wanawake, lakini pia tunakaribisha mtu yeyote mwenye kikundi chake ambaye anahitaji msaada kuhusu ulasimishaji wa biashara au kutatua migogoro inayohusiana na biashara.

Utoaji wa elimu ni mchakato endelevu kwa jamii.kuhusu changamoto zinazojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu, amesema hizo ni fursa kwao kwani wanapo mwelekeza mtu kutatua tatizo , wanakuwa wapo katika
kutekeleza majukumu yao kwasababu asilimia kubwa ya kazi yao ni utoaji
wa elimu.

Huduma za miliki bunifu, faida zake, na masuala mengineyo yanapojitokeza, ni muhimu kutoa elimu ili jamii iweze kuelewa na kutumia huduma tunazotoa, hivyo ni lazima tutumie vyombo vya habari” amesema.

Joyce amesema mikakati yao kwa sasa ni kuimarisha utoaji wa elimu zaidi kupitia vyombo vya habari na mitandao yao ya kijamii kwa kuandaa vipindi mbalimbali vya mafunzo.

Ofisa sheria kutoka BRELA, Neema Nyansi amesema kuwa jukumu kuu la BRELA ni kuelimisha jamii kuhusu usajili wa makampuni na majina ya biashara kwa njia ya kidijiti.

Amesema kuna umuhimu wa kufuata taratibu zinazohitajika ili kusajili kampuni, kwani usajili pekee haukidhi mahitaji. Kuna matakwa ya kisheria ambayo yanapaswa kutimizwa baada ya kumalizika kwa usajili.

Aliongeza kuwa miongoni mwa taratibu hizo ni pamoja na taarifa za mwaka, ambazo ni muhimu kwa wamiliki, na pia alikumbusha kuhusu notisi za uwasilishaji wa taarifa za makampuni ambazo zilisajiliwa kabla ya
kuanzishwa kwa mfumo wa usajili wa mtandao.

Amesema kwa sasa nchi inahamia kwenye biashara kwa njia ya kizamani na kuhamia kwenye kidigitali katika usajili,kwa hiyo tunahamasisha Umma kuelewa zaidi taratibu za usajili kwa njia mtandao ili kupata huduma
mbalimbali

“Usajili kwa njia ya mtandao umeanza kutumika mwaka 2018, kwa hiyo kuna kampuni zilizosajilia kuanzia muda huo taarifa zake zipo kwenye mfumo wa kidijiti.

Kwa sasa ombi lolote lina anzishwa kwa njia ya mtandao, linachakatwa kwa njia ya mtandao cheti kinatoka kwa njia ya mtandao na kila namna ya uwasilishaji wa tarifa yeyote zinazohusisha kampuni kwa
hiyo”amesema.

Amesema kabla ya mwaka 2018 walikuwa wanatumia karatasi ,taarifa zilikuwa zinajazwa kwenye fomu na mwisho cheti kinatoka anapewa mteja na ingine inabaki kwenye faili.

“Tunatoa wito kwa kampuni ambazo zipo kwenye mfumo wa mafaili,kuingia kwenye mfumo wa kidijiti kujisajili kwa njia ya mtandao kabla muda kwisha.

Kama kuna makampuni yanadaiwa hasa zile ada za uwasilishaji za kila mwaka wasiogope kuja kujisajili kwasababu mwaka jana aziri ametoa msamaha kwa yale makampuni yasiolipa ada nje ya muda wamepewa msamaha wa asilimia 50’’ amesema.