Glorious Luoga (kushoto) na Peter Zakaria
Glorious Luoga (kushoto) na Peter Zakaria

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, imesadifu kile kilichoandikwa na Gazeti la JAMHURI katika toleo namba 385 kuhusu ubadhirifu wa fedha za maendeleo katika Wilaya ya Tarime.

JAMHURI katika toleo hilo liliandika kuhusu mgogoro wa kiuongozi na tuhuma za upotevu wa fedha za maendeleo zikimhusu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Glorious Luoga.

Luoga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais John Magufuli Januari 27, mwaka huu, alikuwa akilalamikiwa na wananchi wa wilaya hiyo kwa upotevu wa fedha za ujenzi wa Kiwanda cha Sukari (Tarime Sugar).

Tuhuma nyingine zilihusu matumizi ya ukarabati wa Hospitali ya Tarime, kiasi cha Sh milioni 87 zilizotolewa na wadau wa maendeleo ili kuboresha hospitali ya wilaya hiyo.

Katika ripoti ya ukaguzi wa CAG, amebaini miamala yenye utata katika Sekretarieti ya Wilaya ya Tarime ya jumla ya Sh milioni 514.

Kiwango hicho cha fedha kilipokelewa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hospitali ya wilaya na kupima eneo lililopendekezwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na kujenga kiwanda cha sukari.

Katika ukaguzi huo alibaini ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime kuhusika na ufunguzi wa akaunti ya Benki ya NMB bila kibali cha mamlaka husika wala kufuata sheria ya fedha za umma ya mwaka 2001 na kuboreshwa mwaka 2004.

Akaunti hiyo ni Na. 30410011011 ambavyo ilifunguliwa bila kuwa na mamlaka ya maandishi kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa kanuni ya fedha za umma ya mwaka 2001.

“Kanuni hiyo inataka ofisa wa umma kutokufungua akaunti ya benki ya amana, kuihifadhi au kutoa fedha za umma au fedha nyingine ambazo ofisa husika anawajibika nazo kulingana na majukumu ya ofisi au kwa ajili ya kufanya miamala ya kibenki bila kibali kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa Serikali,” anaeleza CAG.

Katika ukaguzi huo, CAG anaeleza Agosti 14, mwaka juzi  Ofisi ya DAS Tarime alihawilisha Sh milioni 300 kutoka Akaunti ya DAS NMB Na. 30410008369 kwenda kwenye akaunti ya biashara Na. 30410011011 iliyofunguliwa kwa jina la Akaunti ya Mageuzi ya Hospitali ya Tarime.

 Lakini tarehe hiyo hiyo (14 Agosti) Sh milioni 300 zilihawilishwa tena kutoka akaunti Na. 30410011011 kwenda kwenye akaunti ya Zacharia Wambura.

“Nina shaka juu ya mzunguko wa hizi fedha kupitia kwenye akaunti iliyotajwa ambayo inamhusisha Zacharia Wambura anayehusika na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime bila kuwa na ushahidi wa nyaraka,” anasema CAG.

Kukosekana kwa nyaraka katika kuhamisha kiasi hicho cha fedha, anasema kunaacha kiasi kilicholipwa kuendelea kuwa chini ya muamala wenye utata.

CAG pia katika ukaguzi huo anabainisha kushindwa kuhakiki matumizi ya fedha zilizochangwa na Kampuni ya Biashara ya North Mara Comm Sh milioni 214.

Anasema hakuhakiki maelezo ya matumizi ya fedha hizo kwa sababu hati za malipo na viambatisho vyake yaliyofanywa na DAS kutoka akaunti Na. 30410008369 zilichukuliwa na ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Katika ukaguzi huo CAG alibaini Ofisi ya DAS Tarime kukosa Kitengo cha Manunuzi ambacho kingezingatia mchakato wa manunuzi kwa mujibu wa Kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.

Hivyo, kushindwa kupata uhakika kama manunuzi ya vifaa vya hospitali yamezingatia matakwa ya Kifungu cha 64(1) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na kanuni zake za mwaka 2013.

JAMHURI lilivyoandika habari hiyo

Siku kadhaa zilizopita mfanyabiashara maarufu, Peter Zakaria, ambaye yuko mahabusu aliibua mambo mapya yanayomhusu Luoga.

Zakaria ambaye amezungumza na Gazeti la JAMHURI kupitia kwa msemaji wa familia hiyo, Samuel Chomete, amesema amefurahishwa na uamuzi wa Rais Magufuli wa kumfuta kazi Luoga.

Januari 27, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Luoga, kisha kumteua Charles Kabeho, kuongoza Wilaya ya Tarime. Kabla ya uteuzi huo Kabeho alikuwa kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka jana.

“Nimeonana na kuzungumza na Peter Zakaria aliyepo mahabusu. Ameniambia amefurahishwa sana na uamuzi wa Rais Magufuli kumfukuza kazi DC Luoga…ameniambia Luoga ndiye chanzo kikuu cha migogoro ya familia yake, kwa vile alikuwa anamdai fedha.

Zakaria yupo Gereza la Musoma, mkoani Mara akishikiliwa kutokana na tuhuma za kujaribu kuwaua kwa kuwapiga risasi maofisa Usalama wa Taifa, zogo hilo lilitokea mwaka jana katika ofisi yake mjini Tarime. Tuhuma nyingine inayomkabili Zakaria ni uhujumu uchumi.

Baadhi ya wananchi wanasema uongozi wa Luoga haukuakisi maendeleo ya wananchi wanyonge. Ikumbukwe kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimewahi kuwa na mgogoro na DC Luoga.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) aliwahi kumtuhumu kuhusika na fedha za ujenzi wa Kiwanda cha Sukari (Tarime Sugar).

Luoga ajibu mapigo

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu tuhuma hizo, Luoga amekanusha na kuziita uzushi mtupu.

“Watu bwana… watu husema ondoka usemwe! Tujifunze hata kusema mazuri mtu aliyoyafanya. Hayo wanayosema ni uzushi tu.

“Hiyo mashine ya kutengeneza mikate siyo ya milioni 25 kama walivyokwambia. Hiyo mashine mimi ndiye niliyemuagiza Zakaria aninunulie kutoka China.

“Alininunulia na kuniletea. Mashine ilikuwa ya Sh milioni 11.7 hivi. Ilikaa kwake baadaye nikaikomboa kwa kuuza gari la mke wangu.

“Yeye mwenyewe Zakaria alitafuta mnunuzi wa hilo gari, akampata. Nakumbuka gari hilo lilinunuliwa na Chomete, mpaka leo hii wanalo gari hilo hapo Tarime,” amesema Luoga.

“Acacia walikuwa wanakuja kuangalia ujenzi kisha wanatoa fedha. Fedha zote zilikuwa zikiingizwa kwenye akaunti ya kamati na imefanyiwa uchunguzi hadi Takukuru, hawakubaini wizi wala udanganyifu wowote.

“Sasa mimi nilichukuaje hizo fedha?” anahoji Luoga huku akisema anashangaa kama tuhuma hizo zinatolewa na Zakaria mwenyewe.

Amesema kama anadaiwa fedha wakafungue kesi mahakamani, si magazetini. “Kwa ufupi, hayo ni majungu na naomba usitumike,” amesema Luoga.

Luoga alikwenda mbali zaidi na kusema: “Zakaria ana matatizo yumo ndani. Watu wanasema kukamatwa kwake mimi nimehusika.

“Zakaria alikuwa rafiki yangu, rafiki yangu na ataendelea kuwa rafiki yangu,” amesema Luoga.

By Jamhuri