Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma

Leo naandika makala hii baada ya kutoka kanisani. Imenifikirisha nikiwa kanisani, hasa baada ya kukomunika katika kipindi cha ukimya, nikajiuiza hii habari ya CCM kuzindua Ilani yake ya 2025 – 2030 niandikeje? Nikajiuliza mafanikio makubwa waliyotangaza wakati wa uzinduzi wa Ilani hii, wakionyesha waliyofanya kwenye Ilani ya 2020 – 2025 niyaandikeje? Mara kichwani yakanijia maandiko matakatifu ya kuanza nayo.

Maandiko haya ni ya Zaburi ya 118:22 -24. “Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa BWANA, Nalo ni ajabu machoni petu. Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA, tutashangilia na kuifurahia.” Binafsi sitafanya tafsiri ya kidini katika neno hili kupitia makala hii, ila nitaeleza umuhimu wa Jiwe Kuu la Pembeni katika ujenzi wa nyumba.

Sitanii, kwanza nielezee kuwa waashi ni mafundi ujenzi. Tangu enzi za jadi, waashi/wajenzi wamekuwa wakitumia jiwe kuu la pembeni la msingi katika miradi yao ya ujenzi. Jiwe la pembeni ndilo nguzo kuu, mara nyingi linawekwa katika pembe ya jumba kubwa linalojengwa kutoa mwongozo kwa wajenzi katika ujenzi. Jiwe kuu la pembeni linakuwa mojawapo ya jiwe kubwa zaidi, gumu zaidi, na jiwe lililojengwa kwa umakini sana kati ya mawe ya jumba husika.

Kwa bahati mbaya, zipo nyakati katika kuchagua jiwe lipi linafaa, waashi hubagua baadhi ya mawe wakiona hayafai, lakini wenye nyumba wakikagua maendeleo ya ujenzi, hutumia macho ya ufundi wa asili, uzoefu na weledi, kwa baadhi ya nyakati huchagua jiwe lililokataliwa na waashi, hivyo kulifanya kuwa jiwe kuu la pembeni.

Kati ya mawe haya, waashi ambao ni wachache, kwa maana idadi ya wamiliki wa nyumba na mafundi wajenzi huwa wenye nyumba ndio wengi, kumbe kati ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa, wamiliki wa nyumba (Watanzania) wameichagua CCM ndiyo iwe jiwe lao kuu la pembeni. Baadhi ya mawe waliyochagua waashi, yamekataliwa na wenye nyumba.

Sitanii, swali ni je, CCM ni mwamba imara? Mimi mara zote nafanya uchambuzi. Natenganisha kati ya harakati na uhalisia. Penye nyeupe siwezi kusema ni nyekundu, na penye nyekundu siwezi kusema ni njano au kijani. Natamka rangi halisi. Kama ni kijani, kijani nitaitamka kama kijani. Kama ni maji ya bahari, nitaitamka kama maji ya bahari.

Narudia, Sitanii, kwanza kabla sijagusia hayo nitakayoyataja na kuiona CCM kuwa ni jiwe kuu la pembeni, naomba nieleze niliyoyaona kwenye mkutano wa CCM kati ya Mei 29 – 30, 2025. Kwa kuwamo katika ukumbi ule na kwa uzoefu wangu wa kuhudhuria mikutano mikuu ya CCM angalau kwa miaka 25 sasa, nasisitiza kwa jinsi Ilani ilivyowasilishwa na maudhui ndani ya Ilani, nimeona yafuatayo:-

Sitanii, macho na moyo wangu nimemwona Waziri Mkuu ajaye kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete. Macho na moyo wangu nimemwona Katibu Mkuu wa CCM ajaye. Macho na moyo wangu nimewaona Waziri wa Kilimo ajaye, Waziri wa Maji ajaye, Waziri wa Nishati au zaidi ajaye, Waziri wa Madini ajaye, Waziri wa Utalii ajaye, Waziri wa Elimu ajaye, Waziri wa Afya ajaye… Hii si kwa dhana ya kusadikika, bali kutokana na utekelezaji wa Ilani ya 2020 – 2025 na vipaumbele vya ilani iliyoziduliwa ya 2025 – 2030.

“Sitanii, macho na moyo wangu nimemwona Waziri Mkuu ajaye kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete. Macho na moyo wangu nimemwona Katibu Mkuu wa CCM ajaye. Macho na moyo wangu nimewaona Waziri wa Kilimo ajaye, Waziri wa Maji ajaye, Waziri wa Nishati au zaidi ajaye, Waziri wa Madini ajaye, Waziri wa Utalii ajaye, Waziri wa Elimu ajaye, Waziri wa Afya ajaye…”

Sasa nieleze kilichotokea ukumbini. Uwasilishaji wa taarifa ya serikali zote mbili ulikuwa wa kiwango cha juu. Serikali hizi za CCM zimeonyesha mafanikio makubwa mno kwa Zanzibar na Tanzania. Nafahamu zipo nyakati watu wanaweza kufumba macho gizani au kuwasha taa mchana, lakini hili halibadili ukweli. Nasema bila kigugumizi, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na ya kupigiwa mfano.

Niazime masikio, ninakusimulia kwa ufupi, hadithi aliyoisimulia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wakati anawasilisha taarifa ya Serikali: “Siku moja ndovu alikuwa anavuka mto akipita kwenye daraja. Kwenye sikio la ndovu ikawa yupo sisimizi. Ndovu alipolikanyaga lile daraja likatikisika sana. Alipovuka ng’ambo, sisimizi akamwambia ndovu ‘mimi na wewe tumelitikisa daraja’…”

Baada ya hadithi hiyo, Biteko alianza kusimulia mawaziri walivyokuwa kama sisimizi kwenye sikio la ndovu (Rais Samia), na kwa pmoja wakalitikisa daraja, huku akiwasilisha mafanikio ya serikali aliyofanya Rais Samia kwa mfano huo wa kulitikisa daraja. Alitaja ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kukamilika linalozalisha megawati 2,115 na kufanya kiwango cha umeme unaolizalishwa nchini kutoka megawati 1,602.32 na kufikia megawati 4,000 na ushei ukichanganya na vyanzo vingine vipya.

Katika kutaja jinsi Rais Samia “alivyotikisa daraja” akataja kuongezeka kwa usalama wa chakula kutoka asilimia 114 mwaka 2020 hadi asilimia 128 mwaka 2024. Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 18,665,217 mwaka 2020 hadi tani 22,804,316 mwaka 2024. Kuongeza matumizi ya mbolea kwa wakulima nchini kutoka tani 586,604 mwaka 2020 hadi tani 1,213,729 mwaka 2024. Kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 561,383 mwaka 2020 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2024. Na mengine mengi.

Alipotaja mafanikio ya elimu, afya, utalii, maji na mengine ambayo utekelezaji upo katika viwango vya kuvuka asilimia 100 ya kilichotarajiwa, na hasa baada ya hadithi ya sisimizi na ndovu, ukumbi mzima ukalipuka kwa kushagilia. Kwa Kizungu tunasema akapewa ‘Standing Ovation’ (wajumbe wote wakasimama) na kuimba CCM, CCM, CCM…

Ni wazi katika malengo ya maeneo mengi Ilani imetekelezwa kwa kuvuka viwango. Kwa mara ya kwanza nchi hii ina mashine za kisasa za kupima magomjwa mbalimbali katika kila hospitali ya wilaya. Kimsingi leo nimeona nijadili kilichotokea kwenye ukumbi. Katika makala zijazo nitachambua kwa kina kilichofanyika na CCM inacholenga kufanya katika miaka mitano ijayo.

Nafahamu kuna baadhi ya maeneo nchini yana barabara korofi, ikiwamo hii ya Banana – Kitunda, Dar es Salaam, ila nitayajadili siku zijazo. Jambo moja tu niliseme kwa leo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025 – 2030 imetambua umuhimu wa vyombo vya  habari kwa kuvitaja katika mikakati yake kwenye maeneo matano. Hili nimelipigania kitambo. Katika Ibara ya 3.3 Ilani mahususi inataja Huduma za Habari na Mawasiliano ambapo moja ya malengo ni: “Kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi wa vyombo vya habari ili kuiwezesha sekta ya habari kutoa mchango wake kikamilifu katika shughuli za maendeleo.”

Hili ni suala la msingi. Habari ni sekta wezeshi inayowezesha haki nyingine za binadamu kupatikana na maendeleo katika maeneo mbalimbali. Ni matamanio yangu kuona hata vyama vya upinzani vikiweka kipaumbele katika suala hili la vyombo vya habari. Tukiviacha vyombo vya habari vikafa kwa kukosa uchumi imara, tutajikuta tumechana mkeka wa jamii yetu, na ipo siku tutajuta. Nihitimishe kwa kusema hakika Rais Samia ametenda zaidi ya kilichotarajiwa kwa Watanzania. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827