Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wiki iliyopita nimesoma habari na kusikiliza matamko kwenye mitandoa ya kijamii. Nimemsikiliza askofu Josephat Gwajima. Kwanza niwape pole wakaazi wa Jimbo la Kawe. Nazifahamu ahadi alizozitoa kwao Askofu Gwajima. Mara Japan, Birmingham, magreda, kufufua wafu, kuigeuza Kawe kuwa Ulaya na nyingine kedekede. Sitazungumzia hata chembe ahadi yake ya kufufua misukule.
Gwajima alifahamiana na marehemu Wilbroad Mkinga, a.k.a. Mkinga Mkinga. Mkinga alipata kuwa Mkurugenzi mwenzetu tangu mwaka 2019 hadi Mungu alipomtwaa Juni, 2021. Mungu amlaze Mkinga mahala pema peponi. Kuna kazi Askofu Gwajima alitupatia sisi Gazeti la JAMHURI, wakati wa harakati zake za kugombea ubunge Kawe. Tulitangaza malengo yake. Tulimpatia ankara ya malipo ya EFD. Hadi leo tangu mwaka 2020, labda atatulipa akitoka madarakani.
Nimegusia tukio hilo kuonyesha ujasiri wa Gwajima. Jamani nchi hii ina tabu. Kuna wajasiriamali wanaopitia katika dini. Kwao maadili ni sifuri. Malengo yao ni kuwapumbaza waumini na mwisho wa siku kuvuna sadaka na matoleo. Yapo makanisa kongwe kama Wakatoliki, KKKT, Anglikana na wengine, wema sana. Lakini wapo wapigaji.
Ni kwa bahati mbaya nchi yetu inalea jini katika chupa. Yapo mambo sikubaliani na Rais Paul Kagame wa Rwanda, lakini kwa hakika nakubaliana naye katika kufuta makanisa ya wajasiriamali. Rais Kagame ameweka vigezo. Anayeitwa Mchungaji angalau lazima awe na shahada ya kwanza ya Theolojia nchini Rwanda. Hii imefuta makanisa hewa mengi nchini Rwanda.
Sitanii, najua msomaji utaniambia Gwajima ni msomi kwa kiwango cha uzamivu, yaani shahada ya udaktari wa falsafa (PhD). Hivi tunajiuliza, Gwajima aliingiaje bungeni? Ukiacha PhD yake, mnamkumbuka aliyesema “Nileteeni Gwajima?” Je, ni sahihi viongozi wetu kutumia dirisha la dini kuingia bungeni? Je, waamini wake hata kama hajafufua msukule mmoja bado wanaendelea kumwamini?
Kila kitu kina mipaka. Siijui Katiba ya Kanisa la Gwajima, lakini sisi hatujawahi kumhoji maaskofu wa kanisa lake wanapatikanaje. Kuhoja mamlaka ya Rais kuteua na kutengua, si tu ni utovu wa nidhamu, bali ni kosa la kimantiki. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu wa Rais kuteua na kutengua nyadhifa mbalimbali.

Rais kutumia mamlaka hayo, na baadaye Gwajima akahoji kuteuliwa na kutenguliwa kwa wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, ni utovu wa maadili.
Si hilo tu, kitendo cha Gwajima kuyataka majeshi ya nchi hii kuingia kwenye sekta za uzalishaji, ikiwamo ujenzi kwa nia ya kuzalisha faida kubwa na kujilipa mishahara mikubwa ni uchochezi usiostahili. Kwamba Gwajima anachochea askari wafanye nini?
Ndugu zangu Watanzania, inawezekana tunasikia tu. Tumshukuru Mungu kwa kuwa na taifa hili lenye utawala wa kiraia. Jambo moja nakubaliana na Gwajima, hakuna Mtanzania anayepaswa kupotea. Hili sote tunalikataa duniani na mbinguni. Watanzania wasipotee, wasitekwe. Swali ni moja, nani anawateka? Tunamkumbuka yule wa Noah? Kesi yake mbona hatuifuatilii?
Ninaye rafiki yangu mwingine aliyenikumbusha mkasa wa Wilfred Lwakatare na utekaji akiwa CHADEMA. Je, yaliyosemwa wakati huo yamekwisha? Hivi ni lazima Watanzania tutafute madaraka kwa gharama ya uhai wa wenzetu? Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila Mtanzania awe huru kushiriki mikutano ya hadhara, awe chama tawala au upinzani. Je, tunao uhuru ndani ya vyama vyetu?
Sitanii, na samahani, je, tuko sahihi kuwaruhusu viongozi wa dini kama akina askofu Gwajima na wenzake kuwa wabunge? Najaribu kuwaza kwa sauti tu. Je, ni sahihi kuendelea kuwaruhusu wachungaji kuwa wanasiasa? Je, mchungaji akiwa mwanasiasa kanisa linakuwa katika mikono salama na hasa kwa kutilia maanani wanachama wasio wafuasi wa chama cha mchungaji?
Sitanii, Gwajima, mimi sitaki kumwita askofu, na kwamba yeye ni sikio la kufa. Sina uhakika kama si mjasiriamali wa kiimani, ambaye huenda ubunge wake Kawe, kwake umekuwa fursa. Ukiacha mapadri wachache binafsi, sijaona askofu wa Kanisa Katoliki anayetamani kugombea Jimbo la Uchaguzi kwenye siasa. Akithubutu anapoteza wadhifa wake. Sisemi ndivyo, ila wengi wanakubali kuwa Kanisa Katoliki ukisikia anaitwa askofu, basi huyo ni askofu kweli.
Nisahihishwe katika makala hii kama nimekosea. Sijaona askofu wa kweli kutoka Kanisa Katoliki, Anglikan au KKKT akiwania ubunge au udiwani kupitia chama chote cha siasa, ila haya makanisa mlengezo. Narudia, Gwajima ameambiwa mara nyingi kuwa asichanganye siasa na dini, ila huyu bwana inaelekea ni sikio la kufa halisikii dawa. Naomba kama Watanzania tumpuuze kwa karibu yote aliyosema, yanalenga kutetea nafasi yake jimboni. Kitendo cha kuacha mimbari akaenda kwenye siasa, tayari lilikuwa doa kubwa.
0784 404 827