Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Wafanyabiashara zaidi ya 300 waliokuwa wakifanya shughuli zao katika Soko la Rehema Nchimbi jijini Dodoma wameiomba Serikali kuingilia kati kwa haraka kutatua mgogoro unaohusu eneo mbadala la Umonga, kufuatia kushindwa kuendelea na shughuli zao za biashara kwa zaidi ya miezi saba baada ya kuhamishwa kutoka eneo lao la awali lililochukuliwa na Bunge la Tanzania Oktoba mwaka jana.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2026 katika eneo la Umonga, ambalo wanasema walipewa kama suluhisho la muda na baadaye la kudumu na Serikali, wafanyabiashara hao wamedai kuwa hadi sasa wamezuiwa kufanya biashara katika eneo hilo, hali inayowaweka katika changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.
Prisca Chibwaye, mmoja wa wafanyabiashara hao, amesema tangu walipoondolewa kwenye maeneo yao ya awali mwaka jana, wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kukosa eneo rasmi la kufanyia biashara licha ya juhudi mbalimbali za ufuatiliaji.
“Mwaka jana tuliondolewa kwenye vibanda vyetu bila fidia baada ya eneo kuchukuliwa na Bunge. Tunashukuru Serikali kupitia uongozi wa mkoa kututafutia eneo hili la Umonga, lakini hadi sasa haturuhusiwi kufanya biashara hapa,” amesema Chibwaye.
Ameongeza kuwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba mapema mwaka huu, alitoa maelekezo kuwa wafanyabiashara hao wahamishiwe rasmi katika eneo la Umonga na lifanyiwe maboresho ya miundombinu ikiwemo kumwaga kifusi ili kuzuia mafuriko na kulifanya liwe la kudumu, lakini utekelezaji wa maelekezo hayo haujakamilika hadi sasa.
“Waziri Mkuu alielekeza eneo hili liwe la kudumu baada ya kuboreshwa, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika. Tumeachwa bila shughuli za biashara kwa muda mrefu,” ameongeza.
Wafanyabiashara hao wamesema hali hiyo imewaweka katika hali ngumu ya maisha, ambapo wengi wao wameshindwa kulipa mikopo waliyochukua katika taasisi za kifedha, huku wengine wakilazimika kuuza mali zao za nyumbani ili kukidhi mahitaji ya msingi ya familia.
“Tuna mikopo benki, watoto wanahitaji ada na chakula, lakini biashara zetu zimesimama kwa miezi saba sasa. Maisha yanazidi kuwa magumu kila siku,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Wameiomba Serikali kuingilia kati ili kuruhusu matumizi ya haraka ya eneo hilo la Umonga ili waweze kurejea kwenye shughuli zao za kiuchumi kama ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa Soko hilo, Abdullah Gogo, amesema kufungwa kwa Soko la Rehema Nchimbi Oktoba 29 mwaka jana kumeathiri moja kwa moja zaidi ya wafanyabiashara 300 waliokuwa wakitegemea kipato cha kila siku.
Amesema changamoto kubwa si uamuzi wa Serikali kuhamisha soko hilo, bali ni ucheleweshaji wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kuhusu maandalizi ya eneo mbadala.
Aidha, wafanyabiashara hao wamedai kuwa licha ya maagizo ya Serikali ya kumwaga kifusi kwa takribani magari 18 katika eneo hilo, ni kiasi kidogo tu ndicho kilichofikishwa, huku eneo hilo likikosa huduma muhimu kama maji, umeme na vyoo.
Hata hivyo, uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia Nsubisi Kapura umeeleza kuwa ucheleweshaji wa matumizi ya eneo hilo unatokana na baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kusaini mikataba ya matumizi ya eneo hilo.
Amesema jiji liliandaa mikataba rasmi, lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekataa kuisaini huku wakitaka kuanza biashara bila kukamilisha taratibu za awali, pamoja na kuomba kuongezwa kwa idadi ya wafanyabiashara zaidi ya waliopo kwenye orodha rasmi.
“Suala la mkataba ni la msingi kisheria. Eneo ni mali ya Serikali, haliwezi kutumika bila makubaliano rasmi,” amesema Kapura.
Katika mazingira hayo, wafanyabiashara hao wameendelea kuiomba Serikali kuingilia kati kwa haraka ili kuweka mwafaka utakaowawezesha kurejea katika shughuli zao za kiuchumi, huku wakisema kila siku inayopita inaongeza mzigo wa maisha na madeni kwao.






