Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, ameitaka serikali kuweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuwapa kipaumbele katika upatikanaji wa ardhi ya kilimo na ufugaji, badala ya kuwaachia wawekezaji wakubwa pekee.

Wito huo umetolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ngare Nairobi, wilayani Siha, baada ya kiongozi huyo kukamilisha ziara ya uzinduzi wa vizimba vya chama hicho katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Akihutubia wananchi, Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wenyeji, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mikakati inayohakikisha wananchi wa Siha hawakosi maeneo ya kulima na kuchungia mifugo yao.

“Ni muhimu wananchi wapewe kipaumbele cha kwanza katika maeneo yao ili kuendesha maisha yao, badala ya ardhi kutolewa kwa wawekezaji huku wenyeji wakibaki kutangatanga bila uhakika wa maeneo ya uzalishaji,” alisema kiongozi huyo.

Aidha, alihimiza mamlaka husika kuangalia upya changamoto za ardhi katika wilaya hiyo ili kuwaondolea wananchi uwezekano wa kukosa mwelekeo na vyanzo vya uhakika vya riziki zao.