Home Burudani Chaka Chaka Mwanamuziki shupavu

Chaka Chaka Mwanamuziki shupavu

by Jamhuri

Yvonne Chaka Chaka, mwimbaji, mtunzi wa nyimbo, mjasiriamali, mtetezi wa haki za wanyonge na mwalimu wa wengi nchini Afrika Kusini, jina lake limeorodheshwa kwenye orodha ya wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa Afrika.

Jarida la Avance Media la Marekani ambalo hujishughulisha kutafiti na kuchapisha majina ya watu maarufu wenye ushawishi kila mwaka limeweka jina lake katika orodha hiyo.

Jarida hilo katika kuandaa majina hayo hujumuisha majina ya wanasiasa, waigizaji, waanzilishi wa taasisi mbalimbali, wanamichezo na wanawake wengine wanaofanya kazi zenye kugusa maisha ya watu barani Afrika.

Hellen Johnson, aliyekuwa Rais wa Liberia, jina lake limeorodheshwa humo, Lupita Nyong’o, raia wa Kenya na muigizaji anayefanya vizuri kwenye jumba mashuhuri la maigizo la Hollywood nchini Marekani yumo na Mtanzania Joyce Msuya, mtaalamu wa Sayansi ya Mazingira naye yumo.

Joyce Msuya anafanya kazi katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) Kitengo cha Mazingira nchini Kenya, akihudumu cheo cha katibu mkuu msaidizi katika ofisi hizo.

Huandikwi kwenye jarida hilo kama kazi zako hazina mchango mkubwa kwenye jamii. Ni kupitia sifa hiyo, kazi za Chaka Chaka alizofanya kupitia sanaa yake ya uimbaji zimemuweka katika orodha hiyo.

Mwaka 2017 alishinda tuzo ya kimataifa katika shindano la kila mwaka linaloandaliwa na Black Entertainment Television (BET) nchini Marekani.

Tuzo hiyo aliyopata ilimtambua kama mwanamke anayetumia sauti yake kutetea wanyonge nchini Afrika Kusini.

Alipata tuzo hiyo baada ya kushinda kwenye kinyang’anyiro cha ‘International Global Good Award’.

Mbali na tuzo hiyo, jina lake limewahi kutajwa kuwa miongoni mwa majina manane ya watu wenye ushawishi barani Afrika.

Kutokana na nyimbo zake nyingi kumpa umaarufu duniani, Chaka Chaka anaongoza kwa kushirikishwa kwenye kampeni mbalimbali zikiwemo za kuzuia ugonjwa wa malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Jarida hilo la Avance Media pia limeorodhesha majina ya msanii Tiwa Savage wa Nigeria, Khadja Nin wa Burundi pamoja na Oumou Sangare wa Mali.

You may also like