N Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila,ametoa siku saba kwa watumishi wa makao makuu mamlaka ya Bandari(TPA),kubadilika kabla hajaanza kuchukua hatua dhidi yao.

Chalamila, ametoa agizo hilo wakati akiongea na watumishi wa mamlaka hiyo wakati akikagua shughuli mbalimbali zinazozifanya.

Aliongelea juu ya uholela wa mialo, unaopelekea upitishaji wa madawa ya kulevya.

Amesema kuna mbinu nyingi zinatumika kupitisha dawa hizo ikiwemo kuweka kwenye nyama zinazokwenda Visiwani.

Amesema upitishaji wa mizigo ambayo hailipiwi kwa kutopewa namba ya malipo mfano mizigo ya barafu, mafuta.

“Ninawapa wiki moja tu ya kubadilika kabla ya kuanza kuchukua hatua kwani huduma hii wanayoitoa ni ya umma”amesema.

Hata hivyo aliwataka Watumishi hao wa Bandari kuwa waadilifu, kuheshimiana, kuzingatia maadili ,miongozo na kutekeleza majukumu yao kama taratibu zinavyowataka na kuwaelekeza.

“Mimi sehemu kubwa naangalia mapato ya umma, hivyo ninachoweza kusema bado hakuna utaratibu mzuri wa kibandari, uchakavu wa miundombinu na matumizi sahihi ya teknolojia. Kama bandari haina schanner ni jambo la hatari sana, hili ni muhimu sana Meneja kulishughulikia kwa nguvu na kwa uharaka sana” amesema Chalamila.

Wakati huohuo, mkuu wa mkoa Chalamila ,amewapongeza watumishi wa Shirika la Umeme (TANESCO ) kuendelea kufanya kazi kwa umoja na mshikamano, kuheshimiana na kupendana katika kutekeleza majukumu yao.

“Na kuwataka waondolee dhana ya kufanya kazi Kagera ni mbali, si kweli kuwa Kagera ipo mbali kwani ipo ndani ya mipaka ya Tanzania wasijione wanapita bali wafanye kazi kama wapo nyumbani ili wawe madhubuti”alisema mkuu huyo wa Mkoa.

Sanjari na hilo ameeleza kuwa umeme ni hitaji la sekta nyingi kama kilimo hivyo watambue umeme ni hitaji la muhimu.

Amewataka watumishi hao kusimamia miradi kwa umakini na uaminifu, endapo kuna wizi wowote ukitokea waweke wazi ili viongozi wafahamu.

Hata hivyo amewataka kusimamia ubora wa bidhaa kama nyaya za umeme kwa kutoa elimu kwa watumiaji ili kujua umuhimu wa bidhaa bora sambamba na kufanya ukaguzi kwenye maduka yanazouza bidhaa hizo, endapo bidhaa hizo si bora basi watoe ushauri ili kuepusha hasara ikiwemo kuungua kwa nyumba.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Projestus Rubanzibwa, amewaeleza kuwa ili kujua utendaji kazi katika Taasisi hizo kuanzia sasa kila Taasisi iwe inawasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zao kila robo mwaka.

Amesema hii itawezesha ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya ufuatiliaji wa masuala mbalimbali pale watakapokuta kuna matatizo.

By Jamhuri