CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Pwani (PWMO), kimetoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu (Shalom) kilichopo Msangani, Halmashauri ya Mji Kibaha.

Misaada hiyo ni pamoja na mchele, unga, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni na maharage lengo likiwa ni kuwafariji watoto hao ambao baadhi yao hawana wazazi na wengine wametoka kwenye mazingira hatarishi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo ,Makamu Mwenyekiti wa PWMO Marietha Msembele amesema, misaada kwenye vituo kama hivyo ni endelevu na wataendelea kutoa katika maeneo mengine ndani ya mkoa huo.

“Tumekuja kutoa msaada wetu katika kituo hiki Cha Shalom kuunga mkono jitihada zinazofanya na Mkurugenzi ambaye amefanikiwa kuwakusanya watoto hawa na kuwafanya nao wajumuike kwa pamoja na kuishi vizuri na kupata huduma muhimu kama wengine,” amesema Marietha.

Aliwashukuru wadau ambao huwa wakishirikiana na chama hicho, na kuwaomba waendelee kuwapa ushirikiano kufanya masuala mbalimbali ndani ya jamii.

Mmoja wa Wajumbe Futuna Suleman amewaomba wadau wengine wenye uwezo kujitokeza kusaidia watoto kama hao Ili wapate mahitaji kama wengine.

Mkurugenzi wa kituo hicho Lilian Mbise, amewashukuru wanachama wa chama hicho kwa msaada huo na kusema hadi sasa wanalea watoto wapatao 54.

” Hiki mlichotoa mtaona kidogo lakini kwetu ni kikubwa kuwapa hawa watoto mlo mmoja sio kazi ndogo huwezi kwenda dukani ukakopa chakula wakakupa lakini mnavyotutia moyo hivi tunajisikia kufarijika,” amesema.