Utafiti uliofanyika nchini Uingereza unaonyesha kuwa gharama kwa wazazi ya kutunza mtoto kuanzia anapozaliwa mpaka kutimiza miaka 21 zilikuwa ni Paundi (£) 227,267 za Uingereza. Hii ni taarifa ya mwaka 2014 na ni kwa mujibu wa kituo cha utafiti wa uchumi na biashara kinachojulikana kwa Kiingereza kama Centre of Economic and Business Research (CEBC).
Si gharama ndogo hata kwa Waingereza wa hali ya kawaida ambao baadhi yao wanalazimika kupunguza idadi ya watoto wanaozaa kwa kushindwa kumudu gharama hizo. Ni Watanzania wachache mno wanaoweza kumudu gharama hiyo ambayo ni sawa na malipo ya kila mwezi ya karibia Sh 3,240,000 kufurahia majaliwa ya kupata mtoto. Kila mwezi kwa miaka 21.


Kama wazazi wa Tanzania watajikuta wanakabiliana na gharama za aina hii kwa ajili ya kulea watoto wao, basi wazazi wengi wasingefikia hata kuwaza tu kupata watoto. Kupata watoto lingekuwa jambo ambalo lingeweza kuonekana kwa matajiri tu.
Hali halisi ilivyo ni kuwa hutakuta wanandoa wasio na watoto wanahudhuria warsha, kongamano, au kwenda kwenye safari za mafunzo ili kupata mafunzo yatakoyowaandaa kufikia uamuzi kama kuna faida au hasara ya kuzaa watoto, kama ambavyo baadhi wangefanya kwa uamuzi mwingine wa maisha yao. Mara nyingi kinachotokea ni baba kupewa taarifa na mama kuwa baada ya miezi tisa ajiandae kupokea kichanga kwenye familia.


Labda tuna bahati kuwa haigharimu kiasi kile kile kama kumlea mtoto nchini Uingereza ingawa hata hapa Tanzania si rahisi kumlea mtoto na kumpatia mahitaji yake yote muhimu.
Kwenye ule utafiti wa Uingereza malezi ya mtoto yanagharimu £66,113 (Sh 237,555,907), au asilimia 29 ya gharama zote; pesa ambazo zinatumika kuajiri mfanyakazi wa nyumbani wa kuangalia mtoto pale mzazi anapokuwa anafanya kazi au hayupo nyumbani. Kwa mzazi Tanzania hii ni gharama ambayo inaweza kuepukika au kupunguka kwa kiwango kikubwa pale ndugu au jamaa wanaposaidia kulea mtoto ingawa kwa wakazi wa mjini hawa ndugu na jamaa siyo rahisi kuwapata.


 Katika kipindi cha miaka 21 mzazi wa Uingereza analazimika kulipia £73,803 kwa elimu, £19,804 kwa chakula, £10,935 kwa nguo, £16,506 kwa safari za likizo, £9,433 kwa michezo na vitu vya kuchezea, £7,419 kwa burudani mbalimbali, na £23,254 kwenye matumizi mengine mbalimbali.
 Wazazi wengi Watanzania, hata wale wenye uwezo, hawatalipia baadhi ya gharama zilizoainishwa kwenye utafiti huu, kwa mfano, safari za likizo, michezo na vitu vya kuchezea, na burudani mbalimbali. Mzazi Mwingereza anaweza kumlipia mwanaye gharama za kujifunza kuendesha gari au hata kumnunulia gari jipya; jambo ambalo likitokea Tanzania tutalisoma kwenye magazeti kwa sababu kwa wengi halitakuwa la kawaida.
Nimesikia taarifa za baadhi ya wazazi Tanzania kuwanunulia watoto wao magari, lakini hapa tunazungumzia wachache kati ya mamilioni ya Watanzania. Kwa wazazi wengi jambo muhimu kwao ni kumpatia mtoto chakula, sehemu ya kuishi, tiba, na elimu. Kwa kundi jingine la wazazi chakula tu ndiyo muhimu, mengine yatapatikana kama hali inaruhusu.


Wazazi wenye uwezo wa kulipia elimu ya watoto wao watatarajia kuwa mtoto anapopata elimu nzuri na ajira inayolipa vizuri, labda mzazi ataweza kustaafu akiishi maisha ya kupokea zawadi, safari za likizo, nguo mpya na pengine hata gari mpya kutoka kwa mwanawe. Yale ambayo mzazi hakumpa mwanae atatarajia kuyapata kutoka kwake. Naamini kuwa mila na desturi zetu bado zinamfanya mtoto yule yule ambaye amelelewa katika mazingira magumu kuona fahari kuwapa wazazi wake maisha bora kuliko alioyokulia mwenyewe.
Elimu inaendelea kuwa kipengele cha malezi ambacho kinaumiza vichwa vya wazazi na jambo linalotumia rasilimali kubwa ya wazazi katika jitihada ya kuweka msingi mzuri wa maisha ya baadaye ya kizazi kinachofuata, pamoja na kuwa kitega uchumi ambacho wazazi watakachovuna uzeeni.
 Umuhimu wa elimu unaonekana pale ambako katika miezi ambayo karo za shule na gharama nyingine zinadaiwa wazazi hulazimika kusitisha matumizi mengine yasiyo muhimu kulipia watoto wao. Baadhi ya wazazi hukopa kipindi hicho kikiwadia. Mzigo huu wa elimu umekuwa kilio kikubwa cha wazazi wengi ninaozungumza nao hata hapa Butiama.


Baadhi ya matumizi yanatokana na ufinyu kwenye pesa zinazotengwa na serikali kwa ajili ya elimu na ni suala ambalo limekabili serikali za awamu zote. Kumwandikisha mwanafunzi kwenye shule ya sekondari ambayo inayo majengo, lakini ina walimu watatu pekee haiwezi kuwa misingi imara ya elimu.
Haya ndiyo maoni ya mzazi mmoja ambaye mwanae alichaguliwa kujiunga na shule mojawapo ya sekondari iliyopo Butiama miaka kadhaa iliyopita, lakini mzazi akaamua kumhamishia shule nyingine ya bweni na kulazimika kulipia gharama za ziada kwa ajili ya uhamisho huo.
Tayari alikuwa na mtoto wa kiume ambaye anahangaika kumlipia gharama za elimu na ambaye hubaki shuleni mkoani Mtwara kwa sababu mama yake hawezi kumudu gharama za kumlipia nauli ya kurudi Butiama.


 Jambo la kushangaza ni kuwa huyu mzazi ambaye anahangaika kusomesha watoto wawili bado anaamini kuwa angekuwa na watoto wengi zaidi, basi angepungukiwa na mzigo wa gharama aliyonao. Kwake yeye, watoto wengi zaidi ni ongezeko la nguvukazi nyumbani na ni uwepo wa watoto ambao wataongeza kipato cha kuwalipia wenzao waliovuka kuingia sekondari. Tunafahamu pia kuwa mara nyingi wale wanaobaki nyumbani huwa ni watoto wa kike.
Hii ndiyo hali halisi ya wazazi wengi nchini Tanzania wanaohangaika kusomesha watoto wao. Hawana gharama kubwa kama wazazi wa Uingereza, lakini bado wanajikuta wakikabiliana na mzigo mkubwa wa kulea watoto mpaka kufikia hatua ya watoto kuweza kujitegemea.

 

By Jamhuri