Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) umekutana kujadili masuala muhimu matatu, likiwemo kusaini makubaliano ya kiutendaji (MoU) yanayolenga kuimarisha kazi za umoja huo kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.

Katika kikao hicho, CoRI pia imepitia nyaraka mbalimbali za utendaji kazi kama vile Mpango Mkakati na Mkakati wa Mawasiliano, kwa lengo la kuhakikisha ujumbe wa umoja huo unamfikia ipasavyo mwananchi na jamii kwa ujumla, kwa mujibu wa dira ya miaka minne waliyojiwekea.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho jana Mei 12,2025, Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura amesema umoja huo umejipanga kukuza uhuru wa vyombo vya habari na uwajibikaji, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi.

“Vipaumbele vyetu ni pamoja na usalama wa waandishi wa habari, kuhakikisha kuwepo kwa miundombinu na mbinu rafiki za kufanikisha utendaji kazi bora. Pia tunasisitiza usimamizi wa sheria za uchaguzi kama zilivyoainishwa na Tume Huru ya Uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia weledi katika utoaji wa taarifa,” amesema Sungura.
Aidha, ameeleza kuwa CoRI haitachoka kupigania haki ya waandishi wa habari kupata taarifa, kwani bila taarifa hakuna uandishi wa habari wa kweli na hivyo, hakuna vyombo vya habari vinavyoweza kuwahabarisha wananchi.

Sungura ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ameongeza kuwa maandalizi kuelekea uchaguzi huo yameshaanza, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa waandishi wa habari na upatikanaji wa vitendea kazi vitakavyotumika katika kipindi cha uchaguzi.

Kwa sasa, CoRI inaundwa na wanachama kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika ,Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Chama cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Wengine ni Ofisi ya Habari kwa Wananchi wa Tanzania (TCIB), Sikika, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), JamiAfrica, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Twaweza, OJADACT, Policy Forum, Shirika la Maendeleo na Habari Tanzania (TADIO), na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).