Ukweli dhidi ya uzushi

Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa corona miezi kadhaa iliyopita, kumekuwa na taarifa nyingi zinazotolewa kupitia vyanzo mbalimbali. Lakini baadhi ya taarifa hizo hazina ukweli kuhusiana na ugonjwa huo.





Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia), akiwa na Naibu wake, Dk. Faustine Ndugulile, akitangaza kubainika kwa mtu wa kwanza kuwa na virusi vya corona nchini.

Zipo taarifa nyingine ambazo ni za uzushi ingawa wanaozitoa wanataka kuwaaminisha watu kuwa ni za ukweli. Kwa kupitia vyanzo mbalimbali, JAMHURI linakuletea baadhi ya mambo ya msingi kuhusu corona, yakibainisha taarifa za kweli na zile ambazo ni uzushi.

Chanjo ya kuzuia virusi vya corona (Covid-19) ipo

Hii si kweli. Ukweli ni kuwa hivi sasa wataalamu ndiyo wamo katika majaribio ya chanjo hiyo. Itachukua muda mrefu (zaidi ya miezi 15) kupata chanjo ambayo imethibitishwa kuwa salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Unaweza kujitibu corona kwa kunywa maji ya chumvi, mafuta au vitu vyenye tindikali

Hii nayo si kweli. Vitu hivi vilivyotajwa, na vingine vingi, havitibu corona kwa sababu hadi hivi sasa wataalamu bado hawajathibitisha dawa mahususi ya ugonjwa huu.

Njia kubwa za kujikinga na maambukizi ya corona ni pamoja na kuosha mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni, kutumia vitakasa (sanitizers), kutokukutana na watu walioambukizwa – hasa wanaokohoa au kupiga chafya.

Pia, iwapo umeambukizwa, unaweza kuzuia kusambaa kwa vijidudu vya corona kwa kuziba kinywa chako kwa eneo la kiwiko cha mkono unapokohoa au kupiga chafya na kutokaribiana na watu wengine.

Virusi vya corona vimetengenezwa makusudi ili kudhuru watu

Hili nalo si jambo la kweli. Kwa kawaida virusi vinabadilikabadilika sana. Mara kadhaa, ugonjwa huanza kwa virusi ambavyo hukaa kwa wanyama wengine kama vile nguruwe, popo au ndege vinapobadilika na kuweza kuingia katika mwili wa binadamu. Kwamba, virusi hivi vimetengenezwa maabara na kuachiwa kwa makusudi ni tuhuma ambazo hadi sasa hazijathibitishwa.

Kununua vitu vilivyotokea China kunaweza kusababisha uambukizwe

Si kweli. Ingawa virusi vya corona vinavyoisumbua dunia hivi sasa (Covid-19) vimeanzia China, hiyo haimaanishi kuwa kila kitu kinachotoka China kina virusi hivyo. Wataalamu pia wanaeleza kuwa virusi hivi vya corona haviishi muda mrefu kwenye vitu vingine tofauti na mwili wa binadamu. 

Hivyo, ni vigumu sana kwa kitu kusafirishwa kutoka China na kufika nchi nyingine vikiwa na virusi hivyo vikiwa bado hai, kwa sababu hata kama vitatoka China vikiwa na virusi, wadudu hao watakuwa wameshakufa hadi kuifikia nchi nyingine. Virusi vya corona huambukizwa kupitia matone ya mate, mafua au majimaji mengine kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.

Kuvaa barakoa (mask) ni lazima

Si kweli. Ingawa wengi wameaminishwa kuwa kuvaa barakoa kunaweza kukukinga dhidi ya maambukizi ya corona, lakini wataalamu wanashauri kuwa wahudumu wa afya (hasa wanaoshughulikia wagonjwa wa corona au washukiwa), watu wanaoonyesha dalili au wanaougua na wale ambao wamo kwenye mikusanyiko ya watu ndio wanastahili kuvaa barakoa.

Mtu asiyeambukizwa virusi hivi si lazima avae barakoa, isipokuwa atakapokuwa kwenye makundi ya watu. WHO inashauri busara katika matumizi ya barakoa, kwa kuwa zimekuwa adimu sana duniani.

Hata wale wanaovaa, hawatakiwi kuivaa barakoa moja kwa muda mrefu, kwa sababu inaweza kuwasababishia matatizo.

Ukiambukizwa Covid-19 utakufa

Si kweli. Ni watu wachache sana wanaoambukizwa virusi hivi ambao wanakufa. Wengi wa wanaoambukizwa hutibiwa na kupona kabisa. Hesabu zinaonyesha kuwa ni asilimia tatu tu ya watu wanaoambukizwa Covid-19 ndio wanafariki dunia. Hii ni idadi ya chini ukilinganisha na virusi vingine kama vile SARS ambavyo huua asilimia kumi ya walioambukizwa na MERS ambavyo huua asilimia 35 ya walioambukizwa.

Inaelezwa kuwa watu wenye umri mkubwa (zaidi ya miaka 60) ndio ambao wamo kwenye hatari ya kufa kwa corona kutokana na kinga yao ya mwili kuwa chini sana. Hata hivyo, virusi vya corona husambaa kwa kasi kuliko aina hizo mbili za virusi.

Kila mtu yumo hatarini kuambukizwa

Ni kweli. Hakuna ambaye ana kinga dhidi ya maambukizi ya corona. Kama tulivyoeleza hapo juu, watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 60 ndio wamo hatarini zaidi kuambukizwa na kuugua kuliko wale wenye umri mdogo.

Matumizi ya kiua vijasumu (antibiotic) yanaponya corona

Si kweli. Viua vijasumu (antibiotics) haviui virusi vilivyo katika mwili wa binadamu, hivyo kuitumia kama dawa au kinga hakusaidii chochote. Ni muhimu kujikinga lakini ujikinge kwa kutumia njia zilizothibitishwa na wataalamu kama tulivyoainisha hapo juu.

Unaweza kuambukizwa corona na mbwa/paka wako

Inaweza kuwa kweli, lakini ni jambo lisilowezekana kiurahisi. Ingawa upo uwezekano wa virusi vya corona kuishi katika miili ya wanyama hao, lakini mfumo wa virusi kutoka kwa mbwa au paka, kujibadilisha na kuweza kuishi kwenye mwili wa binadamu na kuleta madhara ni mgumu sana kiasi kwamba ni vigumu kwa mtu kuambukizwa moja kwa moja kutoka kwa wanyama hao.

Kumbuka hata corona hii ya sasa, ingawa inaelezwa kuwa ilitoka kwa popo, lakini virusi viliingia mwilini mwa binadamu kupitia chakula kilichokuwa kinauzwa kwenye soko la vyakula vya baharini.

Kina nani wamo hatarini zaidi kupata corona

Wakati tafiti zikiendelea kufahamu zaidi namna ugonjwa huu unavyoathiri binadamu, wazee na watu wenye magonjwa ya muda kama shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, magonjwa ya mapafu, saratani na kisukari, wameonekana kushambuliwa zaidi kuliko wengine.

By Jamhuri