Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Bodi ya usajili wa makandarasi nchini (CRB) imetakiwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya makandarasi wote wanaothibitishwa kukiuka wajibu wao.
Waziri wa ujenzi Abdala Ulega alizungumza hayo, wakati wa uzinduzi wa mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi uliofanyika leo Mei 15, 2025 ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam.
Ulega amesema sekta ya ujenzi ni muhimu katika kuchangia na kuimarisha miundombinu bora kama vile barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, maji, majengo, umeme, na mawasiliano ya simu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi .

Amesema Serikaki imekuwa ikitoa nafasi kwa sekta binafsi ,kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini.
“Nawapongeza bodi kwa kuanzisha utaratibu huu wa kukutana na wadau kwa mashauriano kila mwaka, kwani mnapata nafasi ya kuelewa na kujadili changamoto za makandarasi na kama mlivyosema, mnafikia maazimio na mapendekezo ya namna ya kuzitatua changamoto hizo”.amesema.
Ulega amesema ni muhimu kwa makandarasi wote kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa ufanisi na kufuata makubaliano katika mikataba ya miradi husika,kwani wanaposhindwa kutimiza wajibu wao, wanachelewesha wananchi kupata huduma zinazokusudiwa na pia wanaipelekea serikali hasara.
“Napenda kuwahakikishia kwamba serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawaunga mkono na inathamini mchango wenu katika uchumi wa nchi yetu” amesema.

Amesema kwa sasa Serikali itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha makandarasi, wanapata malipo yao kwa wakati kwani ucheleweshaji wa malipo hauathiri wao tu bali serikali na wananchi kwa ujumla.
Serikali inajitahidi kupata fedha za kulipa makandarasi, na kila mara fedha zinapopatikana, kipaumbele kinatolewa kwa madeni ya makandarasi wa ndani.
“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kuwasaidia makandarasi wa ndani ili waweze kukua na kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi nchini, na pia kushindana katika masoko ya kimataifa”amedai
Ulega amesema faida ya miradi ya ujenzi kubaki nchini, itachangia katika uchumi wa taifa letu na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kutoka miradi ya nje.
Msajili wa bodi, mhandisi Rhoben Nkori, amesema mkutano huu wa mashauriano ni jukwaa linalounganisha wadau wa sekta ya ujenzi kutoka serikalini na sekta binafsi, , ili kukutana kwa ajili ya kupeana taarifa, kushauriana, kujitathimini na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha ufanisi katika shughuli za ujenzi nchini.
Nkori amesema kauli mbiu ya mwaka huu, “Ni ukuaji wa makandarasi wa ndani fursa na changamoto’ imewekwa ili kusaidia kutathmini mazingira halisi yanayosaidia na yanayokwamisha juhudi za ukuaji wa ndani kwa manufaa ya nchi yetu.
Aliongeza kuwa mwaka jana 2024, bodi ilisajili makandarasi 1,812, hivyo kufanya idadi ya waliosajiliwa kufikia 13,596.

Aidha, bodi iliendesha kozi nane (8) za mafunzo kwa makandarasi ,kwa lengo la kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali, ambapo jumla ya makandarasi 971 walihudhuria mafunzo hayo.
Bodi ilirekodi miradi 4,691 yenye thamani ya shilingi za Kitanzania trilioni 10.472, ambapo asilimia 40.5 ya thamani ilitekelezwa na makandarasi wa ndani na asilimia 59.5 ilitekelezwa na makandarasi wa kigeni.
Nkori alieleza kuwa bodi ilikagua miradi 3,581, ambapo miradi 2,092 (58.4%) hazikupatikana na kasoro yoyote, wakati miradi 1,489 sawa na 41.6% zilipatikana na kasoro mbalimbali, hivyo maelekezo stahiki kutolewa kulingana na sheria.
“Katika mwaka 2024, bodi iliendelea kuimarisha mfuko wa kusaidia makandarasi (Contractors Assistance Funds – CAF), ambao una jumla ya bilioni 4.2 za Kitanzania na unasaidia makandarasi wa ndani kupitia benki ya CRDB ili waweze kupata dhamana za benki kwa ajili ya zabuni na malipo ya awali hata hivyo, mfuko huu hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya makandarasi”Amedai.
Amesema kwa sasa, viwango vya miradi vinavyotekelezwa na makandarasi wa ndani vimeongezeka kutoka shilingi bilioni 10 hadi bilioni 50.

Aidha, kwa miradi yenye thamani zaidi ya bilioni 50, makandarasi wa nje wanatakiwa kuingia ubia au kuwaajiri makandarasi wa ndani kila inapowezekana.
Nkori amedai masharti magumu ya ushindani kwenye zabuni yanawatoa makandarasi wa ndani, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya mauzo ya kila mwaka, dhamana za benki, uzoefu wa kazi zinazofanana, mitambo na fedha za kuendesha kazi utekelezaji wa masharti haya Serikali inaendelea kufanya mawasiliano na wadau mbalimbali ili kuchunguza uwezekano wa kuboresha upatikanaji wa mitaji.
Serikali inashirikiana na wahisani wa maendeleo ili kutathmini uwezekano wa kuhusisha wazawa, katika miradi mikubwa inayotekelezwa nchini bila kuathiri sheria.