Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameongoza watumishi wa wizara hiyo kuhamia na kuanza rasmi kazi katika jengo jipya la kisasa la Wizara hiyo lililopo eneo la Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Hatua hiyo inalenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwakutanisha na vitengo vyote vya wizara katika eneo moja, tofauti na awali ambapo huduma hizo zilikuwa zikitolewa katika maeneo tofauti tofauti hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Akizungumza leo Mei 15,2025 mara baada ya kuwasili katika eneo hilo, Waziri Mavunde amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini lililotaka wizara hiyo kuhamia katika Ofisi rasmi iliyopo Mji wa Serikali Mtumba.

“Nimehamia rasmi leo kwenye Ofisi za Wizara,hatua hii itasaidia huduma zote za wizara kupatikana katika eneo moja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwaweka karibu na huduma zote muhimu kwa wakati mmoja, ” amesema na kuongeza, ;

Nimekamilisha ahadi yangu ya kuhakikisha wizara hii inahamia rasmi hapa kama sehemu ya mageuzi ya kiutendaji, “amesisitiza Waziri huyo

Mavunde ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni matokeo ya usimamizi mzuri na mshikamano wa watumishi wa wizara hiyo huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha mradi huo wa thamani ya Shilingi bilioni 300 unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Amesema kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa namna Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassani ilivyojipanga kuboresha huduma kwa wananchi.

“Tunataka wananchi wapate huduma kwa urahisi bila kukimbizana kutoka ofisi moja hadi nyingine,kwa sasa, vitengo vyote muhimu vya wizara vinapatikana hapa Mtumba,hii ni hatua kubwa ya kuimarisha utendaji wetu,” amesema Mavunde.

Mbali na kuwahakikishia wananchi huduma bora, Waziri Mavunde ameeleza kuwa wafanyabiashara waliopo katika Sekta ya madini nao watanufaika na uboreshaji wa miundombinu hiyo.

Amesema mazingira bora ya kazi yanayopatikana kwenye Ofisi hiyo Mtumba yataongeza ufanisi katika utoaji wa leseni, usimamizi wa shughuli za uchimbaji na ufuatiliaji wa sekta kwa ujumla.

Hata hivyo, Waziri amebainisha kuwa taasisi ya Serikali ya Jiolojia Tanzania (GST) itaendelea kutoa huduma zake kwenye Ofisi za awali zilizopo jiji la Dodoma kwa sababu ya majukumu yake ya kitaalamu na uhitaji wa vifaa vya kiuchunguzi ambavyo haviwezi kuhamishwa kwa sasa.

Amesisitiza kuwa jambo hili halitapunguza ufanisi wa huduma za wizara kwa wananchi.

Licha ya hayo Waziri Mavunde amewataka watumishi wote wa Wizara ya Madini kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji katika kuhudumia wananchi, akisema kuwa jengo jipya ni fursa mpya ya kuonyesha mabadiliko katika utoaji wa huduma bora kwa taifa.