Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imeliagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na taasisi zote zinazosimamia miundombinu ya mawasiliano kuongeza kasi ya kuwaunganisha wananchi, taasisi za Serikali na sekta binafsi kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, alipotembelea Ofisi za TTCL na Shirika la Posta Tanzania kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma na maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano.
Waziri Kairuki amesema pamoja na Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, idadi ya wananchi wanaotumia huduma hiyo bado ni ndogo, jambo linalohitaji juhudi zaidi kutoka kwa watumishi wa TTCL na wadau wengine wa sekta hiyo.
“Kwa Mkoa mzima wa Dodoma hadi sasa ni watu 65 tu ndio wameunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa,tunataka Watanzania wote wanufaike na uchumi wa kidijitali, hivyo ni lazima kuongeza kasi ya kuwafikia wananchi, taasisi za Serikali na sekta binafsi,” amesema Kairuki.
Amesema matumizi ya Mkongo wa Taifa yatasaidia kupunguza gharama za mawasiliano, kuboresha huduma za Serikali mtandao, kuimarisha biashara za kidijitali pamoja na kuongeza ufanisi katika sekta za elimu, afya na uwekezaji.
Kauli hiyo inaenda sambamba na mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini, ambapo katika Mkoa wa Dodoma tayari minara 488 ya mawasiliano imesimikwa, zaidi ya wananchi 150,000 wamefikiwa na huduma bora za mawasiliano, huku kilomita 942.5 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zikikamilika.
Aidha, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuongeza upatikanaji wa mawasiliano, ikiwemo ujenzi wa minara 636 inayotarajiwa kukamilika Machi 2027 pamoja na mradi mwingine wa minara 280 utakaopanua zaidi wigo wa huduma nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa TTCL Mkoa wa Dodoma, Simon Marwa, amesema hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi huo ilikuwa kuunganisha ofisi za Serikali na taasisi za umma, huku hatua inayofuata ikielekezwa kwa wananchi mmoja mmoja pamoja na kaya ili kuongeza matumizi ya Mkongo wa Taifa.
Nao baadhi ya wananchi wa Mpwapwa wameeleza kuwa maboresho ya huduma za mawasiliano yameanza kuleta matokeo chanya, hasa katika matumizi ya intaneti na huduma za kidijitali, wakisema maendeleo hayo yataongeza fursa za biashara, uwekezaji na kuboresha sekta ya elimu kutokana na wilaya hiyo kuwa na taasisi nyingi za elimu.
Japhet Rafael amesema ,”Kwa sasa tunatumia mtandao vizuri Kwa kufanya Biashara mtandao na kuwasikiana na ndugu zetu ni jambo zuri sana na tunaipongeza Serikali Kwa huduma hii muhimu Kwa jamii,”amesema
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki pia alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, miundombinu ya TEHAMA na huduma za mawasiliano, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa sawa za kushiriki katika uchumi wa kidijitali.



