Na Mawamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Timu ya Maafa ya Wilaya ya Mafia imewaokoa manusura 22, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Visiwa vya Comoro, walionusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Comoro kuelekea Kisiwa cha Mayotte kupata hitilafu ikiwa baharini.

Akizungumza Julai 24, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisema manusura hao waliokolewa Julai 22, 2026 katika fukwe za Kijiji cha Kungwi, Kata ya Baleni, baada ya boti yenye ukubwa wa H40 na injini aina ya Yamaha, isiyokuwa na usajili, kushindwa kuendelea na safari kutokana na hitilafu ya kiufundi.

Alisema boti hiyo iliondoka Comoro ikiwa na abiria 36, ambapo 14 kati yao walifariki dunia njiani baada ya chombo hicho kupata hitilafu, huku manusura 22 wakiokolewa na kupelekwa kupata huduma za dharura.

Mangosongo alieleza kuwa raia hao walikuwa wakielekea Kisiwa cha Mayotte wakitarajia baadaye kuingia nchini Ufaransa, wakikimbia migogoro katika nchi zao pamoja na kutafuta fursa bora za maisha barani Ulaya.

Alieleza, uongozi wa Wilaya ya Mafia, kwa kushirikiana na Timu ya Maafa ya Wilaya na wadau mbalimbali, umewapatia manusura hao msaada wa chakula, nguo na mahitaji mengine muhimu.

Manusura hao ni wanaume tisa, wanawake wanane na watoto watano, wakiwemo wavulana watatu na wasichana wawili, ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilindoni.

Mkuu huyo wa Wilaya aliishukuru Serikali ya Kijiji cha Kungwi kwa kutoa taarifa kwa wakati, pamoja na timu za afya, Timu ya Maafa ya Wilaya na wananchi kwa ushirikiano wao uliofanikisha uokoaji na utoaji wa huduma muhimu kwa manusura hao.

Vilevile, Mangosongo aliwataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za usafiri wanaposafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine na kujihusisha na shughuli halali za kujipatia kipato ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na safari zisizo salama.