Marekani imeendelea kuishambulia Iran huku waasi wa Houthi nchini Yemen wakijiingiza katika vita hivyo kwa kuzishambulia meli za mafuta za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, ambazo wanasema zilikiuka kizuizi cha majini
Iran na Marekani zimetishiana hapo jana kuongeza mashambulizi dhidi ya kila mmoja, baada ya washirika wa Tehran wa kundi la Wahouthi kushambulia meli za kibiashara za Saudi Arabia na kusababisha bei za mafuta kupanda kwa kasi.
Masoko ya hisa yameyumba huku bei za mafuta zikivuka dola 100 kwa pipa, baada ya waasi wa Kihouthi kuzilenga meli katika Bahari ya Shamu pamoja na vitisho vya Rais Donald Trump vya kulipiza kisasi kwa kuwashambulia Wahouthi.
Rais Trump alisema kwamba Marekani itaichukulia Iran kuwa inawajibika kwa vitendo vya Wahouthi, na akaonya kwamba Tehran pamoja na Wahouthi wataadhibiwa vikali kijeshi hivi karibuni. Aidha pia Rais Trump alisema Washington itaanza kutumia mali za Iran zilizofungiwa ili kulipia meli na shehena zilizoharibiwa na mashambulizi karibu na eneo la Ghuba.
Wakati huo huo, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, alionya kuhusu “madhara makubwa” kwa uchumi wa nchi zinazotegemea uagizaji wa mafuta kutoka nje. Alisema kuwa “hakuna dalili ya wazi kwamba usitishaji wa mapigano unaweza kufikiwa.” Pistorius alisema hali ya Mashariki ya Kati inaendelea kuzorota na kwamba mwelekeo wake kwa sasa si wa kutia matumaini.



