Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MMKURUGENZI wa Manispaa ya Mji Kibaha, Mkoani Pwani Dkt. Rogers Shemwelekwa, amewasihi wafanyabiashara wa Soko la Mnarani Loliondo kuendeleza biashara zao kwa amani, utulivu na mshikamano, akisema ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yao.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika viwanjani hapo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara, Dkt. Shemwelekwa alieleza serikali imehakikisha mazingira ya nchi yako salama kupitia uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, hivyo hakuna sababu ya mtu yeyote kuwa na hofu katika kufanyabiashara.

“Tutunze amani, endeleeni kufanya biashara bila wasiwasi, Amani ni uchumi, na uchumi ni maendeleo yenu na ya Taifa,” alisisitiza Dkt Shemwelekwa.

Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini na kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapoona wageni au watu wanaotiliwa shaka, akibainisha kuwa zipo nguvu zinazotaka kuivuruga amani ya nchi, hivyo umoja na ulinzi wa jamii ni muhimu.

Vilevile Dkt. Shemwelekwa aliwahimiza wafanyabiashara kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Alisema fedha zipo na zinapatikana kwa vikundi kuanzia watu watano.

Aliongeza kuwa Halmashauri itapeleka Ofisa Maendeleo na Ofisa Biashara katika soko hilo ili kutoa usaidizi wa moja kwa moja katika mchakato wa uundaji na usajili wa vikundi.

“Mikopo hii haina riba, jiungeni kwenye vikundi ili mnufaike na fursa hizi za kuinua kipato chenu,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Wafanyabiashara wa Soko la Mnarani Loliondo akiwemo Amina Swedi anaeuza mbogamboga walieleza kuridhishwa na jitihada za serikali zenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara, ikiwemo ujenzi wa soko jipya la kisasa unaoendelea.

“Tunashukuru kwa kutusikiliza na kutatua changamoto zetu, tuko pamoja na tunaendelea kushukuru,” alisema Amina.

Alifafanua ziara hiyo ni kichocheo cha kuimarisha uhusiano kati ya Halmashauri na wafanyabiashara na kuongeza hamasa ya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa ya Mji Kibaha.