Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kwa miaka kadhaa nimeandika mengi kuhusu uhifadhi, hasa eneo la Ngorongoro ambako kuna Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), na Pori la Akiba Pololeti (Loliondo).

Mambo yanayoendelea katika eneo hili yanahitaji watu wenye roho ngumu wayaseme wazi wazi, pia yanahitaji ujasiri kutoka kwenye mamlaka za nchi na wananchi ili ufumbuzi wa kudumu upatikane.

Bahati mbaya suala la Ngorongoro linageuzwa na kuwaaminisha watu kuwa kuna utesaji, unyanyasaji watu, uhamishaji raia kwa nguvu – na kwamba wote wanaosimama kuomba Ngorongoro isife wanaonekana wanathamini wanyamapori kuliko binadamu.

Mwaka 2021 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwaapisha mawaziri, aligusia Ngorongoro. Nakumbuka alisema tuamue moja – Ngorongoro tunailinda, au tunaiacha ife. Baada ya hapo tukatangaziwa mpango wa wananchi kuhama kwa hiari kwenda Msomera na maeneo mengine nchini. Uamuzi huu ukajumuishwa na ule wa kuligawa Pori Tengefu la Loliondo, hivyo kuzaliwa kwa Pori la Akiba Pololeti. Huu ni miongoni mwa uamuzi wa kishujaa mno uliofanywa na Rais Samia.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa ndani na nje ya nchi, na hata kwa kutumia macho ya kibinadamu, ni wazi kuwa bila hatua madhubuti kuchukuliwa [kupunguza watu, mifugo na shughuli za kibinadamu], Ngorongoro haina miaka 10 mbele.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ‘Kupanga ni Kuchagu’. Je, tumechagua Ngorongoro ife? Tuiache imalizwe na wenye tamaa ya kujaza mifugo yao humo? Kama sivyo, tufanye nini tuendelee kuona ikiwafaidisha wengi miaka mamia mbele?

Kwa miaka miwili wananchi kadhaa wameitika wito wa kuhama kwa hiari, lakini ndani ya mafanikio haya akajitokeza Waziri wa Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa akavuruga hali ya hewa kwa amri yake ya kufuta vijiji. Jambo kubwa kama hili haliwezi kukosa baraka za Baraza la Mawaziri. Kama kweli liliridhiwa kwenye ngazi hiyo, basi mawaziri hawakufanya kazi yao.

Tangazo la waziri kufuta vijiji likafuta ile dhana ya uhamaji wa hiari! Likazua malalamiko mengi na kupata watetezi wa ndani na nje ya nchi. Mwishowe tukamsikia Rais akiingilia kati, akatengua amri ya waziri ambayo bila shaka ni amri ya Baraza la Mawaziri.

Rais Samia asingefikia hatua hii kama mifumo yetu ya uongozi ingekuwa inasomana. Kama mifumo ingesomana, hasa kwa kuwashirikisha NCA na wadau wengine, yote haya yasingetokea. Naamini kama waziri angewashirikisha wenzake kwenye uamuzi huu, bila shaka angeambiwa kitendo cha kufuta vijiji wakati huu ambao wananchi wanaondoka kwa hiari kingeleta zogo kubwa kwa jamii ya Ngorongoro na wachochezi wa huu moto wangekuwa Wakenya na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoweka kambi Kenya.

Rais Samia alichofanya ni kuepusha shari tu, lakini kwa kumsikia na kumtazama usoni, sidhani kama amenuia kweli kuona Ngorongoro ikimfia mikononi.

Sidhani kama uamuzi wake unalenga kuiacha Ngorongoro ife. Ngorongoro haipaswi kuachwa ife. Kama wapo wanaodhani Ngorongoro ikifa tutabaki na Serengeti, wanajidanganya! Manufaa ya Ngorongoro yamevuka mipaka yake, mipaka ya nchi na mipaka ya Afrika.

Kuna kauli dhaifu kwamba kulinda viumbe hawa walio Ngorongoro na kwingineko hifadhini maana yake ni kuwathamini wanyamapori kuliko binadamu.

Maandiko Matakatifu ya dini zote yameeleza bayana jinsi Mwenyezi Mungu alivyoumba ulimwengu na viumbe hai. Yaliyoandikwa kwenye vitabu hivyo ni ya manufaa kwa wanaoamini, pia kwao wasioamini uwepo wa Mwenyezi Mungu.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 55 (Surat Ar-Rahmaan), Aya ya 10, Mwenyezi Mungu anasema: “Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe.”

Maana ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiweka ardhi kwa matumizi ya viumbe wote wakiwamo wanadamu, wanyama, ndege, wadudu wa aina mbalimbali na viumbe wengine.

Katika Biblia Takatifu, Kitabu cha Mwanzo 1:24-28 tunasoma haya kuhusu uumbaji:
24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.

25 Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.

Kwa ufupi, maandiko haya yanathibitisha dhamira ya Mwenyezi Mungu katika kuhakikisha wanadamu wanatawala viumbe hawa kwa manufaa yao. Haya ni maua katika bustani hii ya Mungu (ulimwengu). Mungu ameviumba hivi vitu ili mwanadamu avitawale, si aviangamize.

Bahati mbaya tupo tunaokosa ujasiri kueleza bayana hatari kubwa inayoikabili Ngorongoro na maeneo mengine ya uhifadhi. Wanaojitokeza kutetea ustawi wa eneo hili wanaonekana watu wabaya, wasiowapenda wakazi wa eneo hilo, au watu waliotumwa kufanya kazi hiyo kwa malipo.

Hawa watalii tunaowaona Ngorongoro, Serengeti na kwingineko wanakuja kufaidi urithi huu wa wanyamapori. Takwimu za watalii zinathibitisha kuwa wengi wanakuja kuona wanyamapori maana kama ni suala la mabonde na milima, hata huko kwao vipo.

Ujio wa watalii hawa tafsiri yake ni kuwa haya ni matokeo ya dhambi iliyofanywa na mababu na mabibi zao ya kupuuza kuwalinda wanyamapori na misitu katika mataifa yao, hata wakaacha viteketee. Wanalipa fedha nyingi kuja kuangalia maajabu na utamu vilivyofutwa na watangulizi wao. Wanabebeshwa mzigo wa makosa na dhambi zilizofanywa na watangulizi wao.

Haishangazi leo kuona baadhi yao wakisimama kwa uchungu kupinga utalii wa uwindaji wakiamini kuwaua wanyamapori hawa kutaibua hatari ya kuwafanya watoweke kama ilivyotokea kwao.

Katika hili tunawataka wajue kuwa uwindaji wa kitalii ni uhifadhi na ndiyo maana Kenya ambao walizuia uwindaji tangu miaka ya 1970 tofauti na Tanzania, idadi ya wanyamapori kwao imepungua mno.

Kunapotokea ukinzani wowote wa baadhi ya raia wenzetu wakashirikiana na wageni kutaka urithi huu wa asili utoweke, wapenda uhifadhi hawana budi kujitokeza kulaani hali hiyo.

Wale ndugu zetu wafugaji waliojitokeza kwa wingi kutaka waendelee kuishi ndani ya Ngorongoro kwa kigezo kuwa ni ardhi yao ya asili, hawana maelezo ya kisayansi kuhalalisha misimamo yao.

Tunakosea sana kudhani kuwa Ngorongoro wanatetewa wanyamapori na viumbe wengine tu. Tunasahau au kupuuza ukweli kwamba ikolojia ya Ngorongoro inachangia sehemu kubwa sana ya maji, kilimo na hali ya hewa nzuri kwa maeneo ya karibu na hata yale ya mbali.

Kiikolojia, NCA ni eneo muhimu la kuzalia nyumbu na ni kituo cha kupumzika kwa ndege wahamiaji wanaosafiri kati ya Ulaya/Asia na sehemu za kusini mwa Afrika.

Pia, NCA inajulikana kama kitovu cha asili ya binadamu na inasifika kwa kuwa na kaldera kubwa zaidi duniani. Aina za matumizi ya ardhi na shughuli zinazofanyika nje ya mipaka zina athari (chanya au hasi) kwenye ikolojia na usimamizi wa NCA. Ngorongoro ni sehemu ya Urithi wa Dunia, na kuharibiwa kwake kutamaanisha hasara kwa urithi wa binadamu.

Kuilinda Ngorongoro na rasilimali nyingine za nchi hii si suala la hisani, bali ni agizo la kikatiba. Kwa hiyo tunapotetea uwepo wake maana yake tunatetea Katiba yetu isivunje.

Ulinzi wa rasilimali za asili unasisitizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Kwa mujibu wa Ibara ya 27 (1) na (2) ya Katiba:
i. Kila mtu ana jukumu la kulinda rasilimali za asili za Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi, mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuheshimu mali ya mtu mwingine; na
ii. Sheria inawataka watu wote kulinda mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, kupambana na aina zote za ubadhirifu na matumizi mabaya, na kusimamia uchumi wa taifa kwa uadilifu kwa mtazamo wa watu ambao ni mabwana wa hatima ya taifa lao.
Aidha, Ibara ya 26 inasema kuwa: “Kila mtu ana jukumu la kuheshimu na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano.”

Kwa kutambua kuwa Tanzania ina rasilimali zenye tija kubwa kwa ulimwengu, imesaini mikataba na makubaliano ya kimataifa.

Tumeridhia mikataba kadhaa ya kimataifa kuhusu rasilimali za asili na utamaduni, utalii, mazingira na haki za ustawi wa binadamu. Mikataba hii imesainiwa na/au kuridhiwa kati ya Tanzania na nchi nyingine binafsi, na kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), UNESCO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN-WTO), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Shirika la Afya Duniani (WHO), na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

Suala la Ngorongoro limehamishwa kwenye uhifadhi na kufanywa kuwa ni ajenda ya kulibana kabila moja. Ngorongoro kuna makabila mengi, lakini hauwezi kusikia yakitajwa. Hata hao Wasonjo wanaoelezewa kila leo hawana mtetezi.

HALI YA NGORONGORO

Mwaka 1959 idadi ya watu Ngorongoro ilikuwa 8,000, ng’ombe walikuwa 161,034, na mifugo midogo ilikuwa 100,689. Wakati huo, athari kwa mfumo wa ikolojia zilikuwa ndogo.

Taarifa ya mwaka 2017 inaonyesha kuwapo ongezeko kubwa la idadi ya watu hadi 93,136, ng’ombe (238,826), na mifugo mingine 570,633.

Hali hii imesababisha matumizi yasiyostahimilika ya rasilimali asilia na imesababisha matumizi makubwa kupita kiasi yanayodhuru huduma za ikolojia.

Hali ya maisha ya binadamu na mazingira NCA inazidi kudorora, hivyo kudhoofisha ustawi wa jamii na uimara wa eneo hili.

Viashiria vya kudorora kwa hali ya maisha ya binadamu katika eneo hilo ni pamoja na umaskini (asilimia 50%), njaa (asilimia 70%), ujinga (asilimia 64%), na magonjwa. Hizi ni takwimu za NBS za mwaka 2017.

Katika sensa ya hivi karibuni ya watu na mifugo (NBS 2017), ilibainika kwamba kati ya kaya 20,890 za NCA, kaya 4,596 (asilimia 22) hazikuwa na mifugo, hali inayopendekeza kwamba kaya hizi zimepoteza sifa ya kuishi katika NCA kama wachungaji kulingana na Sheria ya NCA 284 (R.E. 2002). Hawa ndio wale wanaotakiwa wahamie Msomera kwa hiari.

Hadi mwaka 2017, kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kwa umri wa miaka mitano na kuendelea kilikuwa kimepungua hadi asilimia 64.2 (NBS, 2017). Kiwango cha elimu kwa wanaume kilikuwa asilimia 44.4 ikilinganishwa na asilimia 27.8 kwa wanawake. Hii ina maana kwamba asilimia 72.2 ya wanawake walikuwa wasiojua kusoma na kuandika mwaka 2017.

MWALIMU NYERERE

Septemba, 1961 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka maneno maarufu ambayo kwa miaka mingi kabla ya sheria mpya za uhifadhi, ndiyo yaliyokuwa, na yanaendelea kuwa dira ya kulinda rasilimali wanyamapori na misitu.

Maneno hayo hadi leo yanatumiwa na wenye dhamama ya kulinda maliasili ya wanyamapori kama mwongozo na hamasa kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na viumbe wengine.

Mwalimu Nyerere alisema: “Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.

Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.

Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri siyo tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”
Kwa miaka yote NCAA imeendelea kuutumia mwongozo huu kama dira ya utendaji kazi wake.

Sheria iliyoanzisha NCAA mwaka 1959 imekipa chombo hicho dhima kuu tatu: Mosi, kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na malikale. Pili, kuendeleza wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi, na Tatu, kuendeleza utalii. Ni wazi kuwa mfumo uliowekwa mwaka 1959 kwa ajili ya NCA, umefeli.

Mwalimu Nyerere hakuchoka kuelezea umuhimu wa kulinda rasilimali hizi. Akizungumza na viongozi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na watumishi wa serikali mkoani Kilimanjaro; Agosti 10, 1975 Mwalimu alieleza mambo yanayowagharimu watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani baada ya kuua wanyamapori na kuharibu misitu. Hapa tutambue kuwa miaka mia kadhaa iliyopita, Ulaya na Marekani walikuwa na wanyamapori wengi, lakini uharibifu wa kibinadamu umewafuta kwenye uso wa dunia.

Mwalimu alisema: “Ni vizuri kujifunza kwa wenzetu waliotangulia. Na wakati mwingine ni kujifunza kutokana na makosa yao. Wenzetu waliotangulia tunaowasema zaidi ni wale wa nchi zilizoendelea sana hasa za Ulaya na Amerika Kaskazini.

“Wamefanya makosa mawili makubwa – wao wanajua, sisi hatujui. Wao wanajua kwa sababu wameyafanya makosa hayo, sisi kwa sababu hatukuyafanya hatujui kwamba ni makosa. Moja, mtashangaa nikilitamka – wameharibu sana nchi zao kwa kitu wanachokiita maendeleo. Wameua vi-nyama vingi sana vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu – vingi. Wameua vyote. Hawana tena makundi makubwa makubwa ya wanyama kama tuliyonayo katika Afrika na hasa katika Tanzania. Hawana kabisa.

“Sasa wao wanajua kwamba wamefanya makosa, na wanakuja huku wanatwambia; ‘Sisi tumefanya makosa, tumeua wanyama wetu wote tumemaliza, tafadhalini msiue wanyama wenu.’ Sisi tunawaona kama wajiiinga wanapotuambia hivyo. Lakini wao wanajua kosa kubwa la kufuta wanyama na kuwamaliza; na kukatakata misitu yao na kuimaliza. Wanajua kosa walilolifanya na wanatuomba tusilifanye kosa hilo.

“Sasa wanakuja kwa wingi, ndio hao mnawaita watalii. Wanakuja kwa wingi kuja kuona wanyama. Wewe unamshangaa huyu mtu mzima anatoka kwao mbaaaaali kuja…anatoka kwao mbaaaali, analipa hela kuja kuona tembo, kwa nini? Ana akili, hana akili! Ni kwa sababu ana akili ndiyo maana anatoka kwao mbaaali sana, analipa fedha anakuja kuona tembo. Angekuwa hana akili asingekuja. Anajua faida ya kuwa na ma-tembo, na ma-simba, na ma-nyati, na ma-chui, na ma-pundamilia katika nchi hii, lakini kwao wameshafuta.

Sasa wanaanza kutuomba, wengine wanaanza kutuomba tuwauzie-uzie angalau wafufue-fufue, lakini kufufua si jambo jepesi. Ukishaifuta misitu, kuifufua na kuweka wanyama waishi kama walivyokuwa zamani ni vigumu sana, kwanza hali yake ile ni tofauti. Huwezi kuifufua, vigumu sana. Wala hawajui ilikuwaje hata waweze kuifufua. Sasa nasema wanatushawishi – Wazungu wanatushawishi katika jambo hilo ambalo hatujafanya kosa, tusifanye kosa.

“Serikali ya Tanzania imekubali, nadhani wananchi wanaanza kukubali kutofanya kosa hilo lililofanywa na wenzetu. Tuhifadhi wanyama wetu na tuhifadhi misitu yetu. Tusivuruge vuruge mazingira ambayo tumeyarithi, na kwa kweli hatujui yamechukua muda gani hata yakawa hivyo; halafu tunafika sisi tunaita maendeleo tunavuruga vuruga, tunaharibu; tunaua wanyama, tunakata miti. Matokeo yake hatuwezi kuyajua.” Mwisho wa kunukuu.

Maneno haya yanapaswa yawe mwongozo wa kulinda rasilimali hii ya wanyamapori, misitu na viumbe wengine.
Makala zitakazofuata nitaeleza kwa kina nani wanaonufaika na Ngorongoro, na kwa nini wako tayari kuona ikitoweka, alimradi tu wao waaendelee kufaidika.

Katika hili serikali inachopaswa kufanya, na kama ilivyokwishaanza kutenda, ni kusimamia haki za raia. Mpango wa wananchi kuhama Ngorongoro kwa hiari hauna budi uendelee. Wananchi watendewe haki.
Lakini kwa hili la juzi la kufutwa kwa amri ya kuondoa vijiji, serikali ijue imejipalia makaa. Zipo taarifa za vikao vinavyoendelea kwenye vijiji fulani ndani ya Ngorongoro vya wananchi kujipanga kwenda ‘kuikomboa’ Pololeti ambayo sasa ni Pori la Akiba. Wanasema kama imewezekana NCA, wanaamini nguvu hizo hizo zitafaa kuirejesha Pololeti.

Makala zitakazofuata nitaeleza nani walio nyuma ya sekeseke la Ngorongoro na wanafaidi nini.

0759 488 95

ITAENDELEA…

Please follow and like us:
Pin Share