Pamoja na hatua zilizofikiwa kukuza demokrasia chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, bado ziko changamoto zinazoathiri hali ya kukua na kushamiri kwa demokrasia nchini. Ile tafsiri asilia ya demokrasia inasema hivi:
Serikali inayoongozwa na watu. Aidha ni aina ile ya serikali ambayo hatamu juu yake imo mikononi mwa watu, na uwezo huo unatekelezwa au moja kwa moja nao wenyewe au na viongozi waliochaguliwa nao. Kwa tafsiri ya sasa ni taifa la jamii ambapo kila mtu ana haki sawa na mwingine.
Tunapenda kuamini kuwa, kinadharia, na ndani ya utaratibu uliowekwa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992, chombo chochote cha kisiasa kinaweza kusambaza ujumbe ambao itaona unapaswa kufahamika na Watanzania.


Hata hivyo, baadhi ya sheria zilizopo, kama Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu, zinapunguza uwezo huu wa kufikisha taarifa mbalimbali kwa Watanzania na hata kwa Watanzania wenyewe kupeana taarifa baina yao.
Unapoachiwa kufanya kazi kama ulivyokusudiwa mfumo huu wa demokrasia una manufaa makubwa. Miongoni mwa faida zake ni kulinda uwezekano wa hoja za pande zote za uwanda wote wa siasa kuwafikia wapigakura ili kuwaruhusu wajenge ufahamu mkubwa wa masuala mbalimbali yanayohusu jamii na inapofikia kupiga kura kuwawezesha kuchagua mgombea ambaye sera za chama chake zitakidhi matakwa yao.


Bila shaka zipo nchi nyingi duniani ambako mfumo huu wa kidemokrasia unaendeshwa kwa ufanisi, lakini uzoefu unadhihirisha pia kuwa hata pale ambako mfumo unajiendesha vizuri bado huweza kutokea matatizo yasiyotarajiwa yatakayoathiri ufanisi huo. Hata bila changamoto hizi za hivi karibuni za kisheria, zipo changamoto za kitamaduni ambazo zinakwaza mfumo wa kidemokrasia.


Miaka mingi iliyopita nilipata fursa ya kuzungumza na mwanaharakati mmoja kutoka Tarime, mwanajeshi mstaafu aliyeamua kuwa mwanasiasa wa mojawapo wa vyama vya upinzani, mtu mwenye uwezo mkubwa wa kutema ujumbe mkali wa kisiasa mithili ya cheche za moto. Alinieleza kuhusu mengi yaliyo mazuri yanayohusu chama chake, na akataja mlolongo wa maovu aliyoyahusisha na Chama Cha Mapinduzi na serikali yake.


Alifafanua kuwa upo uwezekano wa chama kingine cha siasa kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani, lakini alikiri kuwa ni suala litakalochukuwa muda mrefu, tena muda mrefu sana.
Aliendelea kusema kuwa unapotamka kifupi cha Civic United Front, yaani CUF, kwa mojawapo ya lahaja 11 za lugha ya Kikurya, matamshi hayo yanafanana na neno linalomaanisha mchwa kwa Kikurya. Natambua kuwa ukali wa mchwa unaweza kuwa sifa nzuri ya kufananishwa na chama cha siasa, hususani ambacho ni cha upinzani, lakini yule mwanajeshi mstaafu aliona kuwa mkanganyiko huo unaweza kudhoofisha upinzani. Alibainisha ugumu wa kuanza kuelimisha wazee kuhusu tofauti ya CUF na ya mchwa. Na hiyo itakuwa ni hatua ya awali tu. Baada ya hapo ianze kazi ya kuwaeleza wazee kuwa kiongozi anaweza kuondolewa madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na kiongozi mwingine. Kwa asili ya mila za makabila mengi watu hupitia hatua kadhaa za maisha ndani ya rika katika jamii zao wakianzia ngazi ya chini kabisa ya utoto mpaka ngazi ya juu ya uzee.


Waliyo katika hizi rika mbalimbali wanakuwa na dhima zinazoambatana na umri na uwezo wao ndani ya jamii. Kwa kabila la Wazanaki kundi la wazee ni sehemu ya mfumo wa uongozi na si rahisi kupingana na uamuzi wao bila kuonekana unatafuta laana. Wazee wanaaminika kuwa na busara na uzoefu ambao wale wa rika za chini yao hawana.
Wanatambuliwa na jamii kuwa siyo kundi la kufanya makosa, lakini iwapo watafanya hivyo, basi ni wazee wenzao tu ndiyo wanaweza kuwachukulia hatua. Siyo mtu yoyote ambaye mradi tu amefikia umri wa kupiga kura ataruhusiwa kuwakosoa. Kwa jamii hizi kusikilizwa na kila mtu bila kupingwa kunahitaji subira. Kijana wa miaka 21 hana sauti mbele ya mzee wa miaka 65.


Baadhi ya misingi ya kidemokrasia ambayo tunaitumia kwa sasa inakinzana na tamaduni za mababu zetu, kwa sababu kazi ya msingi ya vyama vya upinzani ni kukosoa sera na usimamizi wa sera wa serikali. Ukiangalia mifano ile ya uongozi wa asili ambako wazee walipitisha uamuzi unaogusa maisha ya jamii zao, serikali inachukuwa nafasi ile ya hawa wazee. Tamaduni zetu zinaendelea kufifia kwa sababu kila miaka inavyozidi kupita wanaendelea kuzaliwa Watanzania wanaofahamu zaidi mfumo huu wa vyama vingi kuliko ule wa kusikiliza kauli moja tu. Lakini pamoja na kuwapo haya mabadiliko, bado sauti zile za zamani zinasikika. Nakumbuka kauli ya baba yangu mdogo ambaye mara kwa mara anatukumbusha umuhimu wa nafasi ya wazee ndani ya jamii.


Enzi zake viongozi hawakubadilishwa; walikuwa watawala kama baba yake, na walifia madarakani. Enzi za mfumo wa chama kimoja cha siasa mzee mmoja aliambiwa aende kumpigia kura rais, lakini hakuelewa sababu ya kufanya hivyo. Aliuliza: “Kwani yule anayetuongoza wakati wote ameenda wapi? Amekufa? Si tulishamchagua huyo, kuna haja gani ya kupiga kura tena?”


Mwaka 2005 Rais Benjamin Mkapa, kwenye hotuba yake kwenye Bunge la Uganda, alitoa hoja kuwa wakati ulikuwa umefika kwa Waafrika kuunda mfumo wa kidemokrasia unaoakisi jamii ya Kiafrika.
Alisema: “Ukoloni ulitufanya kutojithamini. Mifumo ya kisiasa na kiutawala barani Afrika ilionekana duni kulinganishwa na ile ya kikoloni. Lakini tumetafakari vyema iwapo mifumo na taasisi hizi zinaendana na mazingira na vipaumbele vyetu?”
Tukitafakari hoja hiyo tukumbuke pia kuwa wale vijana waliopata uelewa wa kisiasa chini ya mfumo wa vyama vingi wanazidi kuongezeka na bila shaka wanashikilia msimamo unaopingana na rika zilizowatangulia.

 

By Jamhuri