Siku hizi kunasikika neno mabadiliko. Kila upande watu wanalilia mabadiliko, kila kukicha kunasikika neno mabadiliko. Wazee tumeanza kujiuliza kwani neno mabadiliko limeletwa na chama cha siasa, au ni kilio cha wananchi wote tangu zamani? Kwanini limeibuka katika uchaguzi huu?

Kwa mujibu wa historia ya nchi yetu hii, sisi wazee tuliokuwa tunasoma Tabora hapo zamani enzi zile Standard XII (Darasa la 12) ndilo ulikuwa ukomo wa elimu ya sekondari hapa Tanganyika, neno mabadiliko si geni katika masikio yetu. 

Niwarudishe wasomaji wangu huko nyuma kabla ya Uhuru wa Taifa letu. 

Nilisoma gazeti la wakoloni likiitwa THE EAST AFRICA and RHODESIA (a London Journal) toleo la Desemba, 1961 liliandika hivi “The change of Independence” yaani “Badiliko la Uhuru”. Sentensi yake ya kwanza ukurasa wa kwanza wa gazeti lile ilikuwa na utangulizi huu na ninanukuu “Tanganyika will become a free, united democratic country on December 9”.

Likaendelea: Free from colonial domination, united behind TANU and democratic in its government and its way of life” – maana yake kwa tafsiri yangu –  Tanganyika itakuwa huru, ya kuunganika na ya kidemokrasia Desemba 9. Huru kwa maana ya kutoka mikononi mwa utawala wa kikoloni, kuunganika nyuma ya chama cha TANU na yenye utawala wa kidemokrasia na mfumo wake wa maisha. 

Hapo lilipatikana wazo la neno hilo la “badiliko” kwa mara ya kwanza katika nchi hii. Ni badiliko kutoka kutawaliwa na kuingia katika hali ya kujitawala wananchi wenyewe. Yaani kujiamulia mambo yao wenyewe katika nchi yao. 

Badiliko hili sote katika nchi ya Tanganyika tulilihitaji. Ni badiliko la kujikomboa kutoka mikoani mwa ukandamizwaji na kujiweka huru kifikra na kiutendaji katika nchi yetu. 

Lakini dhana ya demokrasia kwa asili yake ni dhana ya pande tofauti zenye mawazo na mitazamo ya sera tofauti. Basi hapo inaingia hiyo dhana ya kuwapo na upinzani ili kutoa sera mbadala katika utawala wa kidemokrasia. 

Kukawa na vyama vya upinzani dhaifu wakati ule na vikafa vifo kwa utapiamlo. Kukabaki lile wazo lililotamkwa katika THE EAST AFRICA AND RHODESIA Journal la kuwa Tanganyika iliyounganika chini ya chama tawala cha TANU (united behind TANU). Hapo sasa Serikali ya chama kimoja ikawa inatawala. 

Kuanzia uchaguzi wa mwaka 1965 mpaka ule uchaguzi wa mwaka 1990 tulitumia dhana ya chama kimoja. Wananchi wakajiona, ipo haja ya kutawaliwa kidemokrasia sawa sawa, maana yake pawepo na vyama vingine vya siasa vyenye sera tofauti na hii ya ukiritimba wa chama na wimbo ule ule tulizoea wa “Eeee TANU yajenga nchi” na sasa “Chama chetu cha Mapinduzi chajenga nchi”. 

Jamani, nchi haijajengeka tu miaka yote hii? Chama kitaendelea kujenga nchi hii kwa miaka mingapi? Milele na milele? Wananchi wakasema hapana! Tunataka mabadiliko endelevu katika demokrasia. Hii maana yake nini? Maana yake kuwepo na vyama vingi vya siasa vyenye sera za milengo tofauti ili wananchi wachague watawaliwe na sera gani. 

Pili penye mawazo mengi bila shaka pana mambo mapya pia. Mtu kula kila siku ugali na kauzu au wali kwa samaki wa kupakwa utakuja kinai, basi hitaji la mabadiliko ni huko kuondoa ukinai na kufanya kila kitu kimazoea tu kama walivyofanya mababu zetu, baba zetu mpaka sasa sisi watoto. Ni mtindo wa kufanya kazi kimazoea. 

Serikali ikaliona hilo ndipo mwaka 1992 nchi yetu ikaingia kwenye mfumo wa utawala wa vyama vingi. Vikafumuka vyama vya siasa kama vile uyoga uotavyo katika ardhi yenye mboji. Tukawa na vyama chungu mzima.

Basi ulipofika uchaguzi wa mwaka 1995 vyama vipatavyo 13 vilijisajili na kutoa wagombea katika uchaguzi wa ubunge katika majimbo na vyama vinne katika hivyo 13 vilidiriki kutoa wagombea urais katika nchi hii. Naam, sote tulijisikia vema kuona mabadiliko katika mfumo wetu wa utawala. 

Katika viti 232 vya majimbo, chama tawala kiliibuka na ushindi wa viti 180 hivyo vyama vya upinzani vilifanikiwa kupata viti 46. Mpaka hapo tumeshapata mabadiliko kwa mara ya pili katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.

 

Mwaka 2010 tukawa na Uchaguzi Mkuu tena wa vyama vingi. Sasa tetesi za sauti ya kutaka mabadiliko zilianza kusikika. Mwaka huo vilikuwapo viti 239 vya majimbo na vyama vipatavyo 12 katika Taifa letu vilijitokeza kumwaga sera zao kuomba ridhaa ya wananchii kutawala Tanzania.

Nakumbuka vyama kama CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, Tanzania Democratic Alliance, Tanzania Labour Party, Sauti ya Umma, National Reconstruction Alliance, Association for Farmers Party, Democrasia Makini, Democratic Party, Jahazi Asilia na vingine nimevisahau vilitumia haki yao ya demokrasia kutafuta ridhaa ya wananchi kutawala Tanzania. 

Matokeo bado tunayakumbuka – CCM waliibuka na viti 186 wakati upinzani walipata viti 53 kutoka majimbo ya uchaguzi. Mimi siongelei wabunge wale wa vile viti maalum, la hasha, hapa naongelea waliojinadi kwa sera za vyama vyao tu. Hivyo idadi ya wabunge na rais niwaongeleao ni wale wa kuchaguliwa kidemokrasia, kwa sauti ya watu (popular vote). Hayo mimi nayaita ni mabadiliko endelevu ya kisiasa katika nchi yetu.

Tulianza badiliko la kutoka kwenye kutawaliwa na wakoloni kufikia kujitawala Mbantu mwenyewe!  Tena kutoka kwenye chama kimoja hadi kwenye vyama vingi. Sasa tungali tunalilia mabadiliko mengine. Je, hayo ni mabadiliko ya namna gani? Ni mabadiliko ya kifikra, kiutendaji na maboresho ya hali za wananchi. 

Mimi kwa mtazamo wangu ningefurahi kuona Serikali ijayo inaleta mabadiliko katika mfumo mzima wa utawala bora. Enzi za ukoloni tulikuwa na mfumo wa Serikali yenye mfumo uliojulikana kama utumushi wa umma – The Civil Service”.

Huo utumishi wa umma ndiyo uliokuwa uti wa mgongo wa Serikali. Palikuwa na kanuni za utumishi na sheria zitawalazo maeneo yote ya utendaji wa kazi katika Serikali na katika mashirika. Mfumo ule haukuhitaji watendaji wengi kama leo hii. Ulikuwa safi na wenye ufanisi. 

Katika kila wilaya alikuwapo mtawala mmoja akiitwa District Commissioner. Huyu alipata wasaidizi walioitwa Bwana Shauri (District Officer) Karani Mkuu, Mwangalizi Ofisi, Bwana Fedha na wasaidizi kadhaa. 

Aidha, kila wilaya ilikuwa na wataalamu wa fani mbalimbali – kilimo, ushirika, mifugo, barabara (supporting staff) maliasili na kadhalika. Walitoza kodi, walibuni miradi, walisimamia utekelezaji wote. Mpaka miaka michache baada ya Uhuru utaratibu huo wa utawala ulitumika. 

Pole pole, siasa ikaingizwa kwenye ule mfumo wa utumishi wa umma. Katika wilaya sasa pakawa na mwanasiasa akaitwa Eria Kamishna. Yule mtumishi wa umma aliyetawala wilaya kabla ya Uhuru, akaja kuwa katibu wa mwanasiasa huyu. Likaanzishwa jina jipya katika wilaya likiitwa Eria Sekretari yaani Katibu wa huyo Eria Kamishna. Watu wawili ofisi moja mishahara miwili kazi ni ile ile. 

Februari, 1972 kulikuja mabadiliko katika Serikali. Ulikuja mfumo mpya wa utawala na ulijulikana kama ‘Decentralization’ yaani madaraka mikoani tulivyoita wakati ule. Kama  ningali nakumbuka vema Mwalimu alisema hii, “The Government changes on February 1972 were designed to assist in making these developments effecting through the appointment of senior politicians as Regional Commissioners and by the appointment of a Prime Minister” (Nyerere: Uhuru na Maendeleo uk. 244) Mwalimu akiuelezea mpango huo alisema “in order to make a reality of our policies of socialism and self-reliance, the planning and control of development in this country must be exercised at local level to a much greater extent than at present” Kwa tafsiri yangu ni kwamba ili kufanikisha sera zetu za Ujamaa na Kujitegemea, upangaji na usimamizi wa maendeleo ya nchi hauna budi utekelezeke tangu kijijini (mahali) unakoibuliwa kuliko inavyofanyika hivi sasa – maelezo yote yanapangwa Dar es Salaam kule eti wanatakiwa utekelezaji tu!

Lakini Mwalimu alitoa angalizo katika hili aliposema, ipo hatari ya kuepukwa – Huu upelekaji wa madaraka mikoani na wilayani ufanyike kwa uangalifu isije madaraka namna hiyo kuweza kuhamishiwa kwa watendaji wenye ukiritimba kutoka Dar es Salaam kwenda huko wilayani.

Siyo nia au siyo lengo la mapendekezo haya kuja kuanzishwa utawala wa kibabe na uonevu au wa dhuluma kule mikoani na wilayani. Mwalimu alitumia maneno haya “Nor is it the intention of these proposals to create new local tyrants in persons of Regional and District Development Directors”.  Hapa labda inafaa turejee maneno ya Mwalimu ya mwaka 1962 katika kile kitabu chake cha TANU na RAIA aliwahi kuandika haya “Hatuna budi tuendelee na mazungumzo haya na watu wenyewe mpaka zipatikane njia za kuondoa shida zao ambazo ni zao na zetu pamoja. Baada ya hapo mipango itakuwa ni mipango ya wananchi wenyewe, siyo mipango waliyong’ang’anizwa na wakubwa kutoka juu kama ilivyokuwa kawaida ya Serikali ya kikoloni. Kwa njia hiyo wananchi wenyewe watajua jinsi ya kushughulika na wendawazimu wachache ambao pengine watapenda kuchafua mipango ya kuondoa shida zao”. Nasema Mwalimu alikuwa na dhamira ya kutuendeleza. 

 Hebu angalia leo hii katika kila wilaya wapo watawala wanne – yupo Eria Kamishna, anasaidiwa na DAS (Afisa Utawala). Yupo Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji/Manispaa akisaidiwa na District/Municipal Director (Mkurugenzi) hapo ofisi iliyokuwa ikitoa huduma kwa wilaya nzima enzi zile leo wapo viongozi wakuu wanne kwa kazi ile ile. Hii maana yake mishahara ya vigogo wanne, magari manne na kila mmoja ana wasaidizi kadhaa (supporting staff). Hapo gharama za uendeshaji Serikali katika wilaya zimeongezeka mara nne vivyo hivyo katika mikoa.  

 Ni mzigo kwa uchumi wa Taifa. Basi lile wazo zuri la kupeleka madaraka mikoani na wilayani la mwaka 1972 sasa limekuwa mzigo mzito kwa uchumi wa Taifa.  Maendeleo gani yamepatikana kiwilaya na kimikoa?

 Hapo inaonekana dhahiri mfumo ule wa kupeleka madaraka mikoani na wilayani uliolenga kusaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi mahalia, sasa lakini kama alivyoonya Mwalimu, kama kusingekuwapo watendaji dhalimu na wazembe, mfumo ule ungeibua maendeleo ya haraka sana vijijini. Lakini kama tunavyojua kumekuwapo na ulegevu na usimamizi mbovu wa baadhi ya watendaji katika nchi yetu. Dhuluma, uonevu, ubabe na dharau vilijitokeza. Wananchi hawakunufaika na utaratibu ule wa madaraka mikoani.   

  Vilifumuka vijiji vya Ujamaa visivyokuwa na mpangilio. Kule kusini watu walihamishwa katika malori kutoka kwenye mashamba yao na ardhi nzuri wakaenda kulundikwa sehemu kame wala hakukuwa na huduma kama nyumba za kulala, mashule, zahanati na kadhalika. Matokeo wananchi wakaichukia Serikali. Hapo ndipo ninapoona mabadiliko sasa yanahitajika kuifanya Serikali ipendeke kwa wananchi na waone inawatumikia.

Hapo ndipo wananchi wakajaa chuki na kusema wamechoka na CCM wanataka mabadiliko waone sera ya vyama vingine itawatendeaje. Ndipo mimi nisemapo, tunahitaji mabadiliko endelevu siyo mwendelezo wa uonevu. 

 

>>ITAENDELEA>>

By Jamhuri