Tanzania imechaguliwa kwa kura zote za ndiyo na nchi wanachama wa UNIDO kuwa Mjumbe wa Bodi ya Maendeleo ya Viwanda ya UNIDO kwa kipindi cha mwaka 2025-2029 na Mjumbe wa Kamati ya Programu na Bajeti ya UNIDO kwa kipindi cha mwaka 2025-2027 ikiwakilisha Kundi la nchi za Afrika katika Shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Uchaguzi huo ulifanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO’s General Conference) unaohitimishwa jijini Riyadh, Saudi Arabia, Novemba 27, 2025.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna, Mhe. Naimi S.H. Aziz ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru Mabalozi wote wa Ukanda wa Afrika wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna, Austria kwa imani kubwa walioipatia Tanzania katika kuwakilisha mataifa ya Afrika kwenye vyombo hivyo muhimu vya kisera na maamuzi vya UNIDO.

Balozi Naimi alieleza kuwa ujumbe kwenye Bodi ya Maendeleo ya Viwanda na Kamati ya Programu na Bajeti utatoa fursa ya pekee kwa Tanzania kushauri kuhusu sera na programu za shirika zinazohusiana na maendeleo ya viwanda, na kushiriki kikamilifu maamuzi ya mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya UNIDO kwa nchi wanachama.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Felister Mdemu; na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Juma Mwampamba.