Na Abdala Sifi WMJJWM- Dar Es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu amewasihi wahitimu wa mafunzo ya malezi mbadala/ malezi ya Kambo kuhakisha wanafikisha elimu hiyo katika jamii ili kuongeza idadi kubwa ya wataalam hao kwa mahitaji ni makubwa katika jamii.
Dkt Jingu amesema hayo leo tarehe 27 Novemba 2025 Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza katika mahafali ya 27 ya wahitimu 120 wa fani hiyo waliofuzu mafunzo hayo ya miezi sita ambayo yanaedeshwa na kusimamiwa na Shirika la Fair Start la Dermark kwa kushirikiana na SOS Village Tanzania kwa ushirikiano.

“Kesho ya Taifa letu inategemea Watoto wa leo, ambapo kwa bahati mbaya siyo wote wanaopata fursa ya kulelewa na wazazi wao, wapo watoto ambao wanalelewa na walezi mbadala, hivyo ni muhimu kuhakikisha pia na wao wanapata malezi mazuri kwa hatma njema ya kesho yao” amesema Dkt Jingu.
Ameongeza kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ina wajibu wa kusimamia malezi ya kambo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora kwa maendeleo na ustawi wao na Taifa kwa ujumla.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Shirika la SOS Tanzania Thomas Kipingili amesema lengo la kutoa mafunzo ya malezi mbadala ni kusaidia kuongeza wigo mpana wa elimu hiyo katika jamii, ambapo wahitimu wataweza kutoa huduma ya malezi mbadala katika maeneo yao na kuwafundisha wengine.

Naye miongoni mwa wahitimu wa mafunzo hayo Laizer Kirave amesema kupitia mafunzo hayo, wamepata uelewa mpana kuhusu malezi chanya, ulinzi wa mtoto, malezi mbadala/kambo, yanayozingatia haki za mtoto, pamoja na namna ya kuimarisha familia na jamii.
Ameongeza kwamba wataendelea kuhamasisha malezi salama, jumuishi na yenye kujenga utu wa mtoto, ili kujenga Taifa lenye watoto wanaothaminiwa, kulindwa na kuendelezwa ipasavyo.





