Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amewataka makandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona huku wakiendelea kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati.

Akizungumza wakati akiwasha umeme katika Kituo cha Afya cha Bwina, Chato, mkoani hapa pamoja na taa za barabarani zinazotumia nguvu ya jua, Dk. Kalemani amewataka pia wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya corona.

Amesema kuwapo kwa ugonjwa huo kusirudishe nyuma usambazaji umeme vijijini kwa kuwa tayari mamlaka husika zimetoa miongozo ya kujikinga na kujihadhari dhidi ya virusi hivyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kazi ya kusambaza umeme vijijini lazima iendelee kwa kasi na miradi ikamilishwe kwa wakati uliopangwa. Cha muhimu ninyi makandarasi ni kufuata miongozo iliyotolewa. Tufanye kazi, tusambaze umeme, wananchi wanataka umeme uwake,” anasema Dk. Kalemani.

Amesisitiza kuwa kuwapo kwa corona hakupaswi kuwa kikwazo cha maendeleo ya miradi ya umeme vijijini na ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme kwa kutumia maji wa Mwalimu Nyerere kwa kuwa elimu dhidi ya ugonjwa huo imefika kila kona ya taifa.

Kujenga tabia ya kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka misongamano na mikusanyiko na kutoa taarifa anapoonekana mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ni baadhi ya maelekezo yanayotangazwa mara kwa mara na Wizara ya Afya kwa Watanzania.

Kuhusu taa za barabarani alizoziwasha wiki iliyopita, Dk. Kalemani amesema lengo la kuziweka ni kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hizo nyakati za usiku.

Aidha, umeme katika Kituo kipya cha Afya cha Bwina utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya wakati wote kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa.

Ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu hiyo idumu kwa muda mrefu.

Katika ziara hiyo, Dk. Kalemani alichukua tahadhari kwa kutofanya mikutano ya hadhara na wananchi, kuweka umbali muafaka kati  yake na maofisa alioambatana nao wakiwamo waandishi wa habari huku wote wakinawa mikono kila mara.

Ikumbukwe Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka mawaziri na viongozi wote kuhamasisha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

2309 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!