MAGUFULIMgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewataka Watanzania kupuuza majigambo ya vyama vya ushindani akidai endapo watashinda uchaguzi huu, watawatesa wananchi.

Kadhalika, Dk. Magufuli ameshangazwa na mabosi wake wa zamani-mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa kubeza kwamba CCM haijafanya lolote tangu ilipokuwa TANU.

“Miongoni mwa mafanikio waliyopata ni kuaminiwa na chama hiki na kupewa uwaziri mkuu. Mmoja amengoza miaka 10 na mwingine miwili. Nafasi nyeti ambayo iliyowapa nafasi ya kuifanyia makubwa nchi hii. Hawakufanya, wataweza sasa? Bora wakakaa kimya,” anasema Dk. Magufuli.

“Wengine wanakuja hapa wasema, watawaondolea nyumba za nyasi na tembe, mimi naomba muwahoji je wameondoa hizo nyumba kwenye majimbo waliyoongoza?” anahoji Dk. Magufuli bila kutaja majimbo hayo.

Sumaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Hanang ambalo kwa sasa linaongozwa na Dk. Mary Nagu wakati Lowassa ameliacha jimbo la Monduli kwa Namelok Sokoine aliyekuwa mbunge wa viti maalimu katika bunge la 10.

“Mimi kama nilivyosema, sitaki kusema uwongo. Mimi nataka kuwa mkweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, ninachoahidi hapa ujue nitatekeleza,” anasema Dk. Magufuli akiwa safarini kwenda Mbeya kuendelea na kampeni.

Dk. Magufuli anajaribu kutafakari yanayosemwa na viongozi hao hasa wanavyomsakama, na kudai kuwa amebaini kuwa huenda hawajui wanachokifanya wakati wanaongoza nchi na yeye akiwa naibu waziri baadaye waziri kamili.

“Sijui, maana walikuwa katika madaraka hayo (ya uwaziri mkuu) kama washauri wakuu wa marais waliopita akiwamo huyo mzee mtarajiwa Rais Kikwete, sijui,” anasema Dk. Magufuli huku akionyesha mshangao.

Anasema: “Hata siku moja huwezi kubeza miaka 54 ya uongozi wa CCM halafu ukamtaja Mwalimu Nyerere, maana naye yumo ndani ya miaka hiyo 54. Ina maana naye unamzomea?

“Mimi nakwenda kuendeleza pale walipoishia wengine,” anasema na kuweka tahadhari kuwa wanaotaka kuingia Ikulu kwa mgongo wa fedha, “Ni hatari.”

Hata hivyo, Sumaye amemjibu mara moja Dk. Magufuli juu ya ‘makombora’ yake dhidi ya Mawaziri wakuu wastaafu, akisema, “Dk. Magufuli ameasi nguvu ya Rais Kikwete na ndiyo maana anajitangaza yeye.

“Wewe soma mabango yake, yameandikwa chagua Magufuli. Lakini pia msikie anavyosema: Serikali ya Magufuli kana kwamba nchi ni yake peke yake. Nchi hii ni ya Watanzania wote.”

Anasema, “Lakini sisi tunasema Serikali ya Rais Kikwete imeua uchumi na CCM itoke kwa sababu haina miujiza ni kwa sababu tulikuwa huko. Hatukufanya chochote kwa sababu  ya mfumo lakini tulipunguza hata gharama za maisha, leo hii, sukari, mafuta, mchele na unga mlalahoi hawezi kununua. Utashangaa nini?”

Lakini Dk. Magufuli anasema kwamba CCM imefanya mengi na makubwa ukilinganisha na nchi nyingi barani Afrika zenye umri kama wake. 

Anasema kwamba kuna taarifa za kimataifa ikiwamo ya Taaisis ya KPMG inayoelezea nchi na miji inayokua kwa kasi kubwa barani Afrika.

“Hivi jamani mimi nihoji, unaweza kukua kwa kasi bila amani? Nchi hii ina amani na mimi nakwenda kuongoza Tanzania yenye amani na upendo,” anasema na kuongeza:

Kutokana na sera za CCM, Tanzania ni nchi ya sita baada ya Afrika Kusini, Nigeria, Angola, Msumbiji na Ethiopia zinazovutia wawekezaji wengi ambao wanajitokeza kwa wingi barani Afrika. 

“Wawekezaji wanakimbilia Tanzania kuweka mitaji, kungekuwa hakuna amani wangekuja? Si Rahisi kwa mtu kama Dangote awekeze Mtwara kiwanda cha Saruji .Mimi nahoji na ninyi mpime,” anasema Dk. Magufuli.

Anasema kwamba Tanzania iko kwenye nchi kumi bora Afrika zinazoongoza kwa uchumi maridadi unaokuwa kwa kasi.

“Vyombo vya habari na Watanzania wafanye utafiti. Tatizo watu hawapendi kufanya utafiti. Wasome wapete taarifa,” anasema.

Kwa upande wake anasema hata yeye hawezi kujivunia kujenga barabara kilometa zaidi ya 17,000 na madaraja bila nguvu ya Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa anahaha kila kona ya dunia kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili.

Anasema barabara nyingi, zikiwemo zile za kiwango cha lami, ni sehemu ya kazi nzuri iliyofanywa na CCM chini ya awamu nne za uongozi kuanzia Mwalimu Julius Nyerere hadi sasa Rais Jakaya Kikwete yeye akimwita “Mzee mtarajiwa” akiwafuata Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Anasema akiingia madarakani wakulima wataendesha kilimo chenye tija, huku ujenzi wa shule za sekondari sambamba na mabweni utaendelezwa kwani serikali atakayoongoza elimu itakuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Kwa upande wa sekta ya afya, Dk. Magufuli anasema Serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha sekta hiyo inaimarishwa na kuboreshwa zaidi ili wananchi waweze kupata tiba stahili na kwa wakati.

Anakiri: “Kuna changamoto iliyopo ni uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji katika hospitali yetu ya wilaya, mimi nasema Serikali ya Magufuli, eeh, uwiii hili tunaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi kero hii ili hospitali hii iwe kimbilio la wananchi wengi,” anasema.

“Ole wenu muwaweke madarakani hao. Ulizeni Libya, ulizeni Iraq. Leo wanajuta. Uamuzi ni wenu na ningependa mnipe kura nyingi na si asilimia 65 au 75, nataka asilimia 95,” anasema.

Anasema kwamba CCM imeamua kwa dhati kukomesha rushwa ndani ya chama na serikalini na ndiyo maana anahubiri mabadiliko ndani ya chama kimoja.

Anasema ili kukomesha rushwa inayoitafuna Tanzania kwa sasa ni kuanzisha kwa mahakama ya mafisadi maalumu kwa ajili ya kushughulikia watuhumiwa wa rushwa.

By Jamhuri