Wiki iliyopita Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alisoma mipango lukuki katika bajeti ya Wizara ya Uchukuzi. Sitataja takwimu maana hizo kila awaye amezisikia. Sifurahi kutaja hata kiasi cha fedha zilizotengwa maana siku hizi namba zinatajwa bungeni, katika utekelezaji inakuwa sifuri.

Nimefurahishwa na mpango wa Dk. Mwakyembe kufufua reli ya Kati na nimefurahishwa pia na mpango wa kurefusha reli ya TAZARA kutoka Dar es Salaam hadi Tanga. Mipango hii ni mizuri na inapendeza masikioni. Nilipata kuandika kuwa nchi hii haiwezi kuendelea bila reli ya kuaminika.

 

Mizigo mikubwa inayosafirishwa kwa magari na kuharibu barabara, ilipaswa kusafirishwa kwa reli. Tusichofahamu au tunachosahau ni kwamba reli inachukua mzigo mwingi kwa wakati mmoja na ikiboreshwa ikawa ya umeme, kwa maana ya kuwa treni ya kasi itaongeza ufanisi ajabu.

 

Kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa wastani kuna umbali wa kilomita 1200. Umbali huu kama unatumia treni ya umeme ni mwendo wa saa nne tu. Treni za umeme zinakwenda kasi kati ya kilomita 350 hadi 570 kwa saa. Lori hata kama ikiwaje haliwezi kwenda kasi hiyo.

 

Ukithubutu kulikimbiza lori kama FIAT kwa kasi hiyo, mabati yote yatachanika na litapepesuka na kutoka barabarani. Behewa lina uzito wa kutosha. Likiwa kwenye reli, linakuwa limejishindilia. Likiwa na mzigo wa kutosha pia, unakwenda kasi hiyo bila wasiwasi wowote.

 

Sitanii, kinachotokea sasa ni kuhujumu uchumi. Kwamba mwaka 1906 Mjerumani aliona inafaa mizigo bandarini kutolewa kwa reli akajenga reli ya kati, leo miaka 107 baadae sisi tunaona reli haifai, bali tuingize bandarini malori yanayotoa kontena moja moja.

 

Tatizo hapa si upungufu wa uelewa, bali ni kwa makusudi matajiri na wanasiasa wachache wanaamua kuua reli kupata fedha za malori. Tulimsikia Ezekiel Maige akisema kuwa anamiliki malori mawili yanayomwingizia dola 20,000 kila mwezi, sawa na Sh milioni 26. Wapo wanaomiliki malori 200.

 

Wamiliki wa malori wanahonga viongozi wa kiserikali na kukwamisha mipango ya kuzuia malori. Utitiri wa malori yenye kuharibu barabara, utajiondoa wenyewe treni ikifanya kazi kwa ufanisi. Je, nani yuko tayari kumfunga paka kengele? Hapo ndo tatizo lilipolala.

 

Sitanii, kuhusu suala la ndege ni aibu. Nimejaribu kufuatilia bei za ndege katika viwanda mbalimbali Ulaya na Amerika. Kwa wastani wa dola milioni 80 au sema Sh bilioni 150 tunaweza kupata ndege nzuri aina ya Boeing 737. Tunaweza kuchukua makusanyo ya mwezi mmoja ya TRA tukanunua ndege tatu kama nchi. Boeing zinaweza kuchukua kati ya abiria 85 na 215.

 

Ukiacha Boeing, zipo ndege nyingine kama ATR-72 zinazotumiwa kwa wingi na shirika kama Precession zinauzwa kwa bei ndogo usipime. Hizi zinauzwa kati ya dola milioni 16 na 20. Zina uwezo wa kubeba kati ya abiria 48 na 88. Hapa unazungumzia wastani wa Sh bilioni 30 kwa kila ndege.

 

Hii ina maana kuwa kama tukitoa Sh bilioni 150 kama nchi, tunaweza kupata ATR-72 zipatazo tano. Ndege hizi zina uwezo wa kufanya kazi hadi miaka 30, hivyo kwa maana nyingine kama umenunua ndege moja Sh bilioni 30, unaweza ukachukulia kwa mfano kuwa Kila mwaka ndege imekugharimu Sh bilioni moja.

 

Sitanii, ukichukua hiyo Sh bilioni moja kwa mwaka ukaigawa kwa miezi 12 ni sawa na Sh 83,333,333 kwa mwezi. Bado inawezekana ukaona kiasi hiki ni kikubwa, lakini ukikigawa kwa siku 30 za mwezi unakuta kuwa ndege inapaswa kutengeneza Sh 2,777,777 kila siku kurejesha msingi.

 

Ndege hii ikifanya kazi ya Dar es Salaam kwenda Afrika Kusini na kurudi, ikabahatika kupata abiria 40 kwa wastani wa dola 1,000 kwa kila abiria ukichanganya na mizigo, ina maana itapata dola 40,000 sawa na milioni 72. Ukiweka gharama za uendeshaji tusema milioni 22 kwa siku, hii ikiwa ni mafuta, wafanyakazi, bima na kodi nyinginezo, hakika kila siku utalaza Sh milioni 47.3. Huu ni utajiri wa kutisha.

 

Najua wapo watakaosema gharama za uendeshaji ni kubwa, nasema ndio ni kubwa kwa sababu hatuna mipango sahihi. Huwezi kumiliki ndege moja, ukawa na wafanyakazi 3,000. Idadi ya wafanyakazi inapaswa kuongezeka kadri ndege zinavyoongezeka.

 

Huwezi kuwa na ndege kama za ATC ambazo uaminifu ni sifuri kwa tiketi kuonyesha umepakia watoto ndege yote, lakini unashusha kreti 10 za bila zilizonyewa kwenye ndege inapotua uwanjani. Watoto wanabwia kreti 10?

 

Huwezi kuwa na Shirika kama ATC ambalo wafanyakazi wakifika saa 9:30 mchana wanafunga biashara na kwenda kulala nyumbani. Nadhani ili tutoke hapa, ATC ibadilishwe kutoka Shirika kuwa Mamlaka. Ijitegemee kila kitu bila ruzuku kutoka serikalini, watachapa kazi. Vinginevyo, tumeamua wenyewe kuua mashirika haya.

Please follow and like us:
Pin Share