Wiki moja iliyopita, mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba, aliwaaga wachezaji wenzake wa Chelsea baada ya kuitumikia timu hiyo kwa miaka minane akitokea Marseille mwaka 2004.

Wakati timu hiyo ya Ufaransa ikimaliza Ligi Daraja la Kwanza (Legue 1) nchini humo ikiwa katika nafasi ya 10, Chelsea imekuwa ya sita kwenye Ligi Kuu ya England, lakini imepata mafanikio makubwa kuliko zote msimu huu.

Imetwaa mataji mawili ambayo ni Kombe la Chama cha Soka cha England (FA) na Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya – lile ambalo ni kubwa kushinda yote katika mchezo huo katika bara lolote duniani.

Wakati akiondoka Chelsea licha ya juhudi kubwa za kutaka abaki aendelee kuitumikia zilizoanza hivi karibuni, huko Italia, mshambuliaji mwingine maarufu nchini humo, Ulaya na duniani kote, Alessandro del Piero, amestaafu soka lake kwa huzuni baada ya timu yake aliyoichezea kwa miaka 19 mfululizo, Juventus, kusambaratishwa katika fainali ya Kombe la Coppa, siku tisa zilizopita.

Juventus, maarufu kama Kibibi Kizee cha Turin ilikung’utwa mabao 2-0 na Napoli katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Olimpico uliopo mjini Roma.

Hata hivyo, furaha yake katika timu hiyo aliyoanza kuichezea mwaka 1993 ni kubwa zaidi ikilinganishwa na huzuni aliyokuja kupata. Amenyakua mataji 19 akiwa nayo likiwamo Kombe la Dunia la klabu mwaka 2006.

Tofauti na Del Piero (37), Drogba ameiacha Chelsea ikiwa Klabu Bingwa ya Soka ya Ulaya baada ya siku ileile iliyolizwa Juventus huko Italia, kunyakua Kombe hilo kwa kuifunga Bayern Munich ya Ujerumani kwa penalti 4-3 nyumbani kwake, Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich.

Awali, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika muda wa dakika 120. Hapo ndipo hatua ya kupigiana matuta ilipokuja na Chelsea kulinyakua Kombe hilo, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe.

“Nimechukua uamuzi huu mgumu kwa makusudi. Siko tayari kukaa benchi na kuangalia wengine wakicheza…Hicho ndicho kitu pekee nilichoshindwa kukifanya,” alisema nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ivory Coast (The Elephants) alipokuwa akizungumza na wachezaji wenzake wa Chelsea jijini London, wiki moja iliyopita.

Aliongeza: “Kwa hiyo, wakati wangu wa kuondoka hapa sasa umefika, nitakwenda sehemu nyingine isiyojulikana. Nataka kutengeneza historia tofauti.”

Alieleza kwamba hakutaka kulisema jambo hilo kwa namna nyingine isipokuwa kuwaambia wachezaji wenzake akiwa nao uso kwa uso.

“Hatutakuwa pamoja msimu ujao. Kama nilivyoamua kuondoka, hakika nilitaka kuwaambia wote huku tukiangaliana hivi,” alisema.

Alikiri kuwa alitaka kubaki na timu hiyo ya Stamford Bridge, London, endapo ingeshindwa kunyakua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, lakini baada ya kufanikiwa ameshindwa kuamua vinginevyo.

Pamoja na kutotaja timu anayokwenda kuichezea, Drogba ambaye mkataba wake na Chelsea unamalizika rasmi Juni 30, mwaka huu, anahamia Shanghai Xinhua ya China.

Tangu mwaka huu ulipoanza, mshambuliaji huyo amekuwa akihusishwa kuhamia huko hasa baada ya mshambuliaji mwingine aliyekuwa na Chelsea, Nicholaus Anelka kujiunga na timu hiyo iliyopania kulijenga soka la China duniani.

Tofauti na mshahara wa pauni 150,000 kwa wiki (shilingi milioni 360,000) anaolipwa na Chelsea, Drogba atakuwa analipwa pauni 250,000 (shilingi milioni 600) akiwa na Shanghai Xinhua.

Baada ya miguu yake kuiwezesha Chelsea kuwa Klabu Bingwa Ulaya; watendaji wake, wachezaji wenzake na mmiliki wake, Roman Ibramovich walianza harakati za kutaka abaki ili aendelee kuitumikia akiwa na mkataba mwingine.

Kwa mfano, wachezaji walimwomba hadharani na kuwahamasisha mashabiki wa timu hiyo waungane nao kumshawishi, kampeni ambayo iliongozwa na nahodha John Terry, Jumatatu ya wiki iliyopita, wakati kikosi hicho kiliporejea jijini London kutoka Munich, Ujerumani.

Lakini alipopewa kipaza sauti, Drogba hakulijibu suala hilo au kulizungumzia kwa namna yoyote. Alisema kwa kifupi: “Furaha yetu ni kutwaa kombe hili,” kisha akarudisha chombo hicho kwa Terry na kuendelea kushangilia ubingwa huo.

Kabla ya kumalizika rasmi kwa msimu wa Ligi Kuu ya England wiki mbili zilizopita, timu kadhaa zilitajwa kutaka ajiunge nazo ili azitumikie, moja kati yake ikiwa Real Madrid ya Hispania inayonolewa na kocha maarufu wa Ureno, Jose Morinho.

Nyingine ni klabu aliyotokea wakati akihamia England mwaka 2004, Marseille ya Ufaransa na Manchester City ya England, timu ambayo hatimaye imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara yake ya kwanza baada ya miaka 44 tangu ilipolinyakua taji hilo mwaka 1968.

Kuondoka kwa Drogba kutoka Chelsea kunahitimisha kizazi kilichokutwa na mmiliki wake wa sasa, Roman Ibramovich alipoinunua mwaka 2006. Mrusi huyo anajaribu kuijenga upya kwa kusajili wachezaji chipukizi ili kuifanya iwe kali, ngumu na bora zaidi uwanjani.

Akisemekana kutumia kiasi cha pauni bilioni moja kutafuta ubingwa wa Ulaya, Abramovich amekuwa akifukuza makocha mara kwa mara na mwaka huu peke yake ametimua wawili.

Wa mwisho katika orodha ya makocha waliotimuliwa ni Andre Villas-Boas (AVB) baada ya kuwa naye kwa miezi michache tu. Kabla yake ilikuwa zamu ya kocha Mtaliano, Carlo Anceloti, kutimuliwa, kisha mikoba ikakabidhiwa kwa aliyekuwa msaidizi wa AVB, Roberto Di Mateo. Huyo ndiye aliyeipa Chelsea Kombe la FA na Kombe la Ulaya.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya ubingwa wa Chelsea kwa mataji hayo yote, imetokana kwa kiasi kikubwa zaidi na kuwapo kwa Drogba dimbani katika mechi zote na kuifungia mabao yaliyoipa heshima hiyo.

Yeye ndiye aliyeipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Barcelona katika mechi ya kwanza ya nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, London, hatua iliyowezesha kuitoa timu hiyo ya Hispania ilipotoka nayo sare ya mabao 2-2 ziliporudiana wiki mbili baadaye ugenini.

Katika fainali dhidi ya Bayern Munich siku tisa zilizopita, Drogba aliisawazishia Chelsea dakika nne tu baada ya kutangulia kufungwa bao katika dakika ya 83. Alisawazisha kwa mpira wa kichwa katika dakika ya 88.

Baada ya dakika 120, Drogba pia ndiye alipiga penalti iliyoipa timu yake hiyo ubingwa huo. Mkwaju wake ndiyo ulioamua mshindi na kama angekosa inawezekana kombe hilo lingeenda Bayern Munich.

Didier Drogba alizaliwa Machi 11, 1978 jijini Abidjan, Ivory Coast na ana urefu wa futi 6.125.

Katika umri wake wa miaka 34 hivi sasa, hakika hawezi kurudi na kucheza tena katika ligi ngumu za Ulaya hapo baadaye, hivyo amemaliza enzi zake huko akiwa amepata mafanikio ya kujivunia na heshima kubwa katika mchezo wa kandanda duniani.

By Jamhuri