Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Huduma za Ufundi kutoka Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Dismas Massawe amejipanga kuhakikisha miradi wanayoitekeleza inakamilika kwa wakati.

Akizungumza katika banda la ETDCO kwenye maonesho ya 48 ya Kimataiafa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), maarufu Saba Saba, amesema lengo la kuanzishwa Kampuni hiyo ni kwaajili ya kufanya kazi zote za ukarabati na ujenzi wa Miundombinu ya usafirishaji na usambazaji Umeme Tanzania .

“Kwasasa hivi tuna miradi mingi ikiwemo Mkoa wa Katavi, Geita, Kigoma na mradi wa msongo wa Kilovolts 132 wa usafirishaji Umeme katika Mkoa wa Tabora. Pia tuna miradi katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya ambayo hiyo ni ya ukarabati umeme.

“Sasa hivi tunatekeleza mradi wa msongo wa Kilovolts 132, 220, 33 na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya msongo wa Kilovolts 22 kwenda 33. Kwahiyo tuna miradi katika Mikoa 10 hadi 12 kwa Tanzania. Baadhi ya Mikoa hiyo ni Mbeya, Mtwara, Lindi, Katavi, Geita, Kigoma, Arusha, Dodoma, Pwani na Dar es Salaam.

“Katavi kuna miradi ya aina mbili mradi wa Msongo wa Kilovolts 132 kutoka Tabora hadi Katavi wenye thamani Sh. bilioni 116 na tunatarajia kuukamilisha Oktoba mwaka huu. Lakini pia tuna mradi wa Mbeya ambao ni wa REA thamani yake ni sh. Bilioni 54 ambao unasambaza umeme katika vijiji 139 na mpaka sasa tumeshambaza katika vijiji 130 na mradi huu utakamilika mwishoni mwa Julai mwaka huu,” amesema.

Ameongeza kuwa, wana mradi wa Msomera ambao ni wa Kujenga Miundombinu ya usambazaji Umeme katika nyumba 5000 zinajengwa na serikali na mpaka sasa wanasambaza kwenye nyumba 2500 za awali ambapo awamu hiyo ya kwanza utakamilika mwezi wa saba, mwaka huu.

“Kwa nyumba 2500 zilizobaki zitakamilika ndani ya mwaka huu ambazo zitajengwa kwenye eneo la Kilindi na Simanjiro,” amesema.

Naye Meneja wa fedha kutoka Klkampuni hiyo CPA Sepetu Nyembo amesema kuwa kila mwaka mapato ya kambuni hiyo yamekuwa yakiongezeka.

“Mwaka wa fedha 2020/ 2022 kampuni ya ETDCO iliingiza jumla ya bilioni 48 kwa hesabu ambazo zimekaguliwa na mwaka wa fedha 2022/2023 ambao umeishia juni 30 imeingiza bilioni 64.5 na mwaka huu ambao umeisha juzi kampuni hii inatarajia kuwa na bilioni 90 lakini hesabu hii bado haijakagukiwa,” ameeleza CPA Nyembo.

CPA Nyembo amesema kuwa wao kama taasisi ya Umma wanakaguliwa na serikali, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Afrika Nashariki Staphane Nchimbi amewataka watanzania ambao wapo karibu na nguzo za umeme na hawajavuta umeme huo wavute kwa kuwa ETDCO kazi yake ni kuwahudumia watanzania hao.

Aidha ameipongeza serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa ambazo zinafanya na serikali hiyo ya Uwekezaji katika miundombinu ya umeme huku akisema wao kama waandishi wa habari watakuwa pamoja Kampuni hiyo katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi juu ya kazi zinazofanywa na ETDCO.