NA CHARLES MATESO

Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Pombe Magufuli, alipotoa agizo kwa wasaidizi wake nchi nzima kuhusu kuorodhesha mali zote za chama hicho, nikakumbuka uwepo wa viwanja vingi vilivyochakaa.
Kauli ya Magufuli kutaka kuorodhesha mali sahihi ni muhimu kusemwa katika nyakati hizi za uhuru mpana wa kidemokrasia.
Kwa sisi tulio na ukaribu na mchezo wa soka na michezo mingineyo, tunayo kila sababu ya kukikumbusha chama hicho kwamba suala muhimu zaidi baada ya kuorodhesha rasilimali zote ni kuziboresha kulingana na ulimwengu wa leo.
Kila tukio la kitaifa linalofanyika kwenye mojawapo ya viwanja vingi vinavyomilikiwa na CCM, huwa na ushahidi wa miundombinu ya thamani kuachwa ikiharibika bila uangalizi wa maana.
Sherehe za Uhuru zinaporushwa hewani na vituo vya runinga, huonekana wafanyakazi wakiwa na mabango yao, lakini pembeni tu ya upitaji wao karibu na jukwaa la mheshimiwa, kunaonekana nyasi za uwanja zikiwa zimechakaa kwa kukosa matunzo. Hali hii si kwamba hujionyesha kwenye uwanja mmoja tu kati ya viwanja vingi vinavyomilikiwa na CCM.
Kila mwaka kwenye matukio ya kitaifa, fedheha hii huwa inajirudia. Naamini kwa umakini wa uongozi wa CCM wa Awamu ya Tano, yanaweza kugundulika madudu mengi kuhusiana na watu fulani kuzembea kufanya kazi yao ya utunzaji wa rasilimali.
Hili la ugunduzi wa uzembe katika usimamizi mzuri wa rasilimali za CCM, pengine kwa asilimia kubwa litachangia katika kuleta msukumo mpya wa ukarabati na utunzaji wa viwanja ambavyo vinamilikiwa na chama hicho.
Magufuli ameongelea baadhi ya mapinduzi muhimu yanayopaswa kufanyika ndani ya chama hicho ili kiweze kuendana na maisha halisi ya muongo wa sasa. Naamini kwamba mojawapo ya mapinduzi yanayopaswa kupewa msukumo maalumu ni yale yenye kuhusiana na kuvitumia viwanja kibiashara zaidi.
Baada ya fedha kutengwa kwa ajili ya ukarabati wa viwanja na vikishakuwa vimekarabatiwa, basi kinachofuata ni kutengeneza mfumo wa kibiashara ambao utavifanya viwanja hivi viwe chanzo kingine muhimu cha mapato.
Ukarabati mpana unahitajika, wala si sehemu ya kuchezea mpira peke yake. Baadhi ya viwanja havina hata vyoo. Mfano Uwanja wa Mkwakwani, watu huwa wanajisaidia haja ndogo nyuma ya magari yanayopaki nyuma ya jukwaa la mgeni wa heshima.
Uwanja huo huo wa Mkwakwani umekuwa na sifa mbaya ya mashabiki kuweza kuwadhuru wachezaji na waamuzi. Atakayepewa tenda ya kuvihakiki viwanja hivi, aifanye kazi yake kitaalamu sana, si kulipua huku mtu akiwa mwepesi kuulizia malipo ya kazi yake ambayo imefanyika kienyeji bila ya kuangalia ubora uliohitajika.
Ipo haja kwa CCM kuwa makini sana katika ufuatiliaji wa kazi kwa wale waliopewa jukumu la kuzirejesha rasilimali zote za chama katika ubora uliokuwepo awali.
Nyakati ambazo Azam TV inatoa fedha nyingi kila msimu kwa ajili ya udhamini, ni nyakati ambazo viwanja vinapaswa kulingana na hadhi mpya iliyoboreshwa. Nyakati ambazo watu wanashawishiwa kujenga miundombinu mingi ya michezo huko mikoani, ni nyakati ambazo viwanja vinavyomilikiwa na CCM vinahitajika kuwa katika ubora wenye kulingana na ule wa miundo mipya ya taasisi binafsi.
Haileti heshima kwa serikali ikiwa katika Mkoa kama wa Ruvuma kunakuwa na Uwanja wa Majimaji wenye nyasi zenye rangi nyekundu, halafu umbali usiozidi kilomita moja kuna taasisi binafsi yenye uwanja mzuri na wenye kupata kila aina ya matunzo.
Viwanja hivi ambavyo ni mali ya CCM vinaweza kuwa ni chanzo kingine cha ajira, kuanzia katika michakato ya ukarabati unaotarajiwa kufanyika mpaka katika utunzaji wake wa baadaye baada ya zoezi la ukarabati kumalizika.
Ukarabati wa viwanja utakuwa umetenda haki kwa soka kwa ujumla wake.
Hakutakuwa na sababu kwa kocha Mzungu anayefundisha timu ya Dar kulalamikia ubovu wa uwanja kama sababu ya timu yake kufungwa ugenini.
Hakutakuwa na pengo kubwa la ubora wa mechi inayochezwa pale Uwanja wa Taifa au Chamazi kulinganisha na ile itakayochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro au Dodoma ambao utakuwa umekarabatiwa.
Kutakuwa na ongezeko la ushindani kati ya wachezaji wa timu zetu na ongezeko la ufanisi wa ufundishaji wa makocha wao. Pia CCM kama mmiliki wa viwanja, kitakuwa ni chama ambacho hakionekani kutumia vibaya ushawishi na ukongwe wake katika medani za siasa za Tanzania.
Cha muhimu zaidi ni kuangalia namna mbalimbali ambazo zitavifanya viwanja viingize fedha nyingi ambazo zitakatwa kodi itakayokwenda kuyaboresha maisha ya Mtanzania wa kawaida.
 
Wanasemaje?

Aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Aussems, alikiri mapema hili na kusema viwanja vya Tanzania ni tatizo kubwa.
“Kuna tatizo, lakini ukitaka kusema ukweli lazima upewe adhabu, ni bora kukaa kimya.”
Kocha wa muda wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa Master, naye anakubaliana kuwa viwanja vingi ni tatizo na kunapaswa serikali ikashirikiana na CCM ili kuviendeleza.
“Viwanja vingi vipo chini ya CCM, huu ni uwekezaji mkubwa lakini vinapaswa kuendelezwa ili viwe bora zaidi,” anasema.
 
Tamati…
 
caption
Wachezaji wa timu ya Yanga wakipewa mawaidha na walimu wao wakiwa kwenye benchi la wachezaji wa akiba kutokana na ubovu wa vyumba vya kubadilishia nguo katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati walipocheza na timu ya Majimaji katika kinyanganyiro cha Ligi Kuu Tanzania Bara miaka mitatu iliyopita. Uwanja huo bado haujafanyiwa matengenezo yoyote makubwa hadi sasa.

865 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!