Jina Tanganyika lina kasoro gani?

Rasimu ya Katiba inaeleza, “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye Mamlaka Kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.” (Sura ya kwanza – Jamhuru ya Muungano 1. (i).

Katika sura hiyo hiyo eneo la Jamhuri inasema, 2. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari.

 

Ukiendelea kusoma rasimu hiyo, kwa mfano, katika sura ya sita kuhusu Muundo wa Jamhuri ya Muungano, sura ya nane kuhusu Utaratibu wa Mahusiano ya Washirika wa Muungano na sura nyingine kadhaa utakutana na maneno Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Wala hutakutana na neno Tanganyika wala neno Tanzania Zanzibar kutawala. Hapo ndipo hasa ninapokusudia kuzungumza. Tanganyika kuwa Tanzania Bara na Zanzibar kuwa Tanzania Zanzibar.

 

Kwanza nikiri kwamba mimi si mwanahistoria wala mwana-akiolojia. Simulizi na maandiko ya historia na mambo ya kale niliyopata nyumbani na shuleni vimenifahamisha kuwa majina ya nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar – yamebuniwa na kuanzishwa na wakoloni waliotawala nchi hizo.

 

Neno Tanganyika linatokana na dhana mbili tofauti zinazoelezwa na watu. Kwanza ni neno lililotumika na  wakuzi walioishi kulizunguka lile ziwa kubwa kule mkoani Kigoma wakiliita ziwa hilo ‘Tanganyika’. Dhana ya pili inaelezwa kutokana na neno la mji ‘Tanga’ na ‘Nyika’ nje ya mji huo, na kupata jina kamili Tanganyika.

 

Waingereza walipotawala nchi yetu mnamo mwaka 1919 walichagua jina jipya ambalo ni Tanganyika, kuacha jina la German East Africa lililotumiwa na wakoloni waliowatangulia Wajerumani.

 

Neno Zanzibar linalowezekana linatokana na neno ‘Zhengbar’ la Kiajemi lenye maana ya Zeng – rangi nyusi na bar – ardhi au eneo. Tafsiri ya Kiarabu ya neno hilo lilikuwa ni Zinjibar. Baadaye wenyeji na wageni waliita Zanzibar.

 

Majina ya Tanganyika na Zanzibar yalitumika enzi zote za ukoloni, na hata baada ya nchi hizo kujitawala. Muungano wa nchi hizo April 26, 1964 majina yaliendelea kutumika “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”.

 

Katika kuimarisha uhusiano na udugu wa nchi hizi, mnamo Oktoba 29, 1964 majina hayo na neno Azania kwa maana ya Pwani, yalisanifiwa na kutoa neno TANZANIA.

 

Kumbukumbu zangu katika Tanganyika zimechukuliwa herufi TAN. Neno Zanzibar zimechukuliwa herufi ZAN ili kuleta ladha ya matamshi na urahisi wa kuandika, katika neno la Azania zimechukuliwa herufi IA na kupata neno kamili Tanzania.

 

Hadi leo, sijui asili, mantiki, maana na misingi ya kutumia maneno Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar badala ya Tanganyika na Zanzibar. Wala sifahamu mtu, kikundi au chombo kilichoanzisha na kukoleza maneno hayo kutumika.

 

Hivi, tunaposema Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar haturudii neno lilelile? Ndiyo maana ndugu zetu Wazanzibari hawapendi kutumia Tanzania Zanzibar, wanatumia Zanzibar. Vipi sisi watu wa Bara hatupendi kutumia neno Tanganyika?

 

Wasiwasi na mashaka niliyonayo kuhusu asili na matumizi ya neno Tanzania Bara haipo kwangu tu, bali hata baadhi ya wananchi na viongozi wana mashaka hayo. Kiongozi wangu mmoja wa siasa hapa nchini, Mchungaji Christopher Mtikila wa Chama cha Demokratiki (DP), daima katika mazungumzo yake hutumia neno Tanganyika, na anauliza Serikali ya Tanganyiaka iko wapi?

 

JAMHURI ilimuuliza Mhe. Njela Kasaka: Je,  unakubaliana na Tanganyika kuitwa Tanzania Bara? Mhe. Kasaka  akajibu; “Nchi zilizoungana ni Tanganyika na Zanzibar. Zinapobadili utaratibu wa Muungano, mnayoitoa pale ni Tanganyika tu. Tanzania Bara haikuwapo. Jina hili limetumbukizwa hapa katikati.

 

“Hata mimi sijui kikao gani kilichopitisha Tanzania Bara, sijawahi kuona. Nchi ninayoijua ni Tanganyika. Tunazungumzia juu ya Zanzibar na Tanganyika hatuundi Tanzania Bara.”

 

Majibu ya Mhe. Kasaka na hoja za Mchungaji Mtikila pamoja na utafiti niliyofanya sijapata jibu la kutumia neno Tanzania Bara. Iweje Tume ya Mabadiliko ya Katiba itumie neno  Tanzania Bara na Zanzibar kwa marefu na mapana na wasite kutumia neno Tanganyika na Tanzania Zanzibar?

 

Endapo hoja ya muundo wa Serikali mbili au tatu itapita, tutaendelea kutumia Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar? Kama jibu ni ndiyo, sababu zake za msingi ni zipi? Tunaficha nini, au tuna sababu gani za kukataa kutumia majina halisi? Naomba majibu.

Please follow and like us:
Pin Share