Rais Kikwete ana uzuri, ubaya wake
Siwezi kuamini kwamba Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, ni binadamu asiye na upungufu, la hasha!
Waingereza wanasema, ‘no one perfect’, yaani hakuna binadamu mkamilifu. Hii ni sawa na kusema kwamba kila mtu ana uzuri na ubaya wake.
Ninaweza kuamini kuwa Rais Kikwete ni binadamu mwenye upungufu, lakini pia mwenye uzuri wa aina yake. Ni kiongozi anayejizatiti kuliletea Taifa letu maendeleo makubwa, ingawa baadhi ya wananchi ni wagumu kuukubali ukweli huu. Hao ndiyo wanaolazimisha kuita rangi nyeupe kuwa ni nyeusi!
Leo mtu mwenye akili timamu hawezi kuilinganisha Tanzania ya leo na ile ya enzi za Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi au ya Mzee Benjamin Mkapa. Simaanishi kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana nchini chini ya viongozi waliomtangulia Kikwete.
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Kikwete imeliwezesha Taifa letu kupiga hatua kubwa ya maendeleo, ambayo Watanzania hatuna budi kujivunia.
Kwa mfano, Rais Kikwete ameruhusu uhuru mkubwa kwa wanasiasa, wanaharakati na vyombo vya habari. Leo kila mwananchi ana uhuru wa kuikosoa Serikali na viongozi wake hadharani kwa kadiri anavyoweza. Haya ni maendeleo ambayo hayakupewa nafasi katika Serikali zilizopita. Wengi ni mashahidi wa hili.
Wakati fulani niliwahi kusema, na nitaendelea na msimamo huu, kwamba Rais Kikwete, pamoja na mambo mengine, atakumbukwa zaidi kwa uvumilivu wake mkubwa katika masuala ya siasa na utawala.
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa, wanaharakati na vyombo vya habari vimekuwa vikitumia mwanya huo kumchafua kwa kumzushia kashfa mbalimbali, kwa lengo la kujipatia umaarufu isivyo halali mbele ya jamii.
Tusikomee kwenye uhuru mkubwa wa kutoa mawazo uliopo. Kikwete anatajwa kuwa ndiye Rais wa Tanzania anayeongoza kwa kuomba misaada mbalimbali katika mataifa tofauti kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Lakini cha kushangaza ni kwamba baadhi ya Watanzania wamekuwa wakibeza jitihada hizo za kiongozi huyu wa nchi, kiasi cha kumwita ‘ombaomba namba moja’ katika Bara la Afrika.
Binafsi nimekuwa nikijiuliza kuwa hivi hao wenzetu wanaombeza Rais Kikwete kiasi hicho, wanadhani anakwenda nje ya nchi kupiga magoti kuomba misaada ya vyandarua na magari ya wagonjwa kwa ajili ya familia yake binafsi?
Je, ndiyo kusema wabezaji hao hawajui kwamba Rais Kikwete ana fedha za kujinunulia vyandarua vya kifahari na hata dawa za kujikinga na mbu na familia yake wasiwashambulie na kuwaambukiza malaria? Lakini pia wameshindwa kufahamu kuwa vyandarua, magari ya wagonjwa na misaada mingine anayoihangaikia nje ya nchi ni kwa ajili ya Watanzania wasiojiweza kiuchumi?
Watu wanasema nchi yetu ina rasilimali nyingi zinazotosha kugharamia maendeleo na kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Ni kweli, lakini tusisahau kuwa bado hazijaandaliwa ipasavyo kwa ajili ya kutumika ili ziboreshe maisha ya kila mwananchi.
Sasa basi, Serikali chini ya mwongozo wa Rais Kikwete, inaona kwamba haiwezi kuwaacha wananchi wake walio wengi waendelee kutaabika hadi rasilimali zilizopo zitakapojengewa mazingira ya kuwaboreshea maisha.
Ndiyo maana kiongozi huyu wa nchi pia amekuwa akikazania kujenga mazingira yanayovutia wageni kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini, kama hatua mojawapo ya kupunguza umaskini na kuinua uchumi wa Watanzania.
Ni kweli Rais Kikwete kama binadamu, ana upungufu wake kama vile kutofanya uamuzi mgumu dhidi ya viongozi wanaodhihirika kutapanya na kuhujumu rasilimali za nchi kwa maslahi yao binafsi.
Ni wazi pia kwamba hajasimamia kuhakikisha tamko la Serikali la kutoa elimu ya msingi bure linatekelezwa kwa vitendo nchini. Lakini kiukweli amejitahidi kwa kiasi kikubwa kufanikisha mambo mengi mazuri yenye manufaa makubwa kwa Taifa letu.
Waswahili wanasema, “Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.” Ni unafiki kusema kwamba Rais Jakaya Kikwete hajaliletea Taifa hili maendeleo yoyote. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Rais Kikwete amethubutu, ameweza, anastahili kupongezwa na ni mfano mzuri wa kuigwa.