Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umefanya hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu, ambapo aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Arch. Daud W. Kondoro, amemkabidhi rasmi Ofisi Mtendaji Mkuu mpya, FRV. Said Rajab Mndeme (ndc).
Hafla hiyo imefanyika Oktoba 15, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya TBA Jijini Dar es Salaam, kufuatia FRV. Mndeme mnamo Oktoba 13, 2026 kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mtendaji Mkuu wa TBA.
Akizungumza katika hafla hiyo, Arch. Kondoro amemshukuru Mhe. Rais kwa kumpa fursa ya kulitumikia Taifa kupitia TBA. Vilevile, ametoa shukrani kwa Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Ushauri, Menejimenti na watumishi wote wa Wakala kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake.
Arch. Kondoro ameeleza imani yake kuwa uongozi mpya utaendeleza mafanikio yaliyofikiwa, akibainisha kuwa FRV. Mndeme ana uzoefu wa ndani wa taasisi hiyo na ameshiriki katika maandalizi ya mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya TBA.
Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi iliyowekwa ili kuimarisha utendaji na kuongeza uwezo wa Wakala kujitegemea.
Kwa upande wake, FRV. Mndeme amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumwamini na kumteua kuiongoza TBA, akieleza kuwa uteuzi huo ni dhamana kubwa inayohitaji uwajibikaji, uadilifu na ushirikiano.
Pia, amempongeza Arch. Kondoro kwa mchango wake katika kuimarisha maendeleo ya Taasisi, hususan katika usimamizi wa Miliki za Serikali na kuongeza mapato ya ndani.
Aidha, ameahidi kuendeleza mipango na mikakati iliyowekwa kwa kushirikiana na Wizara, Bodi ya Ushauri, Menejimenti pamoja na watumishi wote, akilenga kuongeza mapato ya ndani, kuimarisha ufanisi na kupunguza utegemezi wa Ruzuku za Serikali.


