Mamia kwa maelfu ya wananchi, wamejitokeza na wanaendelea kujitokeza kulipa kodi ya majengo. Muda uliopangwa ulipungua. Umeongezwa kwa wiki kadhaa, lakini bado idadi ya watu wanaojitokeza kulipa ni kubwa mno.
Maombi ya wananchi ya kuomba kuongezewa muda yameitikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Muda wa malipo bila faini umeongezwa hadi Julai 31, mwaka huu.
Nchini kote kumeripotiwa misururu ya wananchi katika ofisi za TRA na benki mbalimbali. Kwa namna ya pekee, maelfu ya wananchi wamejihimu alfajiri na mapema kwenda TRA na katika benki kulipa kodi hiyo.
Hii ni habari njema mno. Ni mwamko wa aina yake. Ni ishara ya matumaini mapya ya kuijenga Tanzania kwa kutumia kodi zetu wenyewe. Hili si jambo la kutazamwa kwa wepesi kana kwamba ni la kawaida. Linaashiria mabadiliko makubwa ya kifikra miongoni mwa Watanzania. Kwa wazalendo wote, hili ni jambo la kujivunia.

Ulipaji kodi ni jambo halali. Nchi zote zilizoendelea, wananchi wake wanalipa kodi bila shuruti. Kinachogomba mara kadhaa ni wingi na ukubwa wa kodi. Kodi ikiwa ya kuhimilika wananchi huwa hawakaidi au kulazimishwa kuilipa.
Nyuma ya mwitikio huu wa ulipaji kodi ya majengo, kuna salamu mahsusi za wananchi kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Alimradi hatukuona kodi hii ikikusanywa kwa mtutu wa bunduki au kwa vitisho, itoshe tu kuamini kuwa mwitikio wa wananchi wenyewe umesukumwa na matumaini makubwa waliyonayo kwa Rais John Magufuli na Serikali anayoiongoza.
Kuna wakati tuliaminishwa kuwa Watanzania ni wagumu katika ulipaji kodi. Bila shaka mwitikio wa wananchi kwenye ulipaji kodi za majengo umejibu madai hayo na kuthibitisha pasi na shaka kuwa kilichokuwa kimekosekana kwa miaka mingi ni imani haba ya wananchi kwa viongozi na Serikali yao.

Watanzania wameanza kuwa na imani kuwa fedha zao za kodi zinakwenda kutekeleza mambo ya msingi yenye manufaa kwa Tanzania na Watanzania. Polepole, wanaanza kuamini kuwa kodi wanayolipa haiendi kutumiwa na genge la viongozi na wateule wao fulani, bali inatumika kufufua na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Watanzania sasa wanaamini kuwa kodi wanayolipa haitumiwi na rais na wasaidizi wake kwenda kutalii ughaibuni kwa kisingizio cha kwenda kushawishi wawekezaji au ‘kutangaza utalii’. Rais Magufuli anaelekea kutimiza miaka miwili madarakani. Kwa muda wote huo, amezuru Rwanda, Uganda, Kenya na Ethiopia. Safari hizi zina utetezi.
Katika hali ya kawaida tuliyoizoea, miaka hii miwili tungekuwa tumeshuhudia kiongozi wetu akiwa amezuru Marekani, Ulaya na Asia pengine kwa ziara zaidi ya 20. Matumizi haya mabaya ya fedha yangeweza kuhalalishwa na kauli dhaifu kama za ‘kwenda kujitambulisha’, ‘kujenga uhusiano’, ‘kujifunza’, na kadhalika.

Tumshukuru Mungu kuwa katika nchi yetu kumekuwapo usiri mkubwa mno wa matumizi ya fedha za umma yanayofanywa na viongozi wakuu. Kama ingekuwa Watanzania wakaambiwa kiasi cha fedha kinachotumiwa kwenye ziara moja ya rais katika nchi kama Marekani kwa muda wa wiki moja, naamini kungekuwa na maandamano na hata maafa! Kiasi cha fedha kinachotumika ni kikubwa mno.
Watanzania wanamwona Rais akiwa nchini akitumia muda mrefu kutafuta majawabu kwa kero zinazowakabili. Wanamwona Waziri Mkuu akihaha huku na kule nchini kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Wanamwona Makamu wa Rais akiwajibika bila kuchoka, na mara kadhaa akimwakilisha Rais nje; huku akiwa na idadi ndogo ya watu kwenye msafara wake.

Watanzania wameanza kuamini kuwa fedha za umma sasa zinafanya kazi za nchi kwa manufaa ya wananchi. Imani hiyo imekuwa kichocheo madhubuti kinachowasukuma na hata kuwafanya wakeshe kwenye foleni wakitaka kulipa kodi. Imani hiyo ndiyo inayowafanya Watanzania walilie kuongezwa muda wa kulipa kodi! Hili si jambo la kawaida hasa katika jamii ambayo tayari ubinafsi ulishatamalaki.
Nchi zote zilizoendelea zimefikia hatua hiyo kwa wananchi wake kutekeleza wajibu wao wa msingi – ukiwamo wa kulipa kodi. Mabakuli ya misaada tunayopitisha Marekani, Ulaya, Asia na kwingineko duniani yanajazwa na kodi za wananchi wa mataifa hayo. Haiwezekani Tanzania au Afrika ikapata maendeleo kwa kuendelea kuamini kwenye misaada.

Majirani zetu Kenya, ni mfano mzuri wa nchi zinazopiga hatua kimaendeleo kutokana na wananchi wake kulipa kodi. Hata pale ambako mataifa ya Magharibi yalipoinyima misaada, Kenya iliweza kusonga mbele kutokana na kodi za wananchi wake. Asilimia zaidi ya 90 ya bajeti ya Kenya inatokana na fedha za ndani. Sisi hapa ilifika hatua asilimia zaidi ya 50 tukawa tunategemea misaada.
Kama nilivyosema, mwitikio wa Watanzania kwenye ulipaji kodi ya majengo ni ishara njema ya imani ya wananchi kwa Serikali yao. Wananchi wameshaanza kuona thamani ya kodi wanayolipa. Lililo muhimu; imani hii ni vizuri ikadumu. Lakini haiwezi kudumu kama hawataona matokeo mengi mazuri na kwa kasi inayoleta matumaini.
Tunaweza kuwa wazuri katika kuikosoa, au hata kuishutumu Serikali ya sasa na zilizopita, lakini ukweli utabaki kuwa yapo mambo mazuri yaliyofanywa. Matumaini ya wananchi ni kuona hayo mazuri yakiendelea kubuniwa na kutekelezwa kwa kasi zaidi.

Wanataka kuona barabara zenye kiwango kinacholingana na thamani ya fedha wanazotoa. Hawataki kuona barabara kama zile za Kijitonyama, Makumbusho na maeneo mengine ambazo zinaharibika hata kabla ya kuzinduliwa.
Wananchi wanataka kuona dawa zinapatikana kwa wingi na kwa wakati kuanzia katika zahanati hadi kwenye hospitali zote nchini. Hawataki kuona hospitali za Serikali zikiwa hazina dawa, lakini zinazomilikiwa na watu binafsi zikawa nazo.
Pamoja na nia njema ya ulipaji kodi, bado kuna mlolongo na utitiri mkubwa wa kodi kuanzia Serikali za Mitaa hadi Serikali Kuu. Kero inakolezwa na ukubwa wa kodi zenyewe. Nadhani kinachopaswa kufanywa na Serikali ni kuwa na walipakodi wengi wanaolipa vizuri, badala ya utaratibu wa sasa wa wachache wanaolipa viwango vikubwa.

Utafiti uliofanywa na taasisi mbalimbali umebainisha kuwa ukubwa wa kodi ni miongoni mwa sababu zinazowafanya Watanzania wengi waamue kukwepa kuzilipa. Matokeo yake ni ongezeko la rushwa. Wingi na ukubwa wa kodi umewafanya wanaolipa wawe wachache, hasa walio kwenye mifumo rasmi. Hii ni kero inayopaswa kutazamwa kwa lengo la kuipatia ufumbuzi haraka. Sekta kama ya utalii yapo malalamiko kuwa kuna kodi zaidi ya 30! Kodi nyingine si kubwa, ila kero yake ni kuwa ni nyingi mno. Ndiyo maana inapendekezwa zikusanywe kwenye kapu moja kisha zigawanywe kwa wahusika!
Imani hulipwa kwa imani. Viongozi wa Serikali wameona namna wananchi walivyojitokeza kulipa kodi ya majengo. Inawezekana mwitikio ukawa hivyo kwa kodi na masuala mengine ya kimaendeleo. Jambo la muhimu ni kwa Serikali kuendelea na juhudi zake za kuboresha huduma za jamii.

Yanaweza kuwapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kwa sababu haya yanayofanywa sasa na Serikali yanaonekana mapya. Tunaweza kulaumu sasa, lakini ni vizuri tukatambua nia njema ya Serikali katika kusimamia maendeleo. Tushirikiane kuijenga Tanzania njema kwa vizazi vijavyo. Mwitikio wa wananchi kwenye ulipaji kodi ya majengo uwafumbue macho viongozi. Watambue kuwa Watanzania sasa wako tayari kushiriki kuijenga nchi yao. Hawana tena shaka na thamani matumizi ya kodi zao.

By Jamhuri