Waziri wa michezo wa Gabon ametangaza kupigwa marufuku kwa wachezaji wakongwe Pierre-Emerick Aubameyang na Bruno Ecuele Manga, kusimamishwa kwa timu nzima ya taifa, na kufutwa kazi kwa benchi la ukufunzi.

Hii ni kufuatia matokeo mabaya ya Gabon katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) linaloendelea Morocco. Matokeo ya timu ya taifa katika mashindano ya AFCON yalitathminiwa na Baraza la Mawaziri kufuatia kushindwa kwa 3-2 Jumapili na Msumbiji inayoorodheshwa katika nafasi ya 102 katika viwango vya FIFA, jambo lililomaanisha kwamba Gabon haikuweza kusonga mbele hadi hatua ya mtoano. Aubameyang alirudi katika klabu yake ya Ufaransa ya Marseille baada ya Gabon kuondolewa, kutokana na jeraha la paja.

Rais wa Gabon Brice Clotaire Oligui Nguema alizungumzia matokeo hayo akisema timu ya taifa inakabiliwa na matatizo mawili makubwa ambayo ni: ukosefu wa mbinu na mtawanyiko wa rasilimali. Rais huyo aliahidi kufanya “maamuzi imara na ya kimuundo” ili “kurejesha ukali, uwajibikaji na dhamira katika utawala wa michezo ya kitaifa”.

Hata hivyo, hilo linaweza kuiingiza Gabon matatani na shirikisho linaloongoza mpira wa miguu duniani FIFA, ambalo linapiga marufuku kuingilia kati kwa serikali katika masuala ya mashirikisho yake wanachama.