Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa uchunguzi huru wa vifo vya Wapalestina zaidi ya 30 vilivyotokea karibu na kituo cha kugawa misaada kinachoratibiwa kwa ushirikiano Marekani huko Gaza.
Wapalestina zaidi ya 30 waliuawa karibu na kituo hicho. Hii ni baada ya kikosi cha waokozi kudai kwamba vifo hivyo vilisababishwa na mashambulizi yaliyofanywa na Israel.
Katibu Mkuu huyo amesema kwenye taarifa yake kwamba amesikitishwa na mauaji hayo ya Wapalestina wa Gaza waliokuwa wakihangaika kupata msaada huko Ukanda wa Gaza. Akasema haikubaliki hata kidogo, kwamba raia hao wanayaweka hatarini maisha yao wakiwa wanatafuta chakula.
Guterres, akatoa wito wa uchunguzi wa haraka na ulio huru dhidi ya matukio hayo, na kuwawajibisha wahusika.
