Bilionea wa Marekani Bill Gates ametangaza leo Jumanne kwamba kiasi kikubwa cha mapato ya Wakfu wa Gates ya dola bilioni 200 kitatumika barani Afrika katika kipindi cha miongo miwili ijayo.
Gates, ambaye Mei 8 alisema kuwa ataufunga wakfu huo ifikapo mwaka 2045, ametoa ahadi hiyo alipokuwa akiwahutubia viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Amewaambia viongozi hao sehemu kubwa ya fedha hizo zitaelekezwa katika utatuzi wa changamoto barani Afrika, huku akiwahimiza kuimarisha sekta za afya na maendeleo kupitia ushirikiano na uvumbuzi.
Aidha aliyataja mataifa ya Ethiopia, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Zambia na Zimbabwe kama mifano ya nchi zilizoonyesha uongozi thabiti unaokuza uvumbuzi.
