Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati, imeeleza kuridhishwa na hatua kubwa ya maendeleo zilizofikiwa katika ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akizungumza wakati wa ziara ya siku moja iliyolenga kujifunza, kukagua, na kujionea maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo uliopo eneo la Chongoleani mkoani Tanga, Kamishna anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa uchumi wa nchi na ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Uganda.

“Tumeshuhudia kazi kubwa ikifanyika hapa, huu si mradi wa bomba tu, bali ni mrija wa uchumi utakaofungua fursa za biashara, ajira, na teknolojia mpya kwa vijana wetu” alisema Mwandisi Luoga.

Alisema ziara hiyo imeangazia kukagua eneo la ulazaji wa bomba la mafuta ambapo mpaka sasa eneo kubwa limekwishalazwa mabomba bado eneo dogo, anaamini ndani ya muda uliopangwa litakuwa limekamilika.

“Tumepitia na kukagua maeneo yote muhimu ya mradi huu, tumefurahishwa na kuridhika pamoja na taarifa ya mradi iliyotolewa imeoana na hali halisi ya mradi ulipofikia” alielezea Mhandisi Luoga.

Aidha Mwandisi Luoga alibainisha kuwa mradi huo umekuwa mkombozi kwa kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na fursa nyingine mbalimbali kwa jamii zinazozunguka mradi huo.

Miongoni mwa manufaa hayo ni pamoja na kutoa ajira elfu tisa kwa watanzania wenye ujuzi na wasio na ujuzi, kuboresha miundombinu ya vyuo mbalimbali vya ufundi stadi na kufadhili masomo kwa wanafunzi mbalimbali kwenye masomo ya Shahada, Shahada ya Uzamivu na mafunzo kwa vitendo katika nchi mbalimbali.

“ Sisi kama Serikali tunatoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo, huku tukiahidi kuendelea kusimamia mradi huo usiku na mchana ili ukamilike kwa wakati uliopangwa,” alisisitiza Mwandisi Luoga.

Kwa upande wake msimamizi wa maudhui ya ndani (Local content) kutoka EACOP, Bi. Neema Kweka amesema kuwa ziara hiyo ya Wizara imewapa hamasa na kuona namna ambavyo serikali wanatambua mchango wa EACOP katika kuzalisha fursa kwa jamii.

“Tunaendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba kati yetu na Serikali katika maeneo mbalimbali hususani kwa upande wa maudhui kwa wazawa kwani tayari mradi umeajiri zaidi ya Watanzania elfu Tisa”, alibainisha Bi. Kweka.

“Tunashukuru sana kupata ziara za namna hii ambazo zinatupa faraja, na nafasi ya kupokea changamoto zitakazo saidia kuboresha baadhi ya maeneo ya kiutendaji”, alisema Bi. Kweka.

Naye Mhandisi wa mradi kituo cha kupokea na kuhifadhia mafuta (terminal) eneo la Chongoleani, Musa Msafiri alisema kuwa kwa upande wa idara ya matanki ya mafuta wamefikia katika hatua za mwisho sawa na asilimia 94 ambapo yameshafanyiwa majaribio.

“Matanki mawili kati ya manne yamekamilika na yameshafanyiwa majaribio kwa kujaza maji hivyo basi matokeo yanaonesha uimara na ubora wa hali ya juu kuruhusu mafuta kuingia”, alisema Mhandisi Msafiri.

Aidha, Mhandisi Msafiri alibainisha kuwa mradi huo ni wa kisasa na umezingatia ubora wa kimataifa bila ya kuathiri mazingira.

Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.

Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.