Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

SERIKALI  imezitaka halmashauri zote nchini kuendelea kusimamia kikamilifu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 ili kuzuia uchimbaji wa mchanga kudhibiti kupanuka kwa mito huku ikiendelea kutenga fedha za kukabiliana na changamoto hiyo.

Sanjari hilo imezitaka halmashauri hizo kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira ili kudhibiti upanukaji wa mito na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Mhe. Askofu Dkt. Josephat Gwajima katika swali lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariamu Kisangi kuhusu lini ahadi ya kupeleka fedha za ujenzi wa mito iliyopanuka katika Jimbo la Kawe itatekelezwa. 

Akijibu swali hilo amesema Serikali inatambua changamoto ya kupanuka kwa mito iliyopo katika Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam ikiwemo Nyakasangwe, Tegeta, Mbezi, Mlalakuwa, Mpiji na Ndubwi inayotiriririsha maji yake katika Bahari ya Hindi. 

Aidha, Mhe. Khamis amefafanua kuwa kupanuka kwa mito hiyo ni kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kufanyika kwa shughuli za kibinadamu zisizo endelevu ndani ya mita 60 kinyume cha kifungu namba 57 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191. 

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, amesema Serikali itaendelea kutenga na kutafuta fedha kupitia Mifuko mbalimbali Mazingira ikiwemo Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi ya Kijani (GCF) pamoja na Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (AF) kwa ajili ya ujenzi wa mito hiyo.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis ameongeza kwa kusema kuwa Serikali itaanza ujenzi wa mito iliyopanuka katika Jimbo la Kawe kadri fedha zitakavyopatikana.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mariamu kuwa Serikali ina mpango gani wa dharula wa kunusuru nyumba zinazoanguka kutokana na mafuriko, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imejenga vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka maeneo korofi.

Ameongeza kuwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanza kuelimisha wananchi kuhusa athari za uchimbaji wa mchanga kando ya mito.

Halikadhalika, Mhe. Khamis ametumia wasaa huo kuwataka wananchi waache kujenga nyumba katika maeneo ambayo maji yanatuama pamoja na vyanzo vya maji pia wazingatie Sheria ya Mita 60.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha 16 Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 02 Mei, 2025.